1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la dunia 2010

9 Septemba 2009

Ujerumani ina miadi leo na Azerbaijan huko Hannover

https://p.dw.com/p/JYlW
Kocha Löew na nahodha BallackPicha: AP

Kinyanganyiro cha kufuzu kwa Kombe lijalo la dunia 2010 nchini Afrika Kusini, kinaendelea jioni hii tena katika kanda zote: Ujerumani, ina miadi mjini Hannover na Azerbaijan ikijua wazi haimudu kupoteza pointi 3 kabla ya changamoto yake ya Oktoba 10 ya kufa-kupona na Russia itakayoamua nani anakwenda Afrika kusini kati yao.

Mabingwa wa dunia Itali, wanatazamiwa leo nao kuondoka na tiketi yao ya Afrika kusini mradi tu, wanaishinda Bulgaria. Hatima ya Argentina,Ufaransa na Ureno haijulikani . Je, Kombe lijalo la dunia, litachezwa bila stadi wa Argentina Lionel Messi ? Stadi wa Ureno Cristiano Ronaldo au a Franck Ribery wa Ufaransa?

Kikosi cha Ujerumani kikiongozwa na nahodha wake Michael Ballack ,kitamtegemea tena stadi wao mpya na chipukizi wa asili ya kituruki, Mesut Özil kuvunja ngome ya wa-Azerbaijan ambao kiroja cha mambo wanaongozwa na kocha wazamani wa taifa wa Ujerumani,Berti Vogts.Baada ya mchezo wake maridadi dhidi ya Afrika kusini Jumamosi iliopita,macho ya mashabiki wa Ujerumani yanamkodolea Özil jioni hii ili kuhakikisha ushindi. Usoni kabisa,Özil atasaidiwa na washambulizi wenzake akina Gomez,Schweinsteiger na Podolski.

Kipa ni yule yule Rene Adler alielinda maridadi kabisa lango la Ujerumani ilipocheza majuzi na Bafana Bafana.Mahasimu wakubwa wa Ujerumani katika kundi hili la 4-Urusi inacheza leo na Wales wakati Liechtenstein inaumana na Finnland.

Kundi la kwanza linakodolewa macho katika mpambano kati ya Ureno inayoongozwa na nahodha wao Christiano Ronaldo na Hungary.Ureno lazima ishinde leo ama sihivyo,itaula na chua kwa uvivu wa kuchagua.Mabingwa wa Ulaya -Spain wanaeza leo kukata tiketi yao ya Kombe la dunia wakitamba dhidi ya Estonia iliokwishapigwa kumbo,mradi tu mahasimu wao Bosnia watashindwa kuwatoa waturuki.

Ufaransa,mabingwa wa dunia 1998 ni timu nyengine ilio mashakani na leo inacheza na Serbia ugenini.Tayari kumezuka mfarakano kati ya kocha Domenech na nahodha Thiery Henry aliekosoa mbinu za kocha wake.England au Uingereza kama Serbia yaweza leo kutia mfukoni tiketi yake ya Kombe la dunia ikishinda nyumbani dhidi ya Croatia.

Katika kanda ya Amerika Kusini,ambako Brazil imeshakata tiketi yake mwishoni mwa wiki ilipoikomea Argentina mabao 3:1, leo ni zamu ya kikosi cha Maradona kujiokoa na balaa la kupigwa kumbo.Argentina ina miadi na Paraguay wakati Brazil na Chile.

Uruguay, mabingwa wa kwanza kabisa wa dunia lilipoanzishwa Kombe hilo,1930 ina miadi leo na Colombia wakati Venezuela inacheza na Peru.Ni Timu 4 tu kutoka kanda hii zinazoingia moja kwa moja katika Kombe la dunia. Timu ya 5 inabidi kucheza na ile ya kanda nyengine kuania nafasi hiyo.

Kanda ya Asia-Saudi Arabia inaikaribisha nyumbani Riadh, Bahrain wakati Simba wa nyika -Kamerun wanamalizana na Gabon kufuatia ushundi wao wa majuzi wa mabao 2:0 mjini Libreville.

Muandishi: Ramadhan Ali

Mhariri: Abdul-Rahman