1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea mbili hatarini kupigana

Abdu Said Mtullya23 Novemba 2010

Wasiwasi umezuka kwamba huenda Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini zikaingia kwenye vita, baada ya kuanza chokochoko za mapigano ya mpakani hapo jana (22 Novemba 2010)

https://p.dw.com/p/QFtK
Kisiwa cha Yeonpyeong , chimbuko la mvutano baina ya korea mbili.Picha: AP

Askari mmoja wa Korea ya Kusini ameuawa baada ya majeshi ya korea ya Kaskazini kukishambulia kisiwa cha Korea ya kusini kilichopo karibu na mpaka wa nchi hizo mbili.

Askari wengine kadhaa wa Korea ya kusini walijeruhiwa katika shambulio hilo.Vyombo vya habari vimearifu kuwa askari wengine wasiopungua 13 wa Korea ya Kusini walijeruhiwa katika shambulio hilo lililotokea kwenye mpaka baina ya nchi mbili za Korea ambapo pana kisiwa cha Yeonpyeong. Kisiwa hicho kilifunikwa na moshi na wakaazi wake walikuwa wanakimbia kwa kutumia mashua ya kuvulia.Na kwa mujibu wa habari za televisheni raia pia walijeruhiwa.

Majeshi ya Korea ya Kusini yalijibu mashambulio kwa kuzilenga ngome za mizinga za Korea ya Kaskazini zilizopo kwenye pwani ya kaskazini ya nchi hiyo.

Mkuu wa majeshi ya Korea ya Kusini pamoja na wizara ya ulinzi ya nchi hiyo pia imearifu kwamba ndege za kijeshi zilipelekwa kwenye kisiwa cha Yeonpyeong .Nyumba kwenye kisiwa hicho kilichopo umbali wa kilometa 12 kutoka pwani ya Korea ya Kaskazini zilikuwa zinawaka moto.

Askari 1000 wa Korea ya Kusini wamewekwa katika kisiwa hicho ambacho wakati wote kimekuwa chimbuko la mvutano baina ya Korea mbili kutokana na umuhimu wa mahala kilipo na kutokana na utajiri wake wa samaki.

Habari zaidi zinasema pamekuwapo mapambano baina ya majeshi ya majini ya nchi mbili hizo.Habari pia zinasema ,Korea ya Kusini imeitisha kikao cha dharura na imeyaweka majeshi yake katika hali ya tahadhari.Rais wa nchi hiyo Lee Myung Bak aliitisha mkutano huo kwenye handaki la mawaziri.

Afisa mmoja wa wizara ya Korea ya Kusini inayoshughulikia masuala ya muungano, ameliambia shirika la habari la Yonhap kwamba Korea ya Kusini inafikiria juu ya kuwahamisha wakaazi wa kijiji cha Yeonpyeong.

Wakaazi wapatao 1300 wa kijiji hicho wamo katika hali ya wasiwasi.

Mvutano huo umekuja siku chache tu baada ya Korea ya Kaskazini kutangaza kwamba imejenga mtambo mpya wa kurutubishia madini ya Uranium.

Ofisi ya rais wa Korea ya Kusini imesema inachunguza ili kubaini iwapo Korea ya Kaskazini ilianzisha mashambulio kama ishara ya kuyapinga mazeozi ya kijeshi yanayofanywa na Korea ya Kusini kwenye pwani ya magharibi,ya nchi hiyo ambapo wanajeshi alfu 70 wanashiriki.

Mashirika ya habari yamesema kiwango cha hatari inayotokana na mkasa huo hakijawahi kufikiwa tokea kumalizika vita vya Korea mnamo mwaka wa 1953.

Marekani imeilaani vikali Korea ya Kaskazini kwa kuanzisha mashambulio .

Mwandishi/Mtullya Abdu/AFPE/BBC./

Mhariri/ Othman Miraj/