1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongamano la tano la kimataifa kuhusu ukimwi kuanza Jumapili Afrika Kusini

Charo Josephat17 Julai 2009

Hali ya wagonjwa wa ukimwi Ujerumani si nzuri licha ya matibabu mazuri

https://p.dw.com/p/Irii
Mgonjwa wa ukimwi Amelia Radebe akiwa nyumbani kwa dadake huko Soweto Afrika KusiniPicha: picture-alliance / dpa/dpaweb

Kongamano la tano la kimataifa kuhusu ukimwi linaanza hapo kesho Jumapili mjini Capetown, Afrika Kusini. Mkutano huo wa siku tatu unawaleta pamoja wajumbe na wataalm kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni. Mkutano huo unafanyika wakati ambapo hapa Ujerumani maisha ya waathiriwa wa ukimwi na watu wanaoishi na virusi vya HIV sio rahisi.

Mji wa Captown nchini Afrika Kusini ni mahala panapofaa kufanyia kongamano la kimataifa kuhusu ukimwi kwani idadi kubwa ya watu milioni 40 ulimwenguni walioambukizwa virusi vya ukimwi wanatokea barani Afrika. Hali ya kimaisha ni mbaya kwani kunakosekana dawa za kupunguza makali ya ugonjwa wa ukimwi na matibabu yanayofaa kuwasaidia kuendelea na maisha ya kawaida.

Mkutano wa Capetown unaelezwa kuwa mkubwa wa kisayansi kuhusu matibabu, dawa na kuzuia kuenea kwa maambukizi ya ukimwi. Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano na asasi isiyo ya kiserekali nchini Afrika Kusini, Dira Sengwe, ambayo huandaa mfululizo wa mikutano hiyo nchini humo.

Kongamano hilo ambalo, kwa kawaida, hufanyika kila baada ya miaka miwili, huwavutia wajumbe takriban 5,000 kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni kote. Ni nafasi muhimu kwa wanasayansi, madaktari, watalaam wa afya ya umma na viongozi wa kijamii, kuchunguza maendeleo mapya kuhusiana na tafiti za virusi vya HIV na ukimwi. Wajumbe pia hupata fursa ya kuchunguza vipi maendeleo ya kisayansi yanavyoweza kwa njia rahisi kueneza habari kuhusu juhudi za kukabiliana na ugonjwa wa ukimwi.

Mkutano wa Afrika Kusini unafanyika wakati ambapo hali ya maisha ya waathirika wa ukimwi hapa Ujerumani imeendelea kuwa duni, licha ya kuwepo matibabu mazuri. Jan Löwenherz ni mtaalam wa sayansi ya kijamii na raia wa Ujerumani ambaye amekuwa akiishi na virusi vya HIV kwa miaka 15. Ana hofu sana hata kusikia jina lake likitajwa kwenye redio. Wakati bosi wake alipogundua kwamba ana virusi, alipoteza ajira yake kwenye maonyesho ya sanaa.

"Tayari nimepata uzoefu mbaya kikazi. Nilimdokezea mkubwa wangu kuhusu hali yangu. Baadaye ikasababisha mimi kupoteza kazi yangu, ikisemekana kuwa mimi mwenyewe nilitaka kuacha kazi. Sikuacha kazi bali niliachishwa kwa sababu ilithibitika ninaugua maradhi ya ukimwi na hiyo ingekuwa hatari kubwa katika siku za usoni."

Miaka tisa iliyopita, Jan Löwenherz alianza kutumia dawa za kupunguza makali ya ukimwi za ARV. Dawa hizi zinatakiwa kuzuia muathirika asipate ugonjwa wa ukimwi. Kila raia wa Ujerumani mwenye bima ya afya hulipiwa gharama za matibabu na kutokana na matibabu mazuri, Jan, mwenye umri wa miaka 35, anaweza kuendelea kuishi maisha ya kawaida. Kwa mujibu wa uchunguzi wa kiafya aliofanyiwa, Jan anaweza kuishi hadi kufikia umri wa miaka 70 au zaidi.

Jan ni miongoni mwa watu 63,000 wenye virusi vya ukimwi nchini Ujerumani. Zaidi ya watu 2,000 huambukizwa virusi kila mwaka. Kama ilivyo kwa Jan, maisha ni magumu kwa waathirika wengi. Volker Martens wa wakfu wa ukimwi wa Ujerumani anafahamu mateso yanayowakabili waathirika wengi wa ukimwi.

Blutprobe in Reagensglas
Simone Kaiser akionyesha damu yenye virusi katika kliniki ya chuo kikuu cha Eppendorf huko HamburgPicha: AP

"Mbali na huduma nzuri za matibabu, bado kungali na hofu ya unyanyapaa miongoni mwa wagonjwa wengi wa ukimwi. Majibu yanapobainisha wana virusi vya ukimwi, hawajui wamwamini nani kumwambia siri yao. Je wanaweza kuzungumzia wazi hali yao katika familia yao, pamoja na marafiki zao au pengine wanaweza pia kulizungumzia mahala wanapofanya kazi. Watu wengi wamepata uzoefu mbaya sana."

Kama ilivyo barani Afrika kwamba swala la ukimwi ni mwiko kuzungumziwa wazi hadharani, ndivyo ilivyo hapa Ujerumani. Kuna kampeni kubwa ya kuwahamasisha watu inayofanywa Ujerumani na uelewa wa ukimwi katika sehemu nyingi za humu nchini ni mkubwa kama ilivyo barani Afrika.

Na huku wataalam na mabingwa wa maswala ya afya wakikutana mjini Capetown Afrika Kusini, inasubiriwa kuona ni mchango gani utakaotolewa na kongamano hilo katika kuboresha huduma za matibabu na kuangamiza unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na virusi vya HIV na wagonjwa wa ukimwi.

Mwandishi: Nancy Wayua/ Josephat Charo

Mhariri: Othmanf Miraji