1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kufuatia mauaji ya Mazeruzeru nchini Tanzania Serikali yatoa tahadhari kwa wananchi kuhusu Waganga wa jadi.

Scholastica Mazula3 Aprili 2008

Serikali ya Tanzania,imesema itahakikisha inachukua hatua kali ili kukabiliana na mauaji ya mazeruzeru ambayo yamekuwa yakifanyika nchini humo kwa imani za kishirikina.

https://p.dw.com/p/DbQN
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Rais George .W. Bush wa Marekani, nchini Tanzania.Picha: AP

Hatua hiyo imetangazwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa nchi hiyo jana wakati akizungumza na wazee Mjini Dar es Salaam, ikiwa ni utaratibu wake wa kulihutubia Taifa kila mwisho wa mwezi.

Rais Jakaya Kikwete amesema mauaji yanayotokana na imani za kishirikina ni tatizo la muda mrefu nchini humo hata kabla na wakati wa ukoloni na yameendelea hata baada ya Uhuru wa nchi hiyo.

Amesema mauaji mengi ya Kishirikina hufanyika kutokana na imani potofu walizonazo baadhi ya watu kwamba kwa kutumia viungo vya watu wengine wanaweza kufanikiwa katika biashara wanazozifanya au katika shughuli za uchimbaji madini na uvuvi.

Tangu mwezi Julai mwaka 2007, kumekuwa na taarifa za mauaji ya Mazeruzeru wakivamiwa na kuuawa na wengine kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Rais Kikwete amesema kuanzia mwezi Machi mwaka 2007 hadi April mosi mwaka huu, jumla ya Mazeruzeru kumi na tisa wameuawa na wengine wawili mpaka sasa hawajulikani waliko.

Katika kuhakikisha tatizo hilo linakomeshwa, Rais Kikwete amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa kushirikiana na wadau , wakiwemo waganga wa jadi waliosajiliwa na Serikali.

Amesema kwa kushirikiana na chama cha Mazeruzeru Tanzania, Serikali itaendelea na zoezi la kupata idadi kamili ya Maalbino wote nchini humo na sehemu wanazoishi ili waweze kuandaa mazingira ya ulinzi yatakayoweza kuwahakikishia usalama wao.

Aidha Rais Kikwete amelitaka jeshi la polisi la nchi hiyo kujipanga upya, kuyatambua na kuyakamata magenge ya watu wanaokodishwa kufanya mauaji hayo.

Haji Manala ni Katibu mwenezi wa chama cha Mapinduzi mjini Dar es Salaam na mwanachama wa chama cha Mazeruzeru nchini humo anasema tatizo kuu lililopo ni ukosefu wa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu mazeruzeru.

Hata hivyo anasema ongezeko la waganga wa jadi limechangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa vitendo kama hivyo kwani kila mtu anajaribu kutafuta mbinu za kuwavutia wateja wake na haamini kama viungo vya Maalbino vinaweza kumletea mtu yeyote utajiri.

Kwa mujibu wa rais Kikwete uzoefu unaonyesha kwamba baadhi ya wahanga wanaoathirika na mauaji hayo ni akina mama vikongwe ambao hutuhumiwa kuwa ni wachawi.

Idadi kubwa ya mauaji ya namna hiyo hutokea katika mikoa ya kanda ya Ziwa, ambayo ni Mara, Shinyanga, Mwanza na hata Mkoa wa Tabora nchini humo.

Tiba ya asili na Uganga wa jadi ni sehemu ya asili ya Watanzania, Rais Kikwete amesema Serikali inatambua jambo hilo na wala haikatazi, hata hivyo ametoa wito kwa Watanzania kujiepusha na matapeli waliyoiingilia kazi hiyo wenye nia ya kuwalaghai kwamba kwa kufanya hivyo watakuwa matajiri.

Amesema mauaji ya Mazeruzeru yanayo kwenda sambaba na kunyofolewa kwa baadhi ya viungo vyao ni aibu kwa Taifa hilo na ni ukatili mkubwa, watu wanapaswa kuachana na dhana ya kwamba utajiri huja kwa njia ya miujiza pasipo kufanya kazi kwa bidii.