1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuku ndiye ndege mwenye akili zaidi

Mohammed Khelef
4 Januari 2017

Wakati kwenye jamii nyingi duniani, mtu mjinga hufananishwa na kuku, wanasayansi wanasema ukweli ni kuwa kuku ndiye ndege mwenye akili zaidi kuliko ndege wote ulimwenguni.

https://p.dw.com/p/2VEKp
Weißes Huhn
Picha: Fotolia/Ramona Heim

Jarida la kisayansi liitwalo "Animal Cognition" (Utambuzi wa Wanyama) limechapisha makala ya kitafiti inayoonesha kuwa kuku wana tabia zao binafsi na za peke yao, ambazo aina nyengine ya ndege na wanyama hawana. 

Kwa mujibu wa utafiti huo, kuku wana uwezo wa kutaniana na kufanyiana ujanja wenyewe kwa wenyewe. Wanaweza pia kuwatambua watoto wa binaadamu hadi miaka saba na wakiwa nao huwatendea tafauti na watu wazima.

Mama mwenye vifaranga ana uwezo wa kuwahesabu watoto wake na kujuwa idadi yao tangu siku wanayoanguliwa, na anaendelea kujuwa kila mmoja anapotoweka. 

Kuku pia wana hisia kali za familia na ulinzi wa watoto wao. 

Kuku ndiyo ndege wanaochinjwa kwa wingi zaidi duniani ikiwa ni mara mbili ya wanyama wengine. Inakisiwa kuwa kuna kuku bilioni 20 kote ulimwenguni.

Jarida hilo linasema licha ya kuwa watu kwenye nchi za kiviwanda ndio walaji wakubwa wa kuku, wengi wao hawajawahi kuwaona kuku wakiwa hai kwenye maeneo wanayofugwa.

"Imani kuwa kuku ni wapumbavu huenda ikasutwa na ukweli kuwa kuku ni ndege wenye akili sana." Linasema jarida hilo. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa
Mhariri: Grace Kabogo