1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kizungumkuti katika uchaguzi wa Zimbabwe

Miraji Othman7 Aprili 2008

Uamuzi bado haujafikiwa kuhusu uchaguzi wa urais wa Zimbabwe.

https://p.dw.com/p/Ddgw
Kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC katika Zimbabwe, Morgan TsvangiraiPicha: picture-alliance/ dpa

Mahakama ya ncvhi hiyo iliahirisha kutoa uamuzi juu ya kutangazwa matokeo hayo. Hata hivyo, vita vya neva juu ya nani aliyeshinda hasa kuwa rais wa nchi hiyo bado vinaendelea.

Wakati wananchi wa Zimbabwe, ikiwa leo ni siku ya nane tangu kwenda katika vituo vya uchaguzi kuamua nani wawe wabunge na rais wa nchi yao, wakiwa bado hawajuwi nani washindi, rais wa nchi hiyo, Robert Mugabe, bado ana'gan'gania madaraka. Ijumaa ililiopita aliteuliwa na kamati ya kisiasa ya chama chake cha ZANU-PF ajimwage tena kwenye kinyanganyiro kingine cha mchuano baina yake na kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC, Morgan Tsvangirai. Lakini kuna alama ya mapambano hapo baadae, kwani wapiganaji wa Mugabe , wale wanaoitwa wapiganaji wa zamani wa vita vya ukombozi, na pia wanamgambo vijana wanajipanga upya. Mwishoni mwa wiki, kwa mara ya kwanza mashamba yalitwaliwa. Chama cha wakulima kiliripoti kwamba kulitokea visa vitano vya aina hiyo, lakini baada ya muda majeshi ya usalama yaliingilia kati. Hapo kabla Robert Mugabe aliwataka Wa-Zimbabwe wailinde ardhi yao na wasikubali ardhi hiyo irejee katika mikono ya Wazungu; wasikubali kurejea nyuma katika mapambano kwa ajili ya ardhi.

Kuna vita vya kupimana nguvu hivi sasa baina ya upinzani na utawala wa Robert Mugabe. Kwa mara ya pili chama cha upinzani cha MDC kiliilazimisha mahakama itangaze mara moja matokeo ya uchaguzi; lakini mbio hizo za upinzani ziliishia sakafuni, bila ya kufanikiwa. Mahakama ilisema itaamua jambo hilo leo. Wakati huo huo, chama tawala cha ZANU-PF kiliiomba tume ya taifa ya uchaguzi iahirishe zaidi kutangaza matokeo, na kikataka kura zihesabiwe upya katika baadhi ya wilaya.

Inasemakana katika wilaya nne za uchaguzi kumetokea makosa ya kuhesabu kura, na makosa hayo yanaweza yakaathiri matokeo. Lakini upande wa upinzani unahisi umeshinda kwa haki katika uchaguzi huo, na umekasirishwa na hatua hiyo ya serekali. Kuhesabiwa upya kura ni jambo la kuchekesha ilivokuwa bado hakujatolewa matokeo rasmi.

Ni kazi ya Tume ya taifa ya uchaguzi kutangaza juu ya hitilafu zilizotokea katika kuhesabiwa kura, na sio kazi ya Chama cha ZANU-PF; hivyo yaonesha Chama cha ZANU-PF cha Robert Mugabe kinafuata njia ilio ya hatari. Kila pale kinaporefusha muda wa kuweko mzozo huo, ndipo utawala huo unapozidi kupoteza imani ya wananchi. Hivyo ndivyo alivoonya mwanachama muasisi wa Chama cha MDC, Grace Nkwenje.

Pia afisa wa Chama cha MDC, Arman Ndlovu, alisema:

+Mugabe amezoea kutumia nguvu. Sisi tunajuwa kwamba yeye anajuwa kwamba watu wanafikia kiwango ambacho hawawezi kukubali tena mambo yalivyo; hapo watu watakasirika na kuanzisha fujo, jambo ambalo tunawahimiza watu wetu wasifanye; tena atangaze sheria ya hali ya hatari, atatumia jeshi kuwatisha watu; hicho ndicho hasa anachotaka kitokee.+

Upinzani unamlaumu Robert Mugabe kwamba yeye hatua kwa hatua anajaribu kufanya ujanja wa kuielekeza nchi hiyo katika sheria ya hali ya hatari, na mkuu wa Chama cha MDC, Morgan Tsvangirai, amesema kwamba Robert Mugabe tangu hapo ameshatangaza vita dhidi ya wananchi, na akaiomba jamii ya kimataifa iwasaidie watu wa Zimbabwe. Pia Morgan Tsvangira ametoa mwito kwa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, lizuwie kutoa msaada wa dola bilioni moja kwa Zimbabwe hadi pale Robert Mugabe atakapokubali kuacha madaraka. Pia ameitaka Afrika Kusini, Uengereza na Marekani zizidishe mbinyo kwa Mugabe ili akubali kwamba ameshindwa. Rais Thabo Mbeki, amelikataa jambo hilo. Mbeki anasema hali imedhibitiwa huko Zimbabwe.

Na habari zinasema kwamba jana jioni kiongozi wa MDC, Morgan Tsvangiraia, alikwenda Afrika Kusini kukutana na walioelezewa watu muhimu. Lakini hakujatolewa maelezo zaidi.