1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini na Marekani zaendeleza vita vya maneno

Isaac Gamba
22 Septemba 2017

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amemuita Rais Donald Trump kuwa ni "ni mtu asiyeweza kufikiri sawasawa" na kusema atalipa gharama kutokana na kauli zake za vitisho anazotoa dhidi ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/2kVtH
Südkorea TV Bildschirm mit Donald Trump und Kim Jong Un
Picha: picture-alliance/AP Photo/Ahn Young-joon

 Kwa mujibu wa shirika la habari la Korea Kaskazini Kim Jong Un amesema hii leo kuwa Trump ni mtu asiyestahili kuwa na hadhi ya kuwa na mamlaka aliyo nayo ya amiri jeshi mkuu wa nchi na kumuelezea Rais huyo wa Marekani kuwa ni mtu "mjanja na jambazi  anayechezea moto".

Matamshi hayo ya kiongozi wa Korea Kaskazini yanafuatia hotuba ya Rais Donald Trump aliyoitoa katika mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa Jumanne wiki hii. Kim Jong Un amesema matamshi ya Trump yamemshawishi kuamini kuwa njia ambayo kiongozi huyo wa Korea Kaskazini aliyochagua kuifuata ni sahihi na kuwa ndiyo anapaswa kuifuata hadi mwisho na kuongeza kuwa alikuwa akifikiria kuchukua hatua kali.  Waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini ameripotiwa akitishia nchi hiyo kufanya jaribio la bomu la Hydrogen katika bahari ya pasifiki.

Trump atangaza vikwazo vipya dhidi ya Korea Kaskazini

Haya yanakuja mnamo wakati Rais Donald Trump akitangaza vikwazo vipya dhidi ya Korea Kasakazini vinavyolega kuidhibiti uwezo wa nchi hiyo katika kuendeleza mipango yake ya kuwa na uwezo wa kutengeneza silaha za nyukilia pamoja na makombora.  Rais Trump alitangaza vikwazo hivyo hapo jana wakati alipokuana na viongozi wa nchi washirika Japan na Korea Kusini ikiwa ni siku mbili baada ya kulihutubia baraza kuu la Umoja wa Mataifa na kutishia kuwa ataisambaratisha Korea Kaskazini iwapo itaendelea na vitendo vyake vya uchokozi.

Trump alisaini hapo jana amri nyingine ya utekelezaji inayolenga kuyapiga marufuku makampuni yaliyoko Marekani  yanayoshirikiana kibiashara na Korea Kaskazini.

Waziri anayehusika na masuala ya fedha wa Marekani Steven Mnuchin amesikika akisema kuwa taasisi za fedha tayari zimetaadharishwa kuwa zinapaswa kuchagua moja ama zinafanya biashara na Marekani au Korea Kaskazini.

Miami Steve Mnuchin US-Finanzminister
Waziri wa fedha wa Marekani Steven MnuchnPicha: picture-alliance/AP Photo/L. Sladky

Tayari Korea Kaskazini imeyapiga marufuku makampuni ya kigeni yanayoshirikiana na Korea Kaskazini katika mipango yake ya kijeshi lakini hatua ya sasa inatanua wigo wa vikwazo vilivyochukuliwa dhidi ya Korea Kaskazini ambavyo sasa vinagusa kuanzia teknolojia ya habari na mawasiliano, sekta ya uzalishaji ikiwa ni pamoja na viwanda vya nguo pamoja na uvuvi.

Hata hivyo nyakati zitaeleza iwapo vikwazo hivyo vya kuchumi vitamlazimisha kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un kurudi nyuma ingawa kiongozi huyo kijana anaonekana kuionyesha dunia kuwa hatishwi na matamshi makali ya Trump.

Sigmar Gabriel asisitiza juu ya ushirikiano kimataifa

USA Bundesaussenminister Sigmar Gabriel spricht vor der UN-Vollversammlung
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel Picha: Reuters/E. Munoz

Wakati huohuo waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel katika hotuba yake kwenye baraza kuu la Umoja wa Mataifa ameonya juu ya kauli za  kutanguliza masilahi ya taifa akionesha dhahiri kutokukubaliana na kauli kama hiyo ambayo imetolewa mara kwa mara na Rais wa Marekani Donald Trump.

Akizungumza pasipo kumtaja Trump, Gabriel alisema kauli za kutanguliza utaifa kwanza ni kauli ambazo zitasababisha migongano kitaifa na mwishowe hakuna faida itakayopatikana.  Amesisitiza kuwa dunia inahitaji ushirikiano zaidi kimataifa na utaifa kidogo na siyo kinyume chake.

Aidha waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani alitoa mwito wa kuimarishwa kwa Umoja wa Mataifa akitolea mfano wa mafanikio ambayo Ujerumani imepata kupitia ushirikiano kimataifa na pia ushirikiano barani ulaya na kuongeza kuwa halikuwa suala la "Ujerumani kwanza" lililoifanya Ujerumani kuwa taifa lenye nguvu kiuchumi bali  ni Ulaya pamoja na kuwajibika kimataifa.

Mwandishi: Isaac Gamba/dw/afpe/dpae

Mhariri   :Mohammed Abdul-Rahman