1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kukombolewa Nahodha Phillips ni ushindi kwa Obama?

-13 Aprili 2009

Wadadisi wa mambo wapongeza mkakati wa Obama wa sera za nje kufuatia kukombolewa nahodha aliyekuwa katekwa nyara na maharamia Somalia

https://p.dw.com/p/HViv
Kulia ni Nahodha wa meli ya Marekani ya Maersk-Alabama Capt. Richard Phillips, akipokewa na Kamanda Frank Castellano, baada ya kukombolewa kutoka kwa maharamia.Picha: AP

Kufanikiwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwa opresheni ya Marekani ya kumkomboa nahodha wa meli ya mizigo ya Marekani aliyekuwa amezuiliwa mateka na maharamia wakisomali katika pwani ya Somalia ni hatua ambayo pia imemnusuru rais Barack Obama katika matatizo ya sera zake za nje.

Utawala wa Marekani ulikuwa ukichukua tahadhari kutolipa suala hilo umuhimu mkubwa wakati kukifanyika mazungumzo juu ya kuachiliwa huru nahodha huyo.

Utawala wa rais Barack Obama umelichukulia suala la kutekwa nyara Nahodha wa meli yake ya mizigo katika pwani ya Somalia na maharamia kwa uangalifu mkubwa bila ya kuliaangazia kwa kishindo suala la kufanyika mazungumzo ya chinichini ya kutaka kuachiliwa huru nahodha huyo.


Hadi dakika za mwisho binafsi rais Obama hakuwahi kutoa tamko ili kuonyesha hali ya kutolipa umuhimu suala hilo ikizingatiwa kuna changamoto nyingine za mambo ya nje zinazoukabili utawala wake kuanzia suala la Korea Kaskazini,Iran Afghanistan na kwingineko.

Maersk Alabama nach Piraten-Entführung im Hafen vom Mombasa
Meli ya Maersk Alabama ikijiandaa kutia nanga katika bandari ya Mombassa,Kenya, jumamosi April 11, 2009.Picha: AP

Kutokana na kukombolewa nahodha huyo katika opresheni ya kijeshi,Obama ameepukana na fedheha iliyomkumba rais Bill Clinton mwaka 1993 wakati wanajeshi 18 wa Marekani walipouwawa nchini Somalia wakijaribu kumsaka mbabe wa kivita Mohammed Farah Aideed katika mapambano yaliysababisha janga kubwa na hata kufungua njia ya kuandikwa kitabu na kutengenezwa filamu inayoitwa ''BackHawk Down''


Wataalamu wa mambo wanasema kwamba mzozo huo wa kutekwa nyara nahodha wa meli ya mizigo ya Marekani ungemalizikia kinyume chake basi hali hiyo ingesababisha dosari katika sifa ya sera za Obama kuhusiana na usalama wa kitaifa na kuwapa wakosoaji na hasa upinzani unaongozwa na chama cha Republican,silaha ya kuonyesha ni kwa jinsi gani Obama ni dhaifu linapokuja suala la usalama na vita dhidi ya Ugaidi.


Na kwahivyo basi ushindi wa kukombolewa nahodha huyo umemuonyesha dhahiri kiongozi huyo wa Marekani kuwa mtu jasiri katika suala la usalama.

Haikujulikana wazi ni kwa kiasi gani rais Obama amehusika katika kufanikisha shughuli za kumkomboa nahodha Richard Phillip lakini taarifa aliyoitoa baadae imeonyesha anaamini kwamba serikali yake inabidi kuchukua jukumu kubwa katika kukabiliana na uharamia katika eneo la pwani ya Somalia.



Hata hivyo wadadisi wa mambo wanasema kwamba hivi sasa ikizingatia hali ya kwamba mkakati wa sasa wa kulijaza eneo hilo kwa meli za kivita ni jambo ambalo halijafanikiwa kwa kiasi kikubwa,walimwengu wanaachwa katika hali ya kusubiri na kuona ikiwa rais Obama atakuwa na mipango mingine.


Baadhi ya wataalamu wanasema opresheni za kijeshi za nchi kavu dhidi ya maficho ya maharamia ni uwezekano uliobakia ingawa hatua hiyo inaweza kuwatia hatarini mateka 270 kutoka nchi mbali mbali walioko kwenye mikono ya maharamia hao wanaozunguka nao katika ghuba ya Aden na bahari ya Hindi.


Sera nyingine inayoweza kuwa ya hatari zaidi ni kuwashughulisha zaidi wanajeshi wa Marekani kwani hilo linaweza kutoa uwezekano wa kurudi tena kwa jeshi hilo nchini Somalia ambako jarida linalozungumzia masuala ya sera za nje la Marekani limeitaja kuwa ni mahala hatari kabisa duniani.


Mwandishi Saumu Mwasimba-RTRE

Mhariri Mohd Abdul-Rahman