1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi jipya la wakimbizi wa Kiiraki lawasili Ujerumani leo hii

19 Machi 2009

Tangu miaka mingi nchini Ujerumani kundi kubwa kabisa la wakimbizi ni wakimbizi kutoka Irak. Na hii leo unaanza utaratibu wa kuwapokea wakimbizi wengine 2,500 kutoka nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/HFGB

Hiyo ni idadi ya wakimbizi wa Kiiraki ambayo Ujerumani ipo tayari kuchukua katika mwaka huu. Ndege ya kwanza itawasili leo mchana katika uwanja wa ndege wa Hannover-Langenhagen, ikiwa na Wairaki waliokuwa wakiishi katika kambi za wakimbizi nchini Syria na Jordan. Muandishi wetu Eva Völker amechunguza hali ya wakimbizi wa Kiiraki wanaoishi Ujerumani tangu miaka mingi.

Ghassan El-Zuhairy ni miongoni mwa wakimbizi 72,000 wa Kiiraki wanaoishi Ujerumani hivi sasa. Mkasa wa mkimbizi huyo mwenye umri wa miaka 30 ulianza mwaka 2002 alipotaka kwenda Sweden kwa mchumba wake kwa kupitia Ujerumani. Lakini msafiri huyo alieingia Ujerumani kinyume na sheria alikamatwa na polisi ndani ya treni.Kuambatana na sheria za Ulaya kuhusu wakimbizi, El-Zuhairy alilazimika kubakia Ujerumani na kesi ya kuomba hifadhi ya ukimbizi ikafunguliwa.Ombi hilo likakataliwa. Kwa hivyo,tangu Septemba mwaka 2002 El-Zuhairy anavumiliwa tu kubakia nchini.Je nini maana ya kuvumiliwa? Kwa mujibu wa Kai Weber wa Baraza la Wakimbizi katika jimbo la Niedersachsen,mtu anaevumiliwa huruhusiwa kubakia bila ya hati halali kwa muda usiojulikana mpaka utaratibu wa kumrejesha kule alikotokea utakapokamilishwa. Lakini El Zuhairy anasema:

"Kwa kweli mimi sina familia. Sijabakiwa na ye yote katika familia yangu huko Baghdad, Irak. Kwa hivi sasa haiwezekani kabisa kurejea Irak -huko kuna umwagaji damu."

Kai Weber anasema kuwa haiwezekani kuwarejesha nyumbani wakimbizi wa Kiiraki hivi sasa kwa sababu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini humo. Na hakuna matumaini kuwa hali hiyo itabadilika hivi karibuni. Kwa hivyo,anaamini itakuwa sawa kuwapa Wairaki wanaovumiliwa vibali vya kuwaruhusu kuishi Ujerumani, hali halisi ya huko Irak ikizingatiwa.

Watu wanavumiliwa kubakia Ujerumani kama vile El-Zuhairy hukabiliana na vizingiti vingi. Kwa mfano yeye anaishi Northeim katika jimbo la Niedersachsen na haruhusiwi kusafiri nje ya eneo hilo. Kwa sababu hiyo, El-Zuhairy aliesomea ufundi wa vyuma, amepoteza nafasi yake ya kazi kwani hakuweza kutumwa kikazi nje ya kule anakoishi.El-Zuhairy amejifunza lugha kwa bidii yake mwenyewe lakini bila ya kuwa na kibali cha kuishi kihalali nchini basi ni vigumu sana kwa El-Zuhairy kujijumuika katika jamii ya Kijerumani.Kwa maoni ya Weber, hiyo ni hali isiyokubalika hasa hii leo wakimbizi zaidi wa Kiiraki wakipokewa kutoka Syria na Jordan. Anasema:

"Mtu upande mmoja hawezi kusema kuwa kwa sababu ya hali inayokutikana Irak tunawachukua wahanga wa vita, na upande mwingine kufikiria vipi watu hao wataweza kurejeshwa huko."

El-Zuhairy angefurahi kupewa matumaini ya kuwa maisha mapya nchini Ujerumani,kwani ile ndoto ya kwenda Sweden imetoweka.Mchumba wake alimngojea miaka mitano mizima. Baadae akakata tamaa na sasa ameolewa na mtu mwengine.

Mwandishi; Prema Martin/Völker/ZR

Mhariri: Miraji Othman