1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kufa kupona leo Italia na Uruguay

24 Juni 2014

Mabingwa wa zamani Italia na Uruguay wanakutana katika pambano litakalokuwa na patashika nguo kuchanika la kuamua nani anaingia katika duru ya awamu ya mtoano katika kombe la dunia jioni ya leo(24.06.2014).

https://p.dw.com/p/1CPUw
WM 2014 Gruppe D 2. Spieltag Italien Costa Rica
Mario Barlotelli wa ItaliaPicha: Getty Images

Kocha wa Uingereza Roy Hodgson anatarajia kuteremsha dimbani kikosi cha majaribio wakati ndoto za jinamizi za timu hiyo zinafikia mwisho baada ya vipigo mara mbili na inapimana nguvu na Costa Rica ambayo tayari imejihakikishia nafasi katika timu 16 bora za kombe la dunia.

Cote d'Ivoire nayo itajitupa uwanjani kupambana na Ugiriki, wakati huo huo Japan ina miadi na Colombia inayoongoza kundi hilo la C.

Fifa WM 2014 Uruguay England
Luis Suarez wa UruguayPicha: Getty Images

Mabingwa wa zamani Italia na Uruguay zinatiana kifuani jioni ya leo mjini Natal kuamua ni timu ipi itajiunga na timu kundi la timu 16 zitakazosalia katika kinyang'anyiro cha kombe la dunia nchini Brazil mwaka huu. Timu hizo mbili zilizo na points 3 kutokana na michezo miwili, zote zilipoteza michezo yao dhidi ya Costa Rica na kuifunga Uingereza. Italia inahitaji sare tu , hata hivyo ni kutokana tu na kuwa na tofauti nzuri ya magoli.

Fifa WM 2014 Uruguay England
Wayne Rooney wa UingerezaPicha: Reuters

Suarez yuko fit

Habari nzuri kwa Uruguay ni kwamba mshambuliaji wao hatari Luis Suarez , ambaye alikosa mchezo wao wa kwanza kutokana na kuumia lakini alikuwamo katika kikosi kilichoizamisha Uingereza kwa magoli mawili, yuko fit kuikabili Italia.

Uingereza ambayo tayari imeyaaga mashindano haya itajaribu kulinda hadhi yake dhidi ya Costa Rica mjini Belo Horizonte. Lakini kikosi hicho kutoka America ya kati , kina lengo la kupata nafasi ya kwanza na kimejiweka tayari kwa washindi wa pili wa kundi C katika kinyang'anyiro cha timu 16 bora.

Viongozi wa kundi C Colombia , kikosi kingine kutoka Amerika ya kusini kinachotoa changamoto kwa vigogo wa kanda hiyo , imefuzu kuingia katika timu 16 ikiwa na points 6 lakini itatafuta uwezekano wa kunyakua nafasi ya kwanza wakati itakapoumana na Japan , Samurai wa buluu, ambayo ina point moja mjini Cuiaba.

Fifa WM 2014 Elfenbeinküste Kolumbien
Mpambano kati ya Cote D'Ivoire na ColombiaPicha: Reuters

Japan inaweza kuingia katika awamu ya mtoano ya timu 16 iwapo itashinda lakini Cote d'Ivoire , ambayo kwa sasa inashikilia nafasi ya pili katika kundi hilo , ina nafasi kubwa kufuzu, kabla ya pambano lake la Ugiriki , ambayo ina point moja. Mshindi wa kundi C atapambana na mshindi wa pili wa kundi D katika awamu ya mtoano.

Uingereza yataka kulinda hadhi

Kocha Roy Hodgson wa Uingereza anataka kuteremsha dimbani kikosi cha majaribio . Mlinzi wa kati Gary Cahill na mshambuliaji Daniel Sturridge watakuwa wachezaji pekee ambao wataingia uwanjani kutoka kikosi kilichopoteza mchezo siku ya Alhamis kwa mabao 2-1 dhidi ya Uruguay mjini Sao Paulo. Lakini Hodgson anasisitiza kuwa licha ya kumuengua mshambuliaji Wayne Rooney na nahodha Steven Gerrard , itakuwa hakuna la kutafuta isipokuwa ushindi tu.

Ben Foster atalinda lango, Phil Jones mlinzi wa kulia , Cahill atakuwa mlinzi wa kati pamoja na Chris Smalling , na kijana chipukizi Luke Shaw atakuwa mlinzi wa pembeni kushoto.

Fifa WM 2014 Elfenbeinküste Kolumbien
Mashabiki wa ColombiaPicha: Getty Images

Kiungo kitajengwa na James Milner , Frank Lampard , Jack Wilshere, Ross Barkley na Adam Lalllana , na mshambuliaji ni Sturridge, amesema Hodgson.

Tembo wa Cote d'Ivoire

Cote d'Ivoire itachukua tahadhari sana katika mchezo wake na Ugiriki leo, amesema kocha Sabri Lamouchi, akikataa kutoa majina ya kikosi chake wakati kikosi hicho cha Tembo wa Cote d'Ivoire kikiwania kuingia katika awamu ya mtoano kwa mara ya kwanza katika mashindano hayo.

Kikosi hicho cha Tembo wa Cote d'Ivoire kiko tu nyuma ya Colombia katika kundi C kikiwa kimepata ushindi mara moja na kufungwa mara moja, kitawania kupata mabao lakini pia kuiweka safu yake ya ulinzi kuwa imara bila kuruhusu bao wakati wanataka kupata ushindi ili kuwa na uhakika wa kuingia katika awamu ya timu 16.

Interaktiver WM-Check 2014 Trainer England Hodgson
Roy Hodgson kocha wa UingerezaPicha: Getty Images

Mchezaji wa zamani wa Cameroon Roger Milla amelaumu udhaifu uliojitokeza katika kikosi hicho cha Simba wanyika katika kombe la dunia kwa kile alichodai kuwa ni uroho wa fedha wa maafisa wa shirikisho la kandanda nchini Cameroon , utovu wa nidhamu wa wachezaji na kocha ambaye hana makini.

Milla amesema kuwa Cameroon inahitaji kujitoa kutoka mashindano ya kimataifa na kulenga katika kujenga taswira nzuri ya soka ya nchi hiyo.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre

Mhariri Mohammed Abdul Rahman