1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini: Mazungumzo na Rais Trump 'hayawezekani'

John Juma
10 Agosti 2017

Mkuu wa mikakati katika jeshi la Korea Kaskazini amesema "mazungumzo muafaka hayawezekani na mtu ambaye hana fikira na ambaye anachanganyikiwa. Matumizi ya nguvu dhidi yake ndiyo yanaweza kufanya kazi."

https://p.dw.com/p/2i1kX
Nordkorea - Konflikt - USA
Picha: Getty Images/AFP/K. Won-Jin

Umoja wa Ulaya umepanua orodha ya watu na mashirika ambayo yamejumuishwa kwenye vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini. Haya yanajiri wakati vita vikali vya maneno kati ya Washington na Pyongyang vikizidi kuzusha taharuki, huku Korea Kaskazini ikisema hakuna haja ya kuzungumza na Rais Trump.

Siku moja tu baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutishia Pyongyang kuwa itakumbwa na moto na ghadhabu kubwa ambayo dunia haijawahi kushuhudia, kufuatia mipango yake ya makombora, Korea Kaskazini imejibu kwa kusema hakuna haja ya mazungumzo na Rais Donald Trump.

Korea Kaskazini: 'Mazungumzo hayawezekani'

Mwanajeshi wa Korea Kaskazini akipita karibu na runinga inayoonesha umbali kati ya Korea kaskazini na kisiwa cha Guam
Mwanajeshi wa Korea Kaskazini akipita karibu na runinga inayoonesha umbali kati ya Korea kaskazini na kisiwa cha GuamPicha: Getty Images/AFP/J. Yeon-Je

Korea Kaskazini imeelezea mipango yake kabambe ya kushambulia kisiwa cha Marekani cha Guam kilichoko bahari Pasifiki katika siku chache zijazo. Kauli hiyo ya mkuu wa mikakati jeshini, Kamanda Kim Rak Gyom, ilitangazwa na runinga inayomilikiwa na serikali ya nchi hiyo na ilisema: "Mazungumzo muafaka hayawezekani na mtu kama huyo asiyefikiria na kutumia nguvu dhidi yake ndiyo itamfaa. Huo ndio uamuzi wa maafisa wa mkakati wa jeshi ya KPA"

Kisiwa hicho kina kambi ya jeshi la Marekani yenye ndege za kivita na wanajeshi 7000. Athari ya taharuki ambayo imesababishwa na vita vya maneno na vitisho vya kushambuliana kati ya Marekani na Korea Kaskazini zimesababisha kuporomoka kwa baadhi ya masoko ya fedha yakiwemo ya Ulaya na Marekani.

Vikwazo zaidi kwa baadhi ya Wakorea kaskazini

Wakati hayo yakijiri, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zimesema kupitia taarifa rasmi kuwa zinaongeza watu 9 pamoja na mashirika 4 kwenye orodha ya waliowekewa vikwazo kutoka Korea Kaskazini likiwemo benki linalomilikiwa na Korea Kaskazini FTB. Uamuzi unaofikisha idadi jumla ya waliowekewa vikwazo nchini humo kufikia 103 na mashirika 57.

Bendera ya Korea Kaskazini ikipepea mbele ya makombora yaliyooneshwa katika gwaride la kijeshi wakati wa maadhimisho ya miaka 100 ya muasisi wa nchi hiyo Kim II-Sung
Bendera ya Korea Kaskazini ikipepea mbele ya makombora yaliyooneshwa katika gwaride la kijeshi wakati wa maadhimisho ya miaka 100 ya muasisi wa nchi hiyo Kim II-SungPicha: Getty Images/AFP/E. Jones

Kuongezwa kwa orodha hiyo kunajiri wiki moja baada ya UMoja wa Mataifa kuongeza vikwazo vikali vya kiuchumi dhidi ya Korea Kaskazini. Vikwazo vilivyofuatia hatua ya Korea Kaskazini kufanya jaribio la kombora la masafa marefu linaloweza kufika Marekani.

Umoja Wa Ulaya wenye nchi wanachama 28 za bara la Ulaya zimeweka vikwazo vya usafiri na vikwazo dhidi ya mali ya Korea Kaskazini, kufuatia hatua yake ya ukiukwaji wa mara kwa mara wa maafikiano ya Umoja wa Mataifa kuhusu mipango yake ya makombora.

Baraza la Umoja wa Ulaya limesema litafanya juhudi kutekeleza maafikiano ya Umoja wa Mataifa ikiwemo juhudi za kudhibiti mapato ambayo raia wa Korea Kaskazini wanaofanya kazi ughaibuni hutuma katika nchi yao.

Mwandishi: John Juma/AFPE/DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga