1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yazidi kutishia amani.

Halima Nyanza27 Mei 2009

Korea kaskazini ambayo inakabiliwa na vikwazo vya kimataifa, baada ya kufanya jaribio lake la nyuklia, leo imetishia kuishambulia Korea kusini, baada ya nchi hiyo kuungana na juhudi za Marekani kukamata meli zake.

https://p.dw.com/p/HyAb
Kora kaskazini inazidi kutishia amani, kutokana na ukaidi wake wa kuendelea kufyatua makombora.Picha: AP

Vitisho hivyo vya Korea Kaskazini dhidi ya Korea kusini vimekuja baada ya Vyombo vya Habari vya Korea kasini kuripoti habari kuhusiana na Mtambo wa Korea kaskazini wa madini ya sumu kali yanayotumika katika kutengeneza silaha za nyuklia, kuanza tena kufanya kazi.


Msemaji wa Jeshi la Korea kaskazini amenukuliwa akisisitiza kuwa nchi yake haiko tena katika mapatano ya kusimamisha vita kwa muda yaliyosainiwa mwishoni mwa vita vya Korea vya mwaka 1950 hadi 53, kwa sababu Marekani inadharau wajibu wake kama mtiaji saini kwa kuitayarisha Korea Kusini katika juhudi za kuzuia ueneaji wa silaha za maangamizi.


Amesema hatua yoyote ya uhasama dhidi ya meli zao ikiwemo, kuzipekua na kuzikamata itazingatiwa kuwa ni ukiukwaji wa uhuru wao isiosameheeka na kwamba watachukua hatua za mashambulio ya nguvu ya kijeshi.


Jana Korea Kusini ilitangaza kujiunga na mazoezi ya jeshi la majini, jambo ambalo Korea kaskazini iliizingatia hatua hiyo kwamba ni kutangaza vita.


Jana jioni Korea kaskazini ilifanyia jaribio kombora lingine la masafa mafupi ambalo lilikuwa ni la tatu kwa jana kulifyatua, jambo ambalo linazidi kuongeza hali ya wasiwasi katika eneo hilo.


Korea Kaskazini na Kusini ziliwahi kuingia katika mapigano ya jeshi la majini mwaka 1999 na 2002 karibu na eneo la mpaka wa bahari lililo na mgogoro na kwamba mwaka uliopita Pyongyang ilitishia kushambulia meli za Korea Kusini.


Awali Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon aliitaka Korea kaskazini kuachana na hatua zozote zitakazoongeza hali ya wasiwasi katika eneo hilo.

Naye Balozi msaidizi wa Korea kaskazini katika Umoja wa Mataifa Pak Tok Hun amesisitiza kuwa mpango wake huo wa nyuklia ni kwa ajili ya kujilinda na kutaka baadhi ya nchi kuacha sera zake za chuki.

Aidha jaribio la nyuklia lililofanywa na Korea kaskazini limeongeza hali ya wasiwasi kuhusiana na nchi hiyo kusambaza silaha kwa makundi ama nchi nyingine.


Marekani imeilaumu Korea kaskazini kwa kujaribu kuuza utaalamu wa kinyuklia kwa Syria na nchi nyingine.


Kwa sasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa likijadili njia za kuiadhibu Pyongyang, kutokana na kufanya jaribio lake la Nyuklia siku ya Jumatatu.


Mwandishi: Halima Nyanza(AFP9

Mhariri: Abdul-Rahman