1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KUALA LUMPUR:Mjumbe wa UN yu ziarani Malaysia

17 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7F4

Mjumbe wa Umoja Umoja wa Mataifa Ibrahim Gambari anakutana na viongozi wa Malaysia hii leo zikiwa ni juhudi za kuhusisha mataifa ya Asia ya Kusini mashariki kuzipa msukumo harakati za kutafuta demokrasia nchini Myanmar.Mjumbe huyo ananuia kuona mchango wa mataifa ya eneo hilo katika kutafuta suluhu ya tatizo la kisiasa la Myanmar kufuatia maandamano ya kudai demokrasia yaliyoongozwa na watawa wa Kibudda.Utawala wa kijeshi wa Myanmar unakabiliwa na shinikizo kutoka jamii ya kimataifa tangu kushambulia waandamanaji wanaodai demokrasia katika maandamano ya mwezi jana.

Ziara ya Bwana Gambari ina lengo la kushinikiza uongozi wa kijeshi wa Myanmar kusitisha mashambulizi yake dhidi ya maandamano ya amani ya kudai demokrasia,kuachia wafungwa wa kisiasa aidha kuanzisha mazungumzo na vyama vya upinzani vinavyoongozwa na Aung San Suu Kyi.

Mataifa ya jirani ya jumuiya ya ASEAN yanatakiwa kuchukua msimamo mkali zaidi dhidi ya Myanmar ila hayawezi kusitisha uanachama wake.Malaysia ilidhamini Myanmar kujiunga na jumuiya hiyo mwaka 1997 ila kwa sasa inakosoa vikali uongozi wake wa kijeshi.

Myanmar kwa upande wake inasisitiza kuwa haitashinikizwa na mataifa ya kigeni huku Japan ikisitisha msaada wake na Umoja wa Ulaya kuongeza vikwazo ilivyoiwekea.