1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuna matumaini wasichana wa Chibok wako hai

14 Aprili 2016

Video inayoonekana kuwaonyesha baadhi ya wasichana waliotekwa nyara katika shule ya Chibok kaskazini mwa Nigeria imerushwa hewani pamoja na picha za wazazi waliojaa majonzi wakiwatambua mabinti zao

https://p.dw.com/p/1IV7I
Nigeria Demonstration Bring Back Our Girls in Chibok
Picha: Reuters/A. Akinleye

Wasichana hao hawajawahi kuwasiliana na wazazi wao tangu walipotekwa nyara na kundi la itikadi kali la Boko Haram miaka miwili iliyopita. Televisheni ya CNN hapo jana imeonyesha video, inayoaminika kutengenezwa Desemba mwaka jana, ya wasichana waliovaa hijabu za kiislamu ambapo mama mmoja anaonekana akiisogea skrini ya kompyuta wakati akimtambua binti yake. Kisha anaangua kilio akisema “Saratu wangu”.

Mnamo usiku wa Aprili 14, 2014, Boko Haram iliwateka nyara wasichana wa shule 276 kutoka Shule ya Sekondari ya Serikali katika mji wa kaskazini mashariki wa Chibok. Wasichana kadhaa walifanikiwa kutoroka, lakini 219 wangali hawajulikani waliko. Tukio hilo lilizusha kampeni ya kimataifa iliyopewa kichwa cha Bring Back Our Girls, yaani Warejeshe Wasichana Wetu.

Nigeria Jahrestag Entführte Schulmädchen Boko Haram
Kumbukumbu ya miaka miwili tangu utekaji wa ChibokPicha: Reuters/A. Sotunde

Aliya Yesufu ni balozi wa kikundi kinachojiita Bring Back Our Girls "Nahisi huzuni sana na nimekata tamaa na serikali yetu kwa kushindwa kuwarudisha wasichana wa Chibok haraka iwezekanavyo, kwa sababu nahisi ikiwa ningekuwa mmoja wa wasichana wa Chibok, ningekuwa bado kifungoni na sidhani kama kuna yeyote angependa hilo".

Kushindwa kwa maafisa wa Nigeria na jeshi kuwaokoa wasichana hao kulisababisha shutuma za kimataifa na kuchangia katika Rais Goodluck Jonathan kupoteza uchaguzi wa mwaka jana. Marekani, Uingereza na Ufaransa zilikuwa miongoni, waliotuma washauri, wakiwemo wataalamu wa matukio ya utekaji nyara. Ndege za Uingereza na Marekani zisizoruka na rubani ziligundua angalau kunfi moja la karibu wasichana 80, na kuripoti kwa serikali na jeshi la Nigeria, lakini hakuna kilichofanyika.

Andrew Pocock, ambaye alikuwa balozi wa Uingereza nchini Nigeria hadi alipostaafu mwaka jana, aliliambia jarida la The Sunday Times mwezi uliopita kuwa ilichukuliwa kuwa hatari zaidi kwa wasichana wengine kujaribu kuanzisha operesheni ya nchi kavu au ya angani. Jeshi la Nigeria pia lilitaja hofu sawa na hiyo.

Esther Yakubu ni mama wa mmoja wasichana waliotekwa. "Sijui mbona watoto wengine watapatikana na sio wasichana wetu. Mbona hakuna hata mmoja? Tunajua hatutawapata wote, lakini tunataka kumwona hata mmoja ili atusimulie hadhiti ya kilichotokea kwa wengine. Hivyo ikiwa Boko Haram wametokomezwa bila wasichana wetu sidhani kama Boko Haram wametomokezwa".

Nigeria Trauer - von Boko Haram entführte Mädchen
Wazazi wa wasichana wa Chibok bado wanauliza maswaliPicha: DW/K. Gänsler

CNN imeripoti kuwa video hiyo inayodhibitisha wasichana hao wako hai ilitumwa mwezi Desemba kwa wapatanishi wanaojaribu kuongoza juhudi za kuachiliwa huru wasichana hao. Waziri wa Habari Lai Mohammed amesema serikali inaitathmini na kuichunguza video hiyo.

Mmoja wa wasichana hao 15 anasema kwenye video hiyo "sote tuko salama," akisisitiza neno “wote”. Kumekuwa na hofu kuwa mbinu ya Boko Haram kuendelea kuwatumia wasichana kufanya mashambulizi ya mabomu ya kujitoa mhanga inaashiria kuwa wanawageuza mateka kuwa silaha, wakiwemo wasichana wa Chibok.

Hakujawa na ujumbe wowote kutoka kwa wasichana hao tangu Aprili 2014, wakati kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau aliposema walibadili dini na kuingia katika Uislamu na kutishia kuwauza katika utumwa au ndoa za lazima na wapiganaji wa kundi hilo.

Wengi wa walioachiliwa huru karibuni ni wajawazito. Makamu wa Rais wa Nigeria Yemi Osinbajo anatarajiwa kuhudhuria leo mjini Chibok kumbukumbu ya miaka miwili tangu kutekwa wasichana hao.

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Caro Robi