1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kusini kuanza matangazo ya propaganda

7 Januari 2016

Korea Kusini imetangaza kwamba itaanza tena kurusha matangazo ya propaganda kwenye eneo la mpakani katika nchi jirani ya Korea Kaskazini, ikiwa ni kujibu kitendo cha nchi hiyo kufanya jaribio la bomu la nyuklia.

https://p.dw.com/p/1HZu7
Vipaza sauti vya Korea Kusini
Vipaza sauti vya Korea KusiniPicha: picture-alliance/dpa/J.H. Park

Shirika la habari la Korea Kusini, Yonhap limeripoti kuwa tahadhari ya ngazi ya juu ya kijeshi imetolewa kuhusu maeneo ya mpakani ambako vipaza sauti vitawekwa hapo kesho (08.01.2015), kwa lengo la kuanza tena matangazo ya propaganda kwa sababu Korea Kaskazini imekiuka makubaliano yaliyofikiwa mwezi Agosti mwaka uliopita ya kupunguza mvutano.

Afisa mwandamizi wa rais wa Korea Kusini anayehusika na usalama wa kitaifa, Cho Tae-Yong, amesema matangazo hayo yataanza kesho ambayo ni siku ya kuzaliwa kwa kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un na yanaonekana kuwa yataiudhi sana nchi hiyo.

'' Serikali imeamua kuanza matangazo ya propaganda dhidi ya Korea Kaskazini kuanzia mchana wa Januari 8. Jeshi letu liko tayari kabisa na iwapo Korea Kaskazini itaendelea na uchokozi wake, basi itakabiliwa na adhabu kali mno,'' alisema Cho.

Cho amesema kitendo cha Korea Kaskazini kutangaza kufanya jaribio la bomu la nyuklia siku ya Jumatano, pia limekiuka sheria za kimataifa. Mvutano kati ya nchi hizo mbili ulizuka mwezi Agosti baada ya wanajeshi wawili wa Korea Kusini kuuawa kwa mabomu ya kutega ardhini na tangu Korea Kaskazini ilivyofyatua makombora manne kwenye eneo la mpaka.

Matangazo ya 2015 yalisababisha mzozo wa kijeshi

Matangazo hayo yalichochea mzozo wa kijeshi kati ya Korea hizo mbili mwaka uliopita. Nchi hizo mbili hatimaye zilikubaliana katika masuala kadhaa ikiwemo Korea Kusini kuacha kutangaza propaganda dhidi ya Korea Kaskazini, hadi hapo itakapotokea tena hali isiyokuwa ya kawaida.

Maafisa waandamizi wa Korea Kusini na Kaskazini wakipeana mikono, Agosti 22. 2015
Maafisa waandamizi wa Korea Kusini na Kaskazini wakipeana mikono, Agosti 22. 2015Picha: Getty Images/South Korean Unification Ministry

Korea Kusini imesema pia itaweka kizuizi cha kuingia katika kiwanda cha pamoja kinachoendeshwa na Korea zote mbili na ambao ni mradi mkuu uliobakia katika ushirikiano kati yao.

Korea Kusini haitoathirika na hatua hiyo kwa sababu itawahusu zaidi wateja, wanunuzi wakuu na watoa huduma kutoka Korea Kusini, kuliko mameneja ambao wanasafiri umbali mrefu kufanya kazi na vibarua wa Korea Kaskazini.

Siku ya Jumatano Korea Kaskazini ilitangaza kuwa imefanya jaribio lililofanikiwa la bomu la nyuklia. Hata hivyo, utafiti wa awali uliofanywa na serikali ya Marekani umeonyesha kuwa bomu hilo halikuwa na nguvu kubwa namna hiyo kama ambavyo Korea Kaskazini imedai.

Kutokana na kitendo hicho ambacho kimelaaniwa vikali kimataifa, Marekani na washirika wake wakuu wawili wa kijeshi barani Asia, ambao ni Korea Kusini na Japan, wametishia kuchukua hatua kali dhidi ya Korea Kaskazini.

Aidha, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana kwa dharura kulaani vikali jaribio hilo la Korea Kaskazini na limeahidi kuweka vikwazo vipya dhidi ya nchi hiyo, likisema kitendo hicho kimekiuka maazimio ya awali ya Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,APE
Mhariri: Mohammed Khelef