1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la dunia la wanawake

Ramadhan Ali1 Oktoba 2007

Ujerumani imetwaa kwa mara ya pili mfululizo kombe la dunia la wanawake.Dimba la akina dada limepiga hatua gani ?

https://p.dw.com/p/CHav

Mwishoni mwa wiki,timu ya Taifa ya wanawake ya Ujerumani iliizaba Brazil mabao 2:0 mjini Shanghai,China na kutetea ubingwa wake.

Dimba la wanawake ambalo kitambo halikuwa likitiwa maanani na kupata mashabiki sasa limeanza kutambuliwa.

Nchini China tumejionea mashindano ya kusisimua kabisa ya kombe la dunia .Neno wanawake, tuliweke hapa upande tena makusudi.Walichofanya wanawake wa Ujerumani kutwaa mara 2 mfululizo kombe la dunia, hata timu yao ya wanaume haikufanya.

Timu 16 za wasichana zilizoteremka uwanjani nchini China kuania kombe hilo zimebainisha wazi sasa limeanza kukomaa na limevunja ungo.Limeonesha ufundi mkubwa wa kusakata dimba .

Kwani, mchezo wa dimba wa wanawake hii leo ni wa kasi na hauna ngware nyingi kama ule wa wanaume.Ni wazi kwamba ule wa wanaume ni wa kasi zaidi na nguvu zaidi.

Kwa kadiri gani dimba la wanawake limepiga hatua mbele tangu 1989 pale timu ya Ujerumani ilipoania kombe la Ulaya nakuchekwa, imeonekana huko China.Kwani leo kila mchezaji wa timu hii bingwa anajipatia kitita cha Euro 50.000.

Isitoshe, uwanjani walifika jumla ya mashabiki kiasi cha 40.000 kila mchezo na huu ni ushahidi wa ushabiki wa dimba la wanawake.

Na wakati kombe la dunia kama hili 1999 nchini Marekani lilioneshwa na vituo 67 tu vya TV,mara hii nchini China vituo 220 vya TV vilionesha .Isitoshe, kiwango cha watazamaji nchini ujerumani mara hii kiliongezeka mno.

Kombe la dunia nchini china limetembeza dimba la wanawake duniani.uamuzi kutoka Brazil kuanza sasa kuanzisha mfumo wa ligi ya wanawake ni hatua ya kwanza ya kuendeleza zaidi dimba la akina dada.

Ikiwa dimba la wanawake katika nchi nyengine limeendelea kuzorota na kutokuwa na wachezaji wa kutosha, sababu ni upungufu wa viwanja na zana kwa timu za wanawake.

Kwani, daraja ya dimba kwa klabu iko chini ukilinganisha na ile tuliojionea kwa timu za taifa.

Kwahivyo, itapasa kuzingatia barabara iwapo kombe lijalo la dunia 2011 liwe la timu 16 kama sasa huko China au liingize timu 24.

Kombe hili la dunia lilikuwa pia ni majaribio kwa michezo ijayo ya olimpik 2008 mjini Beijing.

Majaribio hayo kutokana na ushabiki uliooneshwa huko yamefuzu.

Lakini kumekuwapo jambo moja lilokera huko China:

Timu zimelalamika kufanyiwa ujasusi wa kimichezo,kukodolewa macho na kuchunguzwa tena mfululizo tangu wachezaji na hata waandishi habari wa kigeni .Wakihisi hata vyumbani wakisikizwa wasemayo.Hapo ingepasa kuwasihi wenyeji machina ,kuacha mtindo huo ikiwa hawataki kuzusha kashfa kubwa wakati wa michezo ya olimpik ya mwakani.