1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kumshtaki rasmi Rais Bashir ni hatari,wasema AU

Mwadzaya, Thelma15 Julai 2008

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika anaonya kuwa ghasia huenda zikasambaa nchini Sudan endapo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC itamshtaki rasmi Rais wa nchi hiyo Omar Hassan al Bashir.

https://p.dw.com/p/EcbS
Rais wa Sudan Omar Hassan al BashirPicha: AP


Hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya nje wa Tanzania Bernard Membe aliyezungumza na shirika la habari la AFP kwa niaba ya Mwenyekiti wa Umoja huo Rais Jakaya Mrisho Kikwete.


Mwendesha mashtaka mkuu Louis Moreno Ocampo aliiagiza Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC kutoa hati ya kukamatwa kwa Rais Omar al Bashir kwa madai 10 ya mauaji ya halaiki,uhalifu dhidi ya ubinadamu vilevile uhalifu wa kivita kwenye eneo la Darfur la Sudan.


Endapo ombi hilo litaidhinishwa hii itakuwa mara ya kwanza kwa rais aliye madarakani kushtakiwa kwa madai ya mauaji ya halaiki.Hata hivyo Rais Bashir hatofikishwa mahakamani kwa sasa.Sudan kwa upande wake ilipinga vikali hatua hiyo.


Marekani kwa upande wake inaripotiwa kuimarisha usalama wa wafanyakazi wake nchini Sudan kwa kuhofia ulipizaji kisasi.


Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa yapata watu laki tatu wamepoteza maisha yao tangu vita kuanza kwenye eneo la Darfur na wengine yapata milioni mbili u nusu kuachwa bila makazi.Vita katika eneo hilo vilianza mwezi Februari mwaka 2003.Serikali ya Sudan kwa upande inashikilia kuwa watu alfu 10 pekee ndio waliopoteza maisha yao katika ghasia hizo.