1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya maoni Sudan Kusini kufanyika kesho

Kabogo Grace Patricia8 Januari 2011

Kura hiyo itaamua iwapo eneo la Sudan Kusini lijitenge na kuwa taifa huru.

https://p.dw.com/p/zv6A
Rais wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir (Kulia) na kiongozi wa Sudan Kusini. Salva Kiir.Picha: picture-alliance/dpa

Rais wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir, amesema Sudan Kaskazini na Kusini huenda zikaunganisha nguvu zao kwa kufuata mfumo wa Umoja wa Ulaya, iwapo Wasudan Kusini watapiga kura ya kujitenga katika kura ya maoni hapo kesho. Matamshi hayo ameyatoa wakati akizungumza na kituo cha televisheni cha Al-Jazeera.

Rais Bashir amesema kuwa Wasudan Kusini pia wanaweza kupewa haki ya ukaazi wa bure, uhuru wa kwenda wanakotaka na kufanya kazi pamoja na haki ya kumiliki mali nchini Sudan, baada ya maeneo hayo mawili kugawanyika. Hata hivyo, amesema hawataweza kuwa na uraia wa nchi zote mbili.

Aidha, wajumbe watakaosimamia uchaguzi huo wanaendelea kuhakikisha hakuna hitilafu zozote ambazo zinaweza kujitokeza katika dakika za mwisho za kura hiyo ya kihistoria. Akizungumzia na Deutsche Welle kwa njia ya simu kuhusu maandalizi ya kura hiyo, Rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin William Mkapa anayeuongoza ujumbe maalum unaosimamia zoezi hilo la kihistoria alisema kuwa maandalizi hayo yamekamilika.

Aidha, Mkapa amesema maandalizi hayo katika upande wa vifaa vya kupigia kura, orodha ya vituo vya kupiga kura, wasimamizi wa vituo hivyo na waangalizi wa uchaguzi yamekamilika. Ameongeza kusema kuwa usalama katika maeneo ya kupiga kura ni nzuri.

Kura hiyo ya maoni itakayopigwa kuanzia kesho hadi tarehe 15 ya mwezi huu wa Januari, inatokana na mkataba wa amani wa mwaka 2005 uliomaliza vita vya miongo kadhaa vya wenyewe kwa wenyewe kati ya Kaskazini na Kusini. Vita hivyo ambavyo ni vya muda mrefu zaidi kuwahi kutokea barani Afrika vilisababisha kiasi watu milioni mbili kuuawa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE)

Mhariri: Mohamed Dahman