1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya maoni ikikaribia Sudan wasiwasi waongezeka

Saumu Ramadhani Yusuf19 Oktoba 2010

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wapelekwa Abyei

https://p.dw.com/p/PhTt
Rais wa Sudan Kusini inayotaka kujitenga Salva KiirPicha: AP

Umoja wa Mataifa umepeleka wanajeshi wake wa Kulinda amani katika jimbo lenye utajiri wa mafuta la Abyei huko nchini Sudan.Hatua hiyo ya Umoja wa Mataifa inafuatia kuongezeka kwa wasiwasi  wa kuzuka machafuko wakati jimbo hilo likijiandaa kupiga kura ya kuamua juu ya hatma yake. Zoezi hilo limepangiwa kufanyika wakati mmoja na zoezi la kura ya maoni juu ya kutaka kujitenga kwa Sudan Kusini.

Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa mataifa nchini Sudan,UNMIS,Haile Menkerios amesema tayari wameshapeleka wanajeshi wake wa ziada kiasi cha 100 katika jimbo hilo la Abyei kufuatia kuongezeka kwa wasiwasi wa kutokea machafuko.

Kura ya kuamua hatma ya jimbo hilo lenye utajiri wa mafuta itafanyika siku moja na zoezi la kura ya maoni kuhusu kutaka kujitenga kwa Sudan Kusini.Kura zote mbili zinafanyika chini ya makubaliano ya amani ya mwaka 2005 yaliyofanikisha kumaliza vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe kati ya kaskazini ambako kuna idadi kubwa ya waislamu na kusini kunakokaliwa na idadi kubwa ya wakristo.Hata hivyo viongozi wa pande zote mbili wamekuwa wakivutana juu ya nani anapasa kupiga kura katika jimbo hilo la Abyei.

UNMIS im Südsudan
Jimbo la Abyei lina utajiri mkubwa wa mafutaPicha: UNMIS/Frederic Noy

Watu wa kabila la Misseriya wenye asili ya kiarabu na wafugaji ambao wanaitumia ardhi ya jimbo hilo la Abyei kwa msimu  kulisha mifugo wao wametishia  kuvuruga zoezi la kura ya maoni  ikiwa hawatopewa haki sawa ya kupiga kura  kama watakavyopewa watu wa kabila la Dinka Ngok wakulima wakudumu  katika jimbo hilo ambao wanaonekana kupendelea jimbo hilo lijiunge na upande wa kusini.Abyei ni jimbo lililoko kati kati ya Kaskazini na Kusini ya Sudan na hivyo basi limepangiwa kupiga kura ya kuamua itajiunga na upande gani.

 Mazungumzo kati ya pande zote mbili yalivunjika wiki iliyopita huko Adis Ababa Ethiopia ambapo afisa mmoja  kutoka kaskazini walisema kutokana na hali hiyo ni dhahiri kwamba itakuwa vigumu kwa zoezi la kupiga kura katika jimbo hilo la Abyei kufanyika kama ilivyopangwa.

Matamshi hayo yalizusha hamaki katika jimbo hilo na pia kutoka uongozi wa Sudan Kusini ambao baadhi ya maafisa wake wanatokea katika mkoa huo.

Aidha kwa mujibu wa balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Susan Rice,rais wa Sudan Kusini Salva Kiir ameonya kwamba kuna wasiwasi upande wa kaskazini huenda unajiandaa kwa vita na kwamba huenda wameshaanza kupeleka wanajeshi wake kuelekea kusini.

Mwanzoni mwa mwezi huu rais Salva Kiir  atoa mwito kwa mabalozi wa Umoja wa mataifa katika baraza la usalama waliotembelea Sudan kuongeza idadi ya wanajeshi wake katika eneo la mpakani ili kuunda sehemu ya usalama ya kilomita 32 kabla ya kufanyika kwa kura hiyo ya maoni ya Sudan Kusini itakayofanyika tarehe 9 mwezi Januari.

Hata hivyo hapo jana Umoja huo wa mataifa ulisema haujaamua juu ya suala hilo la kutuma wanajeshi zaidi katika eneo hilo la mpaka kati ya kaskazini na kusini ambako kuna  wasiwasi mkubwa ingawa inajishughulisha zaidi kuweka wanajeshi wa amani katika maeneo tete.

Mwandishi Saumu Mwasimba/AFPE

Mhariri:M. AbdulRahman