1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiwango cha wasio na ajira kimepanda Marekani

Kalyango Siraj3 Oktoba 2008

Uchumi wa Ufaransa umedorora

https://p.dw.com/p/FTfF
Mshangao katika soko la Hisa Ujerumani la (DAX) Frankfurt.Picha: AP

Baraza la wawakilshi la Marekani linasubiriwa kupiga kura kuhusu mpango wa serikali uliofanyiwa marekebisho wa dola billion 700 wa kuunusuru mfumo wa fedha.

Lakini kuna wasiwasi kuwa huenda wabunge wa chama cha Democratic ambao jumatatu ya wiki hii waliuunga mkono mpango huo kuwa wanaweza wakaupinga mara hii kutokana na marekebisho yaliyofanywa.

Hayo yanatokea wakati kukitolewa onyo kuwa Ufaransa imekabiliwa na kudorora kwa uchumi.

Leo Ijumaa ndio siku muafaka kwa majaliwa ya mgogoro wa fedha wa Marekani.

Hii ni kwa sababu wabunge wa baraza la wawakilishi, ndio wanapiga kura kwa mara ya pili kuona kama muswada wa dola billioni 700 unahalalishwa baada ya kuukataa siku ya jumatatu.

Hatua ya jumatatu ilipelekea bei za hisa kuporomoka kwa kiwango kikubwa kuwahi kutokea katika masoko ya hisa ya Marekani kwa kipindi cha miaka 21.

Matumaini yapo ya muswada huo kupasishwa.Kiongozi wa wa demokrat waliowengi bungeni, Steny Hoyer,ana matumaini kuwa kutokana na hali tete ilioko na pia haja ya kuuweka sawa uchumi wao na kwa minajili ya wafanyakazi wote wa nchi hiyo,wabunge watauunga mkono.

Lakini kwa upande mwingine anasema kuwa baadhi ya wabunge ambao waliuunga mkono jumatatu,wanaweza wakaukataa mara hii kutokana na mageuzi yaliyofanywa.

Muswada mpya ulipambwa na kifungu cha dola billioni 150 za kutolipa kodi ili kuwashawishi wabunge wa vyama vyote,Republican na Democratic kuweza kuukubali.

Rais Bush jana aliongezea kauli yake ya kutaka muswada huo kupasishwa na baraza la wawakilishi akionya kuwa kazi za walala hoi ziko mashakani.

Kuna habari kuwa kiwango cha watu wanaopoteza kazi nchini Marekani kimeongezeka sana wakati huu ingawa ukosefu wa kazi umekuwa unaendelea kwa kipindi cha miezi tisa mfululizo nchini humo.

Na katika upande huu wa bahari ya Atlantiki, shirika rasmi la takwimu limeonya kuonya kuwa Ufaransa inakabiliwa na kudorora kwa uchumi.

Takwimu za shirika la kitaifa la Takwim la Insee Agency zinaonyesha kama uchumi wa Ufaransa ulididimia kwa 0.3% katika robo ya pili ya mwaka.Tena ljuma shirika hilo limetabiri kuwa zao ghafi la ndani yaani GDP, litashuka zaidi ya 0.1% nyingine katika robo zilizosalia za mwaka huu wa 2008.

Shirika linasema kuwa kiwango cha watu wasiokuwa na ajira nchini humo kimepanda hadi 40,000 mwezi wa Agosti,kiasi kikubwa kuwahi kutokea katika mwezi mmoja katika kipindi cha miaka 15 nchini humo. Aidha inatabiriwa kuwa ukosefu wa ajira unaweza ukapanda zaidi hadi asili mia 7.4 kutoka asili mia 7.2.katika robo ya tatu ya mwaka.

Jambo hilo huenda ndilo limemfanya waziri mkuu wa Ufaransa Francois Fillon kusema kuwa bara la ulaya ni lazima lipate ufumbuzi wa pamoja wa mgogoro wa kifedha unaoendelea ambao unavuruga uchumi wa mataifa mbalimbali.

Ameyatamka hayo katika mkesha wa mkutano wa viongozi wa mataifa manne yenye uchumi mkubwa katika Umoja wa Ulaya unaofanyika mjini Paris jumamosi.

Viongozi wa Ujerumani,Uingereza,Ufaransa pamoja na Italy wanakutana kujadilia mgogoro wa kifedha huku kukiwa na taarifa kuwa Ujerumani imepinga wazo la kuwepo mpango kama ule wa Marekani wa kunusuru mfumo wa kifedha wa Ulaya.