1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongomano la Kijamii la Kimataifa

8 Februari 2011

Bara la Afrika ni mada iliyoshughulikiwa tangu siku ya mwanzo ya Kongomano la Kijamii la Kimataifa linalofanyika katika mji mkuu wa Senegal, Dakar hadi Februari 11.

https://p.dw.com/p/Qz1S
Auftaktsmarsch des Weltsozialforums 2011 in Dakar, Senegal, Februar 2011. Foto wurde am 7. Februar 2011 gemacht. Copyright: Renate Krieger/DW
Maandamano yaliyofungua Kongomano la Kijamii la KimataifaPicha: Renate Krieger/DW

Licha ya kukumbana na matatizo ya upangaji, hiyo jana mamia ya wajumbe waliweza kushiriki katika midahalo ya "Siku ya Bara la Afrika" iliyofanywa katika Chuo Kikuu cha Cheikh Anta Diop mjini Dakar. Mkutano wa "Siku ya Afrika" haukufanyika katika ukumbi rasmi, kwani kulikuweko mvurugano katika ugawaji wa vyumba na kumbi za mikutano. Kwa hivyo, wajumbe walipaswa kukutana nje ya vyumba vya Chuo Kikuu, huku wakipishana na wanafunzi waliokuwa wakitoka masomoni.

Siku hiyo ilipangwa kujadili kwa kina, mada mbali mbali kuhusiana na bara la Afrika. Kwa mfano, kuadhimishwa miaka hamsini ya uhuru katika nchi mbali mbali barani Afrika au matatizo ya uhamiaji na maendeleo. Mvurugano wa upangaji wala haukuwazuia wajumbe wa kongomano hilo kushughulikia kile kilichowapeleka Dakar. Rais wa shirika la RADDHO, linalogombea haki za binadamu nchini Senegal, Alioune Tine amesema, yeye na wanaharakati wenzake wameanzisha mpango maalum kuambatana na mfumo wa maendeleo wa Kiafrika.

Alioune Tine, Präsident der senegalesischen Menschenrechtsorganisation RADDHO, schlug auf dem WSF einen "Afrika-Konsens" vor. Foto wurde am 7. Februar 2011 gemacht. Copyright: Renate Krieger/DW
Alioune Tine, Rais wa RADDHO, shirika linalogombea haki za binadamu SenegalPicha: Renate Krieger/DW

"Bara hili si masikini. Lina utajiri mkubwa sana wa raslimali na ardhi kubwa. Isitioshe kuna kuna makabila mbali mbali. Kwa hivyo baadhi ya mawazo ya kale yanapaswa kufikiriwa upya."

Mwanaharakati huyo amesema, mzozo wa kiuchumi uliotokea mwaka 2008 duniani, umedhihirisha mipaka ya sera za kibepari na ulanguzi. Kwani nchi zingine zimefanikiwa kuimarika kwa kufuata mifumo yake yenyewe. Alioune Tine na wapinzani wenzake wa utandawazi, wanatazamia kuwakilisha mapendekezo yao mbele ya mabunge mbali mbali barani Afrika. Amesema:

"Udhaifu wa taasisi, fedha na miundo mbinu ni hali inayotambulishwa na mashirika ya Kiafrika. Lakini umma una nia imara. Kama ilivyodhihirika huko Tunisia umma umeweza kuwaangusha vigogo. Hayo yanatokea Misri vile vile"

Kwa maoni yake wimbi hilo la mageuzi litafika katika nchi za Afrika ya Magharibi vile vile. Anasema, umma unapaswa kuchukua hatua, juu ya hatima yao kwa maslahi yao wenyewe.

Mwandishi:Krieger,Renate/ZPR/P.Martin.
Mpitiaji:M.Abdul-Rahman.