1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya maoni Sudan ya kusini

Sekione Kitojo9 Januari 2011

Siku ya Kura ya maoni imewadia Sudan kusini.

https://p.dw.com/p/zvJc
Raia wa Sudan Kusini mjini Juba.Picha: AP

Baada  ya  miaka  50  ya  mzozo  ulioleta  maafa makubwa,   watu  wa  Sudan  ya  kusini  hatimaye wanapiga  kura  hii  leo  kuamua  iwapo  waendelee  kuwa sehemu  ya  Sudan  moja  ama  kujitenga  na  kuwa  taifa la  193  duniani. Mpendwa  msikilizaji  natumai  kuwa  nawe kwa  muda  wa  dakika  hizi tano  kuangalia  maandalizi  ya siku  hii  ya  kihistoria  katika  bara  la  Afrika.

Upigaji  kura  unaanza  rasmi  saa  kumi  na  mbili  asubuhi katika  siku  saba  za  kwanza  za   upigaji  kura  katika kura  ya  maoni  ambayo  ni  ya  kihistoria   ambayo  ni kilele  cha   makubaliano  ya  amani   ya  mwaka  2005  kati ya  upande  wa  kaskazini  na  kusini   na  kumaliza  vita vilivyochukua  muda  mrefu  zaidi  katika   bara  la  Afrika.

NO FLASH Sudan Referendum
Mabango yenye ujumbe wa uhuru Sudan kusini.Picha: AP

Hali  ya  shauku  imeukumba  mji  mkuu  wa  eneo  la kusini  wa  Juba   katika  mkesha  wa  upigaji  kura  wakati watu  wa  eneo  hilo  wakifurahia  kujitokeza  kwa   saa  za mwisho  za  mzozo  uliochukua  muda  mrefu  na wakati mwingine  ulioonekana  kuwa  mgumu.

Mcheza  sinema  nyota   kutoka  Marekani  George Clooney  amejiunga  na  viongozi   waliopo  madarakani  na wale  wa  zamani  wa  mataifa   ikiwa  ni  pamoja  na seneta  mwandamizi  wa   bunge  la  Marekani  John Kerry , rais  wa  zamani  wa   Marekani  Jimmy  Carter  na   katibu mkuu  wa  zamani  wa  umoja  wa  mataifa  Kofi  Annan katika  mji  huo  kwa  ajili   ya  siku  hii  muhimu  kwa  watu wa  Sudan  ya  kusini.

Lakini  sherehe  hizo  zilichafuliwa  kidogo  na  mapigano kati  ya  makundi  ya  kikabila  yenye  silaha  pamoja  na wanamgambo  waliojitenga   katika  maeneo  mawili yanayozalisha  mafuta  katika  mpaka  wa  kaskazini  na kusini  maeneo  ambayo  yalikuwa  yakigombaniwa   katika vita  vya  wenyewe  kwa  wenyewe  vya  mwaka  1983  hadi 2005.

Rais  wa   kusini  mwa  Sudan  Salva  Kiir  amewaambia watu  wa  eneo  hilo  katika  mkesha  wa  kupiga  kura kuwa   hakuna  kitu  mbadala   ila  kuishi  kwa  amani  na upande  wa   kaskazini   wa  Sudan.

Amesema   kuwa , tumebakiwa  tu  na  saa  chache kufanya  uamuzi  muhimu  katika  maisha  yetu. Hii  leo hakuna  nafasi  ya  kurejea  katika  vita, amesema  katika hotuba  yake  kabla  ya  kuanza  kwa  kura  hiyo  ya  maoni.

Mjumbe  wa  Marekani  alikuwa  akiongoza  juhudi  za kimataifa  za  kidiplomasia  hadi  katika  dakika  za  mwisho kuhakikisha   kuwa   kura  hiyo  ya  maoni  inafanyika kama  ilivyopangwa  chini  ya  makubaliano  hayo. Mjumbe wa  Marekani  nchini  Sudan  Scott  Gration  amefanya ziara  24  katika  eneo  hilo  katika  juhudi  hizo  za kidiplomasia.

Mzozo  huu  baina  ya  eneo  la  kaskazini  ambalo  wakaazi wake  wengi  ni  Waarabu , Waislamu  na  upande  wa kusini  ambao  wengi  ni  Waafrika  weusi , na  ambao  ni Wakristo, umeigawa  Sudan  tangu  nchi  hiyo  kupata uhuru  kutoka  Uingereza  mwaka  1956, ukichochewa  na udini, ukabila, siasa  na  rasilmali, hususan  mafuta.

Wasudan ya  kusini  wanapiga   kura  hii  ya  maoni wakiwa  katika  sehemu  mbali  mbali, ambazo  ama wamekimbilia  wakati  wa   vita, ama  wamehamia  wakati mwingine. Miongoni  mwa  sehemu  ambapo  kura  ya maoni  inafanyika  pia  ni  nchini  Kenya, ambako  kuna Wasudan ya  kusini  wapatao  200,000. Nilizungumza  na mwandishi  wetu  habari   kutoka  Nairobi  Kenya  Alfred Kiti  kuhusu  hali  ilivyo  na  wapiga  kura  wanatarajiwa kuanza  saa  ngapi  kupiga  kura.

Mwandishi: Sekione Kitojo/AFPE

Mpitiaji: Maryam Abdalla