1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yafanya jaribio la bomu la Haidrojeni

Caro Robi6 Januari 2016

Korea Kaskazini imesema imefanikiwa kufanya jaribio la bomu la haidrojini. Jaribio hilo limezua hofu nchini Japan na Korea Kusini huku jumuiya ya kimataifa ikilaani hatua hiyo ya Korea Kaskazini.

https://p.dw.com/p/1HZ5z
Picha: picture alliance/AP Images/Wong Maye-E

Jaribio hilo, lililofanywa leo na Korea Kaskazini, taifa ambalo limetengwa na Jumuiya ya kimataifa, limeagizwa kufanywa na kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong Un.

Kituo cha televisheni cha serikali ya Korea Kaskazini kimeonyesha waraka ulioandikwa na Kim ukisema wacha ulimwengu uitizame nchi imara na inayojitegemea kwa kujihami na silaha za kinyuklia.

China ambayo ni mshirika wa Korea Kaskazini imelaani jaribio hilo la bomu la kutumia gesi ya haidrogeni na kusema itawasilisha malalamiko yake kwa nchi hiyo.

Bomu la Haidrogini lina nguvu zaidi

Licha ya kuwa jaribio la nne la kinyuklia lilikuwa linatarajiwa kufanywa na nchi hiyo, madai ya kuwa ni bomu hilo ambalo lina nguvu zaidi ya bomu la atomiki, halikutarajiwa kufanyiwa majaribio.

Kituo cha Televisheni cha Korea Kaskazini kikiripoti jaribio la bomu
Kituo cha Televisheni cha Korea Kaskazini kikiripoti jaribio la bomuPicha: picture-alliance/AP Photo/L. Jin-man

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litafanya mkutano wa dharura leo mjini New York kujadili hatua hiyo ya Korea Kaskazini. Mkutano huo wa faragha umeitishwa na Umoja wa Mataifa na Japan.

Msemaji wa Marekani, Hagar Chemali, amesema hawajaweza kuthibitisha iwapo ni kweli jaribio hilo la bomu limefanywa na wanalaani ukiukaji wowote wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuitaka Korea Kaskazini kuheshimu wajibu wake wa Kimataifa.

Iwapo itathibitishwa, kuwa bomu lililofanyiwa majaribio ni la kutumia nguvu za maji, basi litakuwa lenye nguvu zaidi kuwahi kujaribiwa na nchi hiyo na hivyo kudhihirisha kuongezeka kwa uwezo wake wa kinyuklia na kuiepelekea nchi hiyo kuwekewa vikwazo zaidi na Jumuiya ya Kimataifa.

Bomu la haidrogeni lina uwezo mkubwa ikilinganishwa na mabomu mengine yenye madini ya Plutonia ambayo Korea kaskazini imefanya majaribio katika miaka ya awali. Nchi hiyo ilifanya majaribio ya kinyuklia mwaka 2006, 2009 na 2013 na kupelekea kuwekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa.

Jumuiya ya Kimataifa yalaani jaribio la Korea Kaskazini

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Philiph Hammond amelitaja jaribio hilo la kinyukulia kuwa uchokozi na ukiukaji mkubwa wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Philiph Hammond akiwa China
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Philiph Hammond akiwa ChinaPicha: Reuters/China Daily

Hammond ambaye yuko ziarani China, amesema amezungumza na mwenzake wa China Yang Jiechi na wamekubaliana kushirikiana na nchi wanachama wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kufikia jibu muafaka la kujibu kitendo hicho cha Korea Kaskazini.

Raia wa China wanaoishi katika maeneo ya mipakani na Korea Kaskazini wameondolewa kutoka majengo baada ya kushuhudiwa mitetemeko ya ardhi baada ya jaribio hilo.

Kituo cha Televisheni cha China kimeripoti watu wanaoishi katika mipaka ya Ynaji, Hunchun na Changbai katika jimbo la Jilin karibu walihisi mitetemeko ya ardhi leo asubuhi karibu na eneo kuliko na kinu cha nyukilia cha Korea Kaskazini.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Afp

Mhariri: Mohammed Khelef