1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yaonya kushambulia kisiwa cha Marekani Guam

John Juma
9 Agosti 2017

Pyongyang yasema itafanya mashambulizi dhidi ya kisiwa cha Guam chenye kambi ya jeshi la Marekani punde tu Rais Kim Jong Un akiidhinisha. Ni kufuatia matamshi ya Rais Trump dhidi ya Pyongyang.

https://p.dw.com/p/2hwpp
Nordkorea Kim Jong-un
Picha: Reuters/KCNA

Korea Kaskazini imeonya kuwa itakishambulia kisiwa cha Marekani cha Guam. Kauli hii ya Pyongyang inajiri saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutishia kuwa Korea Kaskazini itakabiliwa vikali. Ujerumani na mataifa mengine wamezitaka pande hizo kutumia busara zaidi ili kuepusha balaa.

Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la Korea Kaskazini, watafanya shambulizi wakati wowote dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani iliyoko katika kisiwa cha Guam kwenye bahari ya Pasifiki, punde tu rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un atakapoidhinisha.

Eddie Calvo: Hakuna kitisho Guam

Kulingana na ripoti kwenye shirika la habari la serikali ya Korea Kaskazini, msemaji huyo wa jeshi ameongeza kuwa Marekani inapaswa kukoma kutoa matamshi ya kuchochea vita dhidi ya Korea Kaskazini ili Pyongyang isilazimike kuchukua suluhisho la kijeshi.

Rais Donald Trump
Rais Donald TrumpPicha: Picture-Alliance/AP Photo/E. Vucci

Hata hivyo Gavana wa Guam Eddie Calvo amesema kuwa hakuna kitisho chochote kwa Guam kwa sasa, huku akiwahakikishia wakaazi kuwa wako tayari. "Shambulizi au kitisho dhidi ya Guam, ni kitisho au shambulio dhidi ya Marekani. Ikulu ya White House imesema Marekani italindwa. Na Guam ni sehemu ya Marekani. Tuna Wamarekani 200,000 wanaoishi Guam na Maryana, hivyo sisi si tu kambi ya jeshi".

Cheche za maneno kati ya Marekani na Korea Kaskazini

Onyo la kushambulia kisiwa cha Guam chenye kambi ya Andersen ya wanajeshi wa angani wa Marekani, linajiri saa chache baada ya Rais Donald Trump kusema kuwa ikiwa Pyongyang itaendelea na vitisho vyake, basi itakabiliwa kwa ghadhabu na nguvu kubwa ambayo dunia haijawahi kushuhudia. Kwenye ukurasa wake wa Twitter, Rais Trump ameongeza kuwa kwa sasa silaha za nyuklia za Marekani zimeimarishwa maradufu kuliko zamani.

Hata hivyo seneta wa Republican John McCain ameelezea wasiwasi wake kuhusu kitisho cha Trump akisema hana uhakika ikiwa Trump alikuwa tayari kushambulia Pyongyang. McCain amesema na namnukuu, "sharti uwe na uhakika wa kufanya kile unachosema," mwisho wa kunukuu.

Makombora ya Korea Kaskazini yakirushwa
Makombora ya Korea Kaskazini yakirushwaPicha: Getty Images/AFP/Str.

Marekani imeitaka Korea Kaskazini kusitisha mipango yake ya utengenezaji wa zana zake za kinyuklia ndipo vikwazo dhidi yake viondolewe. Mnamo Jumamosi iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliwekea Korea Kaskazini vikwazo zaidi.

Ujerumani: Marekani na Korea Kaskazini zijizuie

Baadhi ya mataifa yakiwemo Ujerumani, China na Ufaransa yamezitaka Marekani na Korea Kaskazini kujizuia dhidi ya hali inayoweza kusababisha vita vya maangamizi makubwa kutokana na zana za nyuklia.

Kitisho cha makabiliano hayo kwa kutumia silaha za nyuklia kimejiri wakati Japan ikifanya kumbukumbu ya wahanga wa shambulio la bomu la atomiki lililodondoshwa miaka 72 iliyopita, katika mji wake wa Nagasaki, siku tatu baada ya Marekani kudondosha bomu kama hilo mjini Hiroshima. Watu 74,000 waliuawa kufuatia shambulio la bomu la atomiki dhidi ya Nagasaki.

Mwandishi: John Juma/DPAE/RTREAPE

Mhariri: Iddi Ssessanga