1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Klopp kuihama Borussia Dortmund

Admin.WagnerD16 Aprili 2015

Habari ambazo zimewashangaza sana wapenzi wa kandanda siyo tu Ujerumani bali ulimwenguni, ni tangazo la kocha wa Borussia Dortmund Juergen Klopp kuwa ataondoka klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu

https://p.dw.com/p/1F8vz
Deutschland Jürgen Klopp BVB PK Abschied
Picha: picture-alliance/dpa/F. Gambarini

Klopp ameyasema hayo leo katika kikao cha waandishi wa habari wakati kukiwa na ripoti kuwa aliyekuwa kocha wa Mainz Thomas Tuchel huenda akaijaza nafasi hiyo.

Kocha Jurgen Klopp ataondoka Borussia Dortmund mwishoni mwa msimu huu licha ya kuwa mkataba wake unakamilika mwaka wa 2018. Klopp amesema hajihisi tena kuwa mtu anayestahili kuiongoza klabu hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, akiwa pamoja na wakubwa wa klabu hiyo Hans-Joachim Watzke na Michael Zorck, Klopp amesema “Dortmund inastahili mabadiliko”.

Dortmund wamekuwa na matokeo yasiyoridhisha katika ligi ya Bundesliga msimu huu, hata baada ya Klopp kuiongoza klabu hiyo kutwaa mataji ya mwaka wa 2011 na 2012. Klopp mwenye umri wa miaka 47, alichukua uongozi wa BVB mwaka wa 2008 na kando na mataji ya Bundesliga, alishinda Kombe la Shirikisho la Kandanda Ujerumani – DFB, akapambana na Bayern Munich katika kuitawala Bundesliga na pia akatinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka wa 2013. Na hajaandika tu historia katika klabu ya BVB, bali pia amechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kandanda la Ujerumani. Na ndio maana Afisa Mkuu wa BVB Hans-Joachim Watzke amemshukuru kwa mchango wake

Hans-Joachim Watzke und Jürgen Klopp
Afisa Mkuu Mtendaji wa Borussia Dortmund Hans-Joachim Watzke akiwa na kocha Jürgen KloppPicha: picture-alliance/dpa/F. Gentsch

Klopp amekuwa mpenzi wa mashabiki wengi wa klabu hiyo, kwa kuisadia kuirejesha BVB katika kiwango cha juu katika Bundesliga na Ulaya, akitumia mfumo wa kusisimua wa kandanda la kushambulia kwa kasi. Klopp alichukua usukani wakati Dortmund ilikuwa ukingoni mwa kufilisika na akasaidia ukuaji wake wa kifedha. Dortmund kwa sasa wako katika nafasi ya kumi katika Bundesliga wakati zikisalia mechi sita msimu kukamilika. Wamefuzu katika nusu fainali ya Kombe la DFB Pokal, na hiyo ndio nafasi yao nzuri ya kucheza Champions League msimu ujao.

Hivyo, basi, ni nani anayeweza kuchukua nafasi yake? Maafisa wa klabu wamesema hawatazungumzia watu wanaoweza kujaza pengo hilo, kwa sababu ya heshima waliyo nayo kwa Klopp. Lakini ripoti za magazeti ya Ujerumani zinasema aliyekuwa kocha wa Mainz, Thomas Tuchel ndiye anayepigiwa upatu kuvivaa viatu vyake.

Na bila shaka kuna uvumi unaoenea kwa sasa kuhusu klabu anayoweza kujiunga nayo Klopp. Wengi wanasema Manchester City huenda likawa chaguo bora kwake kwa sababu hatma ya Manuel Pellegrini inatiliwa mashaka kutokana na kuyumba kwa mabingwa hao wa Uingereza. Pelelgrini amesalia na mwaka mmoja kwenye mkataba wake. Klopp pia amehusishwa na Real Madrid na itasubiriwa kuona uamuzi atakaofikia msimu ujao.

Lakini, huyu Klopp unamjua kama mtu wa aina gani? Mimi ukiniuliza ntakwambia kuwa namfahamu kuwa mtu mcheshi, mwenye mafumbo, mapenzi tele na mwepesi wa kuzungumza naye ndani na nje ya uwanja. Wakati mwingine lakini anaweza kupandwa na hasira na kuwafokea marefa na maafisa wasimamizi wakati wa mechi. Tuandikie kwenye ukurasa wetu wa Facebook, unavyomjua kocha huyu….

Mwandishi: Bruce Amani/reuters
Mhariri:Gakuba Daniel