1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KUNDI LA G-8 LITIMIZE AHADI

P.Martin11 Mei 2007

Majuma machache tu yakibakia kabla ya kufanywa mkutano wa kilele wa kundi la nchi tajiri kabisa zilizoendelea kiviwanda(G-8),kwa mara nyingine tena mada mojawapo ni Afrika na mahitaji yake makuu.

https://p.dw.com/p/CHEU

Mawaziri Wakuu Hama Amadou wa Niger na Yawovi Agboyibo wa Togo juma hili walikuwepo mjini Berlin kuwasilisha madai yao kuhusika na ushirikiano wa kiuchumi pamoja na nchi tajiri zilizoendelea kiviwanda G-8.

Kama ilivyokuwa katika mikutano ya kilele iliyopita ya kundi la G-8,hata mwaka huu kumepangwa kufanywa mkutano maalum kuhusu bara la Afrika.Kwa mujibu wa afisa mmoja wa mkutano huo wa G-8,umuhimu utatolewa kwa masuala yanayohusika na maendeleo ya kiuchumi, njia za kupunguza umasikini na kupiga vita UKIMWI na virusi vya HIV.Lakini ahadi kama hizo zinazokaririwa na viongozi wa kundi la G-8 tangu miaka kadhaa, zimezusha hali ya shaka tu miongoni mwa wataalamu wa maendeleo na mashirika yasio ya kiserikali.

Kwa mfano maaskofu wa Kanisa Katoliki kutoka nchi za Kiafrika na Bara la Ulaya walipokutana juma hili mjini Berlin walisema,wamevunjika moyo kwani hakuna maendeleo yaliofanywa upande wa kundi la G-8.

Kuambatana na Shirika la Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo-OECD ambalo hujumuisha nchi 30 tajiri, misaada ya maendeleo kwa nchi za Kiafrika zilizo kusini mwa Sahara,iliongezeka kwa asilimia 2 tu. Ongezeko hilo dogo,ni tofauti kabisa na ahadi kubwa zilizotolewa katika mkutano wa Gleneagles huko Scotland mwaka 2005 kuwa misaada kwa nchi za Kiafrika itaongezwa kwa maradufu ifikapo mwaka 2010.

Kwa mujibu wa mwanamuziki wa zamani Bob Geldof aliepata umaarufu katika miaka ya 80 alipozindua kampeni ya kupiga vita UKIMWI barani Afrika kwa kupanga mlolongo wa tamasha za muziki,tatizo si uhaba wa pesa bali tatizo ni uhaba wa mawazo.Yeye anaendelea kukusanya pesa kusaidia miradi ya maendeleo barani Afrika.

Wataalamu mbali mbali waliokusanyika Berlin juma hili wamependekeza mradi wa hatua za kuchukuliwa kuzisaidia nchi za Kiafrika.Wameshauri masoko ya Ulaya na Marekani yafunguliwe kwa mazao ya nchi za Kiafrika;sekta za kilimo,afya na elimu hasa kwa wasichana na wanawake barani Afrika zisaidiwe kifedha;bila ya kusahau ujenzi wa miundombinu katika miji mikubwa hasa kuhusika na ugavi wa maji na kusafishwa kwa maji machafu yanayotoka majumbani.

Rasmi,mwaka huu masuala hayo yote yametiwa maanani katika ajenda ya mkutano wa G-8.Lakini maafisa wa Kijerumani hawakuficha ukweli kwamba maslahi ya G-8 barani Afrika yanahusika pia na utajiri mkubwa wa malighafi katika bara hilo na vipi nchi zinazoibuka kiuchumi kama vile India na China zinavyofanikiwa kujipatia raslimali hizo.

Kwa mfano,tangu mwaka 2000,biashara kati ya Afrika na China imeongezeka kwa mara tano hadi kufikia Dola bilioni 50 katika mwaka wa 2006.Na uwekezaji wa China katika nchi 43 za Kiafrika umepindukia Dola bilioni tano na nusu.Baada ya Marekani na Ufaransa,sasa kiuchumi,China ni mshirika mkuu wa tatu wa bara la Afrika. Kufuatia hali hiyo mpya iliyochomoza,Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema,dhima ya kulisaidia bara la Afrika isiachiwe Jamhuri ya Watu wa China.

Kuanzia tarehe 6 hadi 8 mwezi Juni,viongozi wa serikali za kundi la G-8 yaani Ujerumani, Uingereza,Ufaransa,Kanada,Italia,Japan,Urusi na Marekani watakutana nchini Ujerumani katika mji wa mapumziko wa Heiligendamm.