1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea kaskazini yabanwa na vikwazo vikali zaidi

Sekione Kitojo
6 Agosti 2017

Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa jana Jumamosi(05.08.2017) kwa kauli moja limeunga mkono azimio la Marekani  linaloimarisha vikwazo dhidi ya Korea kaskazini, likipiga marufuku mauzo ya nje yanayoipatia nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/2hl8Y
UN-Sicherheitsrat verhängt schärfere Nordkorea-Sanktionen
Wajumbe wa baraza la Usalama wakipiga kura kuidhinisha azimio la kuiwekea vikwazo Korea kaskaziniPicha: Picture-alliance/dpa/M. Altaffer/AP

Hatua  hizo ni  za  kwanza  za  aina  hiyo  zilizowekwa  dhidi  ya  Korea  kaskazini  tangu rais Donald Trump  kuingia  madarakani  na  kuonesha  kuwapo  tayari  kwa  China  kuiadhibu nchi  hiyo  ambayo  ni  mshirika  wake.

Azimio  hilo linaweka  marufuku  kamili katika  mauzo  ya  makaa  ya  mawe, chuma na mchanga  wa  chuma, risasi  pamoja  na  samaki  na  vyakula vinavyotokana  na  bahari katika  taifa  hilo  lenye matatizo  makubwa  ya  fedha  za  kigeni, na  kuinyima korea kaskazini theluthi  ya  mapato  yake  ya  nje  yanayokadiriwa  kufikia  dola  bilioni 3 kwa mwaka.

Nordkorea Kim Jong Un Freude nach dem Test der Hwasong-14 Rakete
Kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un (kulia)Picha: Reuters/KCNA

Balozi  wa  Marekani  Nikki Haley  amesema  hatua  hizo  ngumu zimeleta athabu  hiyo iliyowekwa  dhidi  ya  Korea  kaskazini  kutokana  na  majaribio  yake  ya  makombora, "katika  kiwango  kipya  kabisa "  na  kwamba  baraza  limemuweka  kiongozi  wa  nchi  hiyo Kim Jong-Un katika  uangalizi.

"Hizi ni  hatua  kali  kabisa  za vikwazo  dhidi  ya  nchi  yoyote ile  katika  kizazi  kimoja," haley ameliambia  baraza  la  Usalama  baada  ya  kura  hiyo.

"Vikwazo  hivi vitaingia  kwa  kina  na  kwa  kufanya  hivyo, vitatoa  kwa  uongozi  wa  Korea kaskazini ladha ya  kujidhalilisha  waliochagua   kuwaletea  wananchi  wa  Korea  kaskazini."

Azimio  hilo  pia  linaizuia Korea  kaskazini kuongeza  idadi  ya  wafanyakazi  inaotuma  nje ya  nchi  ambao  kipato  chao  ni  chanzo  kingine  cha  mapato ya  utawala  huo  wa  Kim.

Uwekezaji utaathirika

Pia  linazuia njia  zote  mpya  za  pamoja  na  Korea  kaskazini , na  kupiga  marufuku uwekezaji  mpya   katika  makampuni  ya  pamoja  na  kuongeza  maafisa  tisa  wa  Korea kaskazini  pamoja  na  mashirika  manne  ikiwa  ni  pamoja  na  benki  kuu  ya  fedha  za kigeni  ya  Korea  kaskazini   katika  orodha  ya  vikwazo  vya  Umoja  wa  Mataifa.

iwapo  hatua  hizo  zitatekelezwa  kikamilifu , zitakaza  kitanzi  cha  uchumi  wa  Korea kaskazini wakati  nchi  hiyo  ikijaribu  kuendeleza  mipango  yake  ya  makombora  na nyuklia.

Trump  amesifu  kura  hiyo  kwa  kauli  moja   katika  baraza  la  usalama  la  Umoja  wa mataifa, akisema  vikwazo  hivyo  vitakuwa  na "athari  kubwa  ya  kiuchumi!"

Ni "vikwazo  vikubwa vya  uchumi  dhidi  ya  Korea kaskazini. Zaidi  ya  bilioni  moja ya  dola katika  gharama  kwa  Korea ," kiongozi  huyo  wa  Marekani ameandika  katika  ukurasa  wa twita.

Nordkorea Raketentest
Kombora la Korea kaskazini Picha: picture-alliance/AP Photo/Korean Central News Agency

Marekani  imeingia  katika  majadiliano  na  China mwezi  mmoja  uliopita kuhusiana  na azimio  hilo  jipya  baada  ya  Pyongyang kufanya  majaribio  yake  ya  kwanza  ya makombora  yanayoweza  kuvuka mabara  Julai 4  ambayo  yalifuatiwa  na jaribio  la  pili Julai 28.

Lakini hatua  hiyo  haitoi  nafasi  ya  kupunguzwa  upelekaji  wa  mafuta  kwa  Korea kaskazini  kama  ilivyopendekezwa  hapo  kabla  na  Marekani , hatua   ambayo  ingetoa pigo  kubwa  kwa  uchumi  wa  nchi  hiyo.

Hatua  hizo  mpya  za  ni  kundi  la  saba   la vikwazo  vya  Umoja  wa  Mataifa vilivyowekewa Korea  kaskazini  tangu  ilipoanza  kufanya  majaribio  ya  kinyuklia  mwaka  2006.

Mwandishi : Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Sudi  Mnette