1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongamano la kimataifa la vyombo vya habari lafanyika mjini Bonn

27 Juni 2012

Mkutano wa kimataifa wa Vyombo vya Habari unaoandaliwa kila mwaka na Deutsche Welle limeanza hapa Bonn tangu tarehe 25-27.2012, mada kuu ni "Dhima ya Elimu, Utamaduni na Vyombo vya Habari katika Kujenga Dunia Endelevu".

https://p.dw.com/p/15LyA
Dr.Reinhard Hartstein akifungua Kongamano la Global Media Forum
Dr.Reinhard Hartstein akifungua Kongamano la Global Media ForumPicha: DW

Mkutano huu wa siku tatu unahudhuriwa na washiriki 1,800 kutoka mataifa, taasisi na vyombo vya habari 127 duniani kote, ambapo jumla ya mijadala 50 inaendeshwa katika jengo la zamani la Bunge la Ujerumani, kando kidogo ya jengo la Deutsche Welle.

Mapema akifungua mkutano wenyewe, Naibu Mkurugenzi Mkuu na Mkurugenzi wa Utawala wa Deustche Welle, Dkt. Reinhard Hartstein, alisema kwamba elimu ni haki ya kila mtu na ndio msingi wa maendeleo ya kila taifa ulimwenguni, na hivyo kuna haja kubwa ya vyombo vya habari kutumia nafasi yao kuhakikisha haki hiyo inapatikana.

"Iwe mataifa yaliyoendelea au yanayoendelea, iwe mashariki au magharibi, malezi, utamaduni na elimu ni ufunguo wa maingiliano mema, maendeleo endelevu na ustahamilivu baina ya tamaduni mbalimbali."

Miongoni mwa mada zilizojadiliwa leo ni "nafasi ya vyombo vya habari katika ulimwengu unaofuata soko na haja ya kupigania elimu kwa wote", ambapo Prof. Franz Josef Radermacher wa Taasisi ya Taaluma ya Ujerumani, alionya juu ya kutumika vibaya kwa vyombo vya habari vya kimataifa na makampuni makubwa duniani, badala ya kuwakomboa wanyonge.

Kwa ujumla mada zote zilizowasilishwa leo zimehusu kwa njia moja ama nyengine, dhima ya vyombo vya habari katika kuutengeza ulimwengu endelevu. Donald Mziray ni mshiriki kutoka Tanzania:

Kila mwaka Deutsche Welle hutayarisha jukwaa hili la kimataifa kwa minajili ya kuwakutanisha wadau wa sekta ya habari ulimwenguni, kuchangiana mawazo na kufanya maamuzi ya namna bora zaidi ya kutekeleza wajibu wao. Mkutano wa mwaka huu, unafadhiliwa pia na Mfuko wa Majadiliano Kati ya Tamaduni wa Benki ya Sparkasse, Wizara ya Mambo ya Nje, Mfuko wa Maendeleo wa Ulaya, serikali ya North-Rhine Westphalia, mji wa Bonn, Shrika la Posta la Ujerumani, wizara ya ushirikiano wa maendeleo ya Ujerumani Wakfu wa Fritz Thyssen.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DW Bonn

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman