1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yafyatua kombora jengine

Sekione Kitojo
15 Septemba 2017

Korea Kaskazini imefyatua kombora jingine la masafa ya kati juu ya anga ya Japan na kuangukia katika Bahari ya Pasifiki, likisafiri kwa muda mrefu zaidi kuliko yote yaliyotangulia na likitajwa kuwa ishara ya ukaidi.

https://p.dw.com/p/2k1UM
Südkorea Raketentest
Picha: picture-alliance/NurPhoto/South Korea Defense Ministry

Waziri mkuu  wa  Japan Shinzo Abe  amesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kutoa  ujumbe wa  wazi kwa Korea kaskazini  kutokana  na  kitendo  hicho  cha  uchokozi.

Tangu  pale  rais  wa  Marekani Donald Trump  alipoitishia  Korea kaskazini  kwa  kile  alichosema "kutakuwa  na  moto  na  hasira" mwezi  Agosti, Pyongyang  imekwisha  fanya jaribio lake  kubwa  la kinyuklia, ikitishia  kurusha  makombora  katika  eneo  la  maji kuzunguka  kisiwa  cha  Guam na  kufanya  majaribio  ya makombora  mawili  ambayo  yanaruka kwa  masafa  ya  mbali  zaidi kupitia  anga  ya  mshirika  wa  Marekani , Japan.

Nordkorea Kim Jong-Un
Kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong UnPicha: Getty Images/AFP/STR

Ongezeko  la wimbi  la  kurusha  makombora, nguvu  na  kujiamini kunakooneshwa  na  majaribio  haya  kunaonekana  kuthibitisha  kile serikali  mbali  mbali  na  wataalamu  wa  nje  walichosema  kwa muda  mrefu  kuwa  Korea  kaskazini  ipo  karibu  na  lengo  lake  la kujenga  hazina  ya  silaha  za  kijeshi  ambazo  zinaweza  kulenga majeshi  ya  Marekani  katika  eneo  la  Asia  na  pia  kufika  katika ardhi  ya  Marekani  kwenyewe. Kwa  upande  mwingine , hii  ina maana ya  kuzusha  shaka  nchini  Korea  kusini  na  Japan  kwamba Marekani   itahatarisha  kusagwasagwa  kwa  mji  wa  nchi  yake  ili kuwalinda  washirika  wake  katika  bara  la  Asia.

Jopo  la  wakuu  wa  vikosi  vya  majeshi  ya  Korea  kusini limesema  kombora  hilo  liliruka  kwa  kiasi  cha  umbali  wa kilometa  3,700  na  kufikia  kima  cha  juu  kabisa  cha  kilometa 770 kwenda  juu.

Korea  kaskazini  imekuwa  ikiapa  kuendelea  na  majaribio  yake kutokana  na  kile  inachokiita  uhasama  wa  Marekani  dhidi  yake, ikiwa na maana ya kuwapo  kwa  mamia  kwa  maelfu  ya  wanajeshi wa  Marekani  nchini  Japan na Korea  kusini.

Südkorea Raketentest
Kombora la Korea kaskazini likivurumushwaPicha: picture-alliance/NurPhoto/South Korea Defense Ministry

Mazungumzo yamekwama

Mazungumzo  ya kidiplomasia  kuhusiana  na  suala  hilo  yamekwama kwa  miaka kadhaa, na  kuna  ishara  ndogo  kwamba  maafisa  wa  ngazi  ya juu  kutoka  Pyongyang  na  Washington  huenda  wakakaa  pamoja kujadili  njia  za  kupunguza  kasi  ya  Korea  kaskazini  yenye dhamira  ya  kujumuishwa  miongoni  mwa  nchi zenye  nguvu  za silaha za kinyuklia.Waziri mkuu wa  Japan Shinzo  Abe amesema.

"Korea kaskazini  imekaidi  nia  ya jumuiya  ya  kimataifa  kufikia suluhisho  la  amani , na  kwamba  Japan haitavumilia kitendo kama  hicho."

Kombora  la  leo  ambalo, Korea  kusini  inasema  ni  la  19 kurushwa na  Korea  kaskazini  mwaka  huu , lilisababisha  tahadhari ya ving'ora  na  tahadhari  kutolewa  kaskazini  mwa  Japan lakini hakuna  uharibifu  uliotokea kwa  ndege  ama  meli.

Indien Ahmadabad Besuch Shinzo Abe aus japan
Waziri mkuu wa Japan Shinzo AbePicha: picture-alliance/AP Photo/S. Solanki

Jaribio  hilo  limezusha  tena  matamshi makali. Rais  wa  Korea kusini  Moon Jae-In ameamuru  jeshi  lake kufanya  luteka  ya kufyatua  makombora  ya mwendo wa  kasi  kujibu  hatua ya Korea kaskazini  na  kuwapa  maelekezo  maafisa  wa  serikali  kutafakari kuchukua  hatua  kali  ili  kuikatisha  tamaa  Korea  kaskazini kuendelea  na  uchukozi.

Waziri  mkuu  wa  Japan  Shinzo Abe  na  waziri  wa  mambo  ya kigeni  wa  Marekani Jim Mattis wamelieleza  jaribio  hilo  la  Korea kaskazini  kuwa  ni  kitendo kilichofanywa bila  kuchukua tahadhari. Baraza  la  Usalama  la  Umoja  wa  Mataifa  limepanga  kikao cha dharura  na  cha  faragha kitakachofanyika  leo  mchana mjini  New York  kujadili  suala  hilo. Jumuiya ya  NATO imetaka pachukuliwe hatua  na  jumuiya  ya  kimataifa  kuhusu jaribio hilo  la  kombora la Korea ya kaskazini.

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape

Mhariri:  Iddi Ssessanga