1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kizaazaa cha mchujo wa kufuzu kwa kombe la Mataifa ya Afrika 2013

27 Februari 2012

Mechi za mkondo wa kwanza za awamu ya mchujo ya kombe la Mataifa ya Afrika zitachezwa Jumatano tarehe 29. Kenya ni mwenyeji wa Togo, na tayari The Sparrow Hawks wako mjini Nairobi tayari kwa kivumbi hicho.

https://p.dw.com/p/14Aud
Timu ya taifa ya Togo
Timu ya taifa ya TogoPicha: AP

Kambi ya Harambee Stars imepigwa jeki na kuwasili kwa wachezaji nyota wao wanaocheza soka ya kulipwa ulaya. Macdonald Mariga anayecheeza FC Parma ya Italia na nahodha Dennis Oliech wa AJ Auxerre ya Ufaransa wamejiunga na wenzao katika kambi ya mazoezi. Victor Mugabe anayechezea Celtic ya Uskochi aliwasili Nairobi leo asubuhi. Kocha Francis Kimani anatarajiwa kukitaja kikosi kamili hapo baadaye. Mshambuliaji wa Tottenham Emmanuel Adebayor atakiongoza kikosi cha Togo.

Taifa Stars wana kibarua

Vijana wa Taifa Stars wa Tanzania nao wanaendelea kufanya mazoezi ya mwisho tayari kwa pambano lao dhidi ya Mambas wa Msumbuji. Mchuano huo utachezwa Jumatano jioni katika uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam.

Nao mchuano kati ya Rwanda na Nigeria umehamishwa kutoka uwanja wa Amahoro mjini Kigali hadi ule wa Nyamirambo. Kulingana na shirikisho la soka Rwanda, ni kuwa uwanja wa Amahoro unafanyiwa ukarabati kwa sasa.

Katika mechi nyingine Uganda Cranes watakuwa ugenini kupambana na Congo Brazaville. Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo itapambana na Ushelisheli. Zimbabwe itachuana na Burundi mjini Bujumbura, Namibia itaingia uwanjani dhidi ya Liberia mjini Monrovia, Malawi itapambana na Chad nao Gambia watafunga kazi dhidi ya Algeria.

Bayern yapata afueni

Katika ligi ya soka Ujerumani Bundesliga, mshambuliaji wa Borussia Dortmund Robert Lewandoski alifunga magoli mawili wakati mabingwa hao walipowarambisha Hanover 96 mabao matatu kwa moja katika mchuano wa jana. Ushindi huo uliisongeza zaidi Dortmund kileleni mwa ligi kwa tofauti ya pointi nne na kuendeleza ushindi wao kwa mechi saba mfululizo. Bayern Munich walisonga katika nafasi ya pili wakiwa na alama 48 kutokana na mechi 23 baada ya kuwalaza Schalke magoli mawili kwa nunge huku Mfaransa Frank Ribery akiyafunga magoli yote mawili. Bayern wako pointi moja mbele ya Borussia Moenchengladbach iliyotoka sare ya kufungana goli moja na Hamburg SV siku ya Ijumaa. Schalke 04 wanasalia katika nafasi ya nne na alama 44. Rais wa klabu ya Bayern Uli Hoeneß

Bayern iliifunga Schalke 4-0
Bayern iliifunga Schalke 4-0Picha: dapd

Katika ligi ya Uingereza, Manchester United iliishinda Norwich magoli mawili kwa moja jana Jumapili. Hiyo ilikuwa mechi ya 900 ya mchezaji Ryan Giggs kuichezea United na akafunga bao la ushindi baada ya Paul Scholes kufunga bao la kwanza. Ushindi huo uliwaweka Man United nyuma ya viongozi Manchester City kwa na tofauti ya pointi mbili, baada ya City kuwanyuka Blackburn Rovers magoli matatu bila jawabu. Nambari tatu Tottenham Hotspurs walinyamazishwa na Arsenal baada ya kulishwa mabao matano kwa mawili.

Liverpool yamaliza ukame wa mataji

Wakati huo huo Liverpool walimaliza ukame wa mataji kwa miaka sita baada ya kushinda kombe la Carling kwa mara ya nane walipowashinda timu ya Cardiff mabao matatu kwa mawili kupitia mikwaju ya penalty. Hii ni baada ya timu zote mbili kufungana magoli mawili katika muda wa ziada. huyu hapa Gerrad

Kabla ya kwenda kunyanua kombe la Carling, uwanjani Wembley, nahodha wa Liverpool Steven Gerrard alimpa pole binamu yake Antony Gerrard, ambaye aliipoteza penalti iliyowapa Liverpool ushindi dhidi ya klabu yake Cardiff.

Tukielekea nchini Uhispania, Lionel Messi alifunga bao kupitia mkwaju wa freekick na kuisaidia Barcelona kusajili uhsindi wa magoli mawili wka moja dhidi ya Athletico Madrid. Naye Christano Ronaldo alifunga bao safi la kisigino na kuwapa real ushindi wa goli moja kwa nunge dhidi ya Rayo Vallecano. Ushindi wa vilabu hivyo viwili uliendelea kuwapa Real uongozi wa tofauti ya pointi kumi kileleni mwa ligi mbele ya Real Madrid.

Real Madrid inaongoza ligi mbele ya Barcelona
Real Madrid inaongoza ligi mbele ya BarcelonaPicha: dapd

Na hatimaye, katika mechi za euro 2012, timu zote 16 zitakazoshiriki fainali za hizo kule Poland na Ukraine zitacheza mechi za kujipima nguvu Jumatano hii tarehe 29.02.2012. Stuart Pierce ataiongoza timu ya Uingereza kama kaimu kocha katika mchuano dhidi ya Uholanzi uwanjani Wembley. Naye kocha Joachim Loew atakuwa nyuma ya timu yake ya Ujerumani dhidi ya Ufaransa mjini Bremen.

Katika mechi nyingine Ireland itacheza dhidi ya Jamuhuri ya Czech, Poland watakutana na Ureno, Denmark itakabiliana na Urusi huku nayo croatia ikipambana na Sweden. Uhispania itacheza na Venezuela, Italia itakuwa mwenyeji a Marekani huku Ugiriki ikipimana nguvu na Ubelgiji. Ukraine itafunga kazi dhidi ya Israel.

Masaibu yamzidi Gebrselassie

Mwanariadha Michael Kipyego wa Kenya alimpita Haile Gebrselassie wa Ethiopia kukiwa kumesalia kilomita nne na kushinda mbio za Tokyo Marathon huku akiandikisha ushindi wake wa kwanza katika taaluma yake. Gebrselassie aliziongoza mbio hizo kwa kilomita 36 lakini Kipyego aliongeza kasi na kumpita katika kilomita ya 38 na kuuvuka utepe kwa muda wa saa mbili, dakika saba na sekunde 37. Mjapan Arata Fujiwara alimaliza wa pili kwa muda wa saa mbili, dakika saba na sekunde 48 akifuatwa katika nafasi ya tatu na Stephen Kiprotich wa Uganda kwa muda wa saa mbili, dakika saba na sekunde hamsini.

Gebrselassie aliyemaliza wa nne kwa muda wa saa mbili, dakika nane na sekunde 17 alikuwa akilenga kujipa nafasi katika kikosi cha Ethiopia kitakachoshiriki mashindano ya olimpiki ya London lakini alihitaji kukimbia chini ya muda wa saa mbili na dakika nne ili kuimarisdha nafasi zake.

Mwanariadha Haile Gebrselassie na Paul Tergat
Mwanariadha Haile Gebrselassie na Paul TergatPicha: picture-alliance/dpa

Gebrselassie mwenye umri wa miaka 38 amekuwa na matatizo katika mashindano ya hivi karubuni, huku akikosa kumaliza katika mbio za New York Marathon mwaka 2010, na kushindwa kuanza mbio za Tokyo Marathon mwaka jana baada ya kuumia akiwa mazoezini.

Katika kitengo cha kina dada, Mu Ethiopia Atsede Habtamu alimaliza wa kwanza kwa muda wa saa mbili dakika 25 na sekunde 32 mbele ya mwenzake Yeshi Esayias. Mkenya Helena Kirop alimaliza wa tatu katika mbio hizo za Tokyo.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/DPA

Mhariri: Abdul-Rahman Mohammed