1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuondolewa Sharif kwazusha mashaka Pakistan

Iddi Ssessanga
28 Julai 2017

Pakistan iko hatarini kutumbukia katika machafuko ya kisiasa baada ya utulivu wa muda, kufuatia hatua ya kuondolewa waziri mkuu Nawazi Sharif kwa tuhuma za rushwa. Sharif anazuwia kushika wadhifa wa kisiasa maishani.

https://p.dw.com/p/2hKWN
Pakistan Premierminister Nawaz Sharif
Picha: Getty Images/AFP/K. Fukuhara

Chama cha Sharif kinachotawala cha Pakistan Muslim League - Nawaz (PML-N) kilichoshinda wingi wa viti vya bunge mwaka 2013, kinatarajiwa kumteuwa waziri mkuu mpya kushikilia wadhifa huo hadi mwakani utakapofanyika uchaguzi mkuu. Miongoni mwa washirika wanaopigiwa chapuo kuchukuwa nafasi ya Sharif ni waziri wa ulinzi Asifa Khawaja, waziri wa mipango Ahsan Iqbal na waziri mafuta Shahid Abbasi.

Kuondolewa kwa Sharif mwenye umri wa miaka 67 ambaye amehudumu kama waziri mkuu kwa vipindi vitatu tofauti, pia kunazusha maswali kuhusu demkorasia tete ya taifa hilo. Hakuna waziri mkuu aliewahi kumaliza muhula kamili madarakani tangu Pakistan ilipopata uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1947.

Hukumu ya mahakama ni ushindi muhimu wa kisiasa kwa kiongozi wa upinzani Imran Khan, nyota wa zamani wa mchezo wa Cricket ambaye mwaka uliopita alitishia kuitisha mandamano ya umma katika mitaa ya nchi hiyo kama utajiri wa Sharif usingechunguzwa. Khan alitumia ufichuzi wa nyaraka za Panama zilizofichua kuwa familia ya Sharif ilikuwa imenunua majumba ya kifahari mjini London kwa kutumia kampuni za nje, kuhalalisha hoja yake.

Pakistan Gegner von Premierminister Nawaz Sharif in Islamabad
Wapinzani wa Nawaz Sharif wakishangilia uamuzi wa mahakama ya juu kumn'goa mamlakani.Picha: Reuters/C. Firouz

Uamuzi wa kihistoria kwa Pakistan

"Uamuzi huu utakuwa na maana kubwa kwa upinzani, uamuzi huu utakuwa na maana kwa demokrasia ya Pakistan. Uamuzi huu unaweza kuingia katika vitabu vya historia. Ingawa kuna maoni ya aina mbili kuhusu uamuzi huu, kwamba iwapo utaimarisha demokrasia au iwapo utadhoofisha demokrasia, lakini katika muktadha mpana zaidi uamuzi huu utakuwa wa kihistoria kwa kuifanya Pakistan kuondokana na rushwa," alisema mchambuzi wa siasa Mahzar Abbas.

Sharif amedai kuwepo na njama dhidi yake, ingawa hakutaja mtu yeyote. Washirika wale lakini, faragahani wanazungumzia juu ya baadhi katika idara ya mahakama na jeshini, ambao Sharif hana uhusiano mzuri nao, kuwa wanafanya nhujuma dhidi yake. Jeshi linakanusha ushiriki wowote.

Jopo la majaji watano wa mahakama ya juu kabisaa ya Pakistan iliamua kwa sauti moja kwamba Sharif anapaswa kuondolewa baada ya timu ya uchunguzi kudai kuwa familia yake ilishindwa kutoa maelezo juu ya utajiri mkubwa ilio nao. Washirika wake wanasema mahakama hiyo imepindukia mipaka yake na wanahoji kuwa hakuna mashitka yoyote ya rushwa au matumizi mabaya ya madaraka yamethibitishwa, na wala hajatiwa hatiani.

Hatari ya machafuko ya kisiasa

Wachamabuzi wameonya kuwa machafuko mengine ya kisiasa yatawatisha wawekezaji wa kigeni, ambao tayari wana wasiwasi kuwekeza Pakistan, kutokana na hofu za kiusalama na mazingira magumu ya uwekezaji. Sharif amekuwa akikanusha mara zote kutenda makosa yoyote na amepinga uchunguzi dhidi yake na kuutaja kuwa wa upendeleo na usiosahihi.

Pakistan Oppositionsführer Imran Khan vor Oberster Gerichtshof in Islamabad
Kiongozi wa upinzani Imran Khan, alieanzisha harakati za kushinikiza waziri mkuu Nawaz Sharif achunguzwe.Picha: picture-alliance/AP Photo/B.K. Bangash

Waziri wa usafiri wa reli Khawaji Saad Rafiq aliandika kwenye ukurasa wake wa twita kabla ya saa kadhaa kabla ya uamuzi kutangazwa, kwamba kinachofanyika siyo uwajibikaji bali kisasi, na kuongeza kuwa katika juhudi za kukiondoa chama cha PML-N madarakani, mfumo wa demokrasia umelengwa.

Mihula miwili ya mwisho ya Sharif ilikatishwa pia, ikiwemo na mapinduzi ya kijeshi mwaka 1999, lakini alirudi kutoka uhamishoni na kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu mwaka 2013. Mahakama hiyo ilisema mwezi Aprili kwamba hakukuwa na ushahidi wa kutosha kumuondoa Sharif madarakani, lakini iliagiza uchuguzi uliohusisha wanachama wa mashirika ya ujasusi ya kijeshi.

Wachambuzi wanataraji Sharif atafanya ushawishi kwa mmoja wa washirika wake kuunda serikali, hadi uchaguzi utakapofaynika mwakani, wakati ndugu yake Shahbaz, ambaye ni waziri kiongozi wa jimbo la Punjab, atakapochukuwa uongozi wa chama.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre

Mhariri: Josephat Charo