1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la Polisi wa kutuliza ghasia nchini Ukraine la Berkut limevunjiliwa mbali

Mjahida 26 Februari 2014

Kaimu rais wa Ukraine Oleksander Turchinov ameanza rasmi majukumu yake kama mkuu wa jeshi la Ukraine. Huku kundi la polisi wa kutuliza ghasia wanaodaiwa kusababisha mauaji ya waandamanaji mjini Kiev likivunjwa.

https://p.dw.com/p/1BFUs
Polisi wa kutuliza ghasia wa Berkut
Polisi wa kutuliza ghasia wa BerkutPicha: picture alliance/CITYPRESS 24

Hatua ya kaimu rais Oleksander Turchinov kuchukua rasmi jukumu la mkuu wa jeshi imetangazwa katika mtandao wa serikali ya Ukraine.

Wakati huo huo waziri mpya wa maswala ya ndani nchini Ukraine Arsen Avakov, amesema kikosi cha polisi wa kupambana na ghasia Berkut, kinachohofiwa nchini humo na kinachodaiwa kusababisha mauaji ya waandamanaji mjini Kiev kimevunjwa

Bunge la Ukraine limekuwa likichukua hatua ya kuzivunja au kuzifanyia mabadiliko taasisi zinazohusishwa na rais aliyeondolewa Viktor Yanukovych, ambaye hadi sasa mienendo yake haijulikani.

Kaimu rais wa Ukraine Oleksander Turchinov
Kaimu rais wa Ukraine Oleksander TurchinovPicha: picture-alliance/Itar-Tass/Maxim Nikitin

Katika hatua ya mgawanyiko inyoonekana kwa wabunge wa upinzani katika serikali iliopita, hapo jana uundwaji wa serikali ya mpito uliahirishwa hadi siku ya Alhamisi.

Baraza jipya la mawaziri kutangazwa

Mbunge anayetokea chama cha kiongozi wa upinzani cha Udar,Valeriy Patskan, amesema wanachama wa baraza jipya la Mawaziri wanatarajiwa kutangazwa leo katika uwanja wa Uhuru mjini Kiev.

Aidha wanaharakati wamedai viongozi wa maandamano yaliodumu kwa takriban miezi mitatu katika uwanja huo wa Uhuru au Maidan wanapaswa kupewa nafasi katika baraza la mawaziri.

Bunge la Ukraine
Bunge la UkrainePicha: Reuters

Kwa sasa Wabunge nchini Ukraine wamepiga kura kuiomba mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC mjini The Hague, kumshtaki rais wa zamani Viktor Yanukovych. Mashtaka hayo yanahusiana na vifo vya raia kadhaa wakati wa maandamano mjini Kiev wiki iliyopita.

John Kerry azungumzia ghasia ya Ukraine

Akizungumzia ghasia za Ukraine, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry amesema lililo muhimu kwa sasa ni raia wa Ukraine kufanya maamuzi juu ya mustakabal wao na wa nchi yao.

"Hili linawahusu watu wa Ukraine, waukraine kufanya maamuzi juu ya maisha yao ya usoni na tunataka kufanya kazi na Urusi na nchi nyengine, na watu wote wengine kuhakikisha kuwa haya yote yanaendelea kwa amani, kwa sababu ghasia zilizoonekana nchini humo ilikuwa ni mshituko kwa kila mtu duniani," Alisema John Kerry.

Kwa upande wake Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov ametoa wito kwa shirika linaloangalia masuala ya demokrasia ya Ulaya, Jumuiya ya usalama na ushirikiano barani ulaya kulaani ukuaji wa matamshi ya kizalendo na kifasishti katika eneo la magharibi mwa Ukraine.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei LavrovPicha: Reuters

Katika taarifa yake, hapo jana Lavrov amesema jumuiya hiyo OSCE inapaswa kulaani hatua za wazalendo kupiga marufuku lugha ya kirusi nchini Ukraine. Hata hivyo shirika hilo bado halijatoa tamko lolote juu ya hilo.

Kuna hofu kubwa kwamba Ukraine inaweza kugawika kutokana na vuguvugu la watu wanaopenda mtengano kukiwa na wasiwasi juu ya kujitenga kwa eneo la Crimea ambapo warusi wa eneo hilo wanataka kulidhibiti eneo hilo baada ya mabadiliko ya utawala mjini Kiev.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed AbdulRahman