1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la Ujerumani

20 Mei 2011

Matumaini ya Schalke dhidi ya Duisburg ni yapi?

https://p.dw.com/p/11Kcw
Msema kweli ni yupi?Picha: picture-alliance/DW-Montage

Katika kuuhitimisha msimu wa soka Ujerumani, timu ya Schalke 04 inatafuta kumaliza kwa kujishindia taji la tano la Kombe la Ujerumani, dhidi ya timu iliopo kwenye divisheni ya pili, Duisburg.

Schalke inaonekana kuwa na nafasi nzuri dhidi ya timu hiyo, ilioanguka katika nafasi ya nane kwenye divisheni hiyo ya pili, na ambayo inawakosa wachezaji wake mahiri kutokana na maumivu walionayo, katika mechi ya leo uwanjani Olympic Stadium mjini Berlin.

Inafahamika kuwa Schalke kwa upande wake imefungwa mara sita msimu huu katika ligi ya Bundesliga na mashindano ya kuwania ubingwa Ulaya na imemaliza katika nafasi ya 14 katika taji la nyumbani, mwaka mmoja baada ya kuwa mshindi wa pili kwenye ligi hiyo.

Schalke inatazamia hii leo kulinyakuwa taji hilo na kipa Manuel Neuer anayewaniwa na timu ya bavaria, Bayern Munich, anatarajia kujinyakulia taji lake la kwanza na Schalke tangu ajiunge nayo mnamo mwaka 1991. Neuer anatazamiwa kuihama timu hiyo mwakani.Kocha wa Schalke Ralf Rangnik akizungumzia mpambano wa huo alisema kuwa sio wa rahisi na ungekuwa rahisi iwapo wangefanikiwa katika michezo yao ya mwisho ya ligi na ndio sababu ni lazima wajaribu.

Manuel Neuer Pressekonferenz Abschied Schalke 04
Kipa wa Schalke 04 Manuel Neuer.Picha: dapd

Nafasi ya Schalke ni kubwa hii leo kulinyanyuwa taji hilo, kutokana na kuwa timu pinzani Duisburg, inawakosa wachezaji wake wakuu kama vile Kapteni Srdjan Baljak, na mlinzi Julian Koch, huku naye pia mchezaji wa kiungo cha kati, Jurgen Saeumel anakosekana kwa kuumia msuli wa paja, na Bruno Soares kutoka Brazil amesitishwa kucheza.

Duisburg kwa upande wake inawania kulishinda kwa mara ya kwanza taji hilo baada ya kujaribu mara nne sasa.

Je ndoto hii itakuwa kweli?

Kwengineko timu nyengine za Ujerumani zipo katika awamu ya uhamisho na usajili wa wachezaji wapya, ili kujiimarisha kwa msimu unaokuja.

Wakuu wa timu ya Bayern Munich, wameamuwa kukaa na mashabiki sugu wa timu hiyo kujadili uendeshaji wa shughuli katika timu hiyo wakitafuta kujifunza kutokana na msimu huu uliokwisha pasi kunyakuwa taji lolote.

Bayern ilimaliza katika nafasi ya tatu kwenye Bundesliga kwa hiyo ni lazima ishiriki mechi ya marudio mwanzoni mwa msimu ujao, kuwania nafasi katika mashindano ya kuwania ubingwa Ulaya. Na pia mashabiki wa timu hiyo walilalama karibu mwishoni mwa msimu huu uliokwisha, kwa namna jinsi timu hiyo inavyoendeshwa.

Uli Hoeness Arjen Robben Karl Heinz Rummenigge Mark van Bommel Louis van Gaal FC Bayern Muenchen Empfang Double Feier
Picha: AP

Mkurugenzi mkuu wa timu hiyo ya Bavaria, Karl Heinz Rummenige amesema hatua hii ni kuwapa nafasi mashabiki wa timu hiyo katika meza ya mzunguko, kuwasiliana moja kwa moja na maafisa na wachezaji wa timu hiyo.

Rummenige alitaja tukio lililotokea Eintracht Frankfurt ambapo mashabiki walilipiga mawe basi la timu hiyo na kuuvamia uwanja baada ya timu hiyo kuondolewa kwenye timu kuu za Ujerumani kwenye matokeo ya msimu uliokwisha.Rummeinge alisema kuwa tukio kama hilo halipaswi kutokea kwenye timu ya Bayern.

Mwandishi: Maryam Abdalla/Rtre/Afpe/Ape
Mhariri:Abdul-Rahman