1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya maoni Sudan

8 Januari 2011

Matayarisho yamekamilika kwa kura ya maoni.

https://p.dw.com/p/zuzq
Harakati za upigaji kura ya maoni.Picha: picture alliance/dpa

Wajumbe nchini Sudan kutoka nchi zenye nguvu ambazo zilihusika katika kupatikana mkataba wa amani wa mwaka 2005, walikuwa katika harakati za mwisho za shinikizo la kidiplomasia katika mji mkuu nchini humo kuhakikisha hakuna hitilafu za dakika ya mwisho kwenye kura muhimu ya maoni ya wiki nzima ya Sudan kusini inayoanza hapo kesho.

Msemaji wa tume inayoandaa kura hiyo ya maoni,George Maker Benjamin, amesema matayarisho yamekamilika  na makaratasi ya kupiga kura yamewasili katika vituo vyote vya upigaji kura Kusini.

Marufuku rasmi ya kufanya kampeni imeanza baada ya kukamilika mikutano ya hapo jana.

Mjini Khartoum mjumbe wa marekani Scott Gration amekutana na maafisa wa serikai na waandalizi wa kura hiyo ya maoni walio chini ya usimamizi wa Senata John Kerry wa Marekani kuhakikisha kwamba hakuna hitilafu zozote katika kutekelezwa kwa mkataba huo amani .

Magari yaliokuwa na rangi za bendera ya Sudan yalionekana katika mji wa Juba  hapo jana, kuzidisha shauku ya kura hizo zitakazo baini iwapo Sudan ya kusini itaamua kujitenga na kuwa taifa huru.

Rais wa Sudan Omar el Bashir amesema wananchi wa Sudan ya kusini watatizamwa kuwa wageni walio na faida fulani iwapo eneo hilo la kusini litapiga kura kuwa huru katika kura ya maoni ya hapo kesho jumapili.

Dschuba al-Baschir
Rais Omar al-Bashir.Picha: dapd

Katika mahojiano kwenye kituo cha televisheni cha Al Jazeera hapo jana, Bashir amesema kwa sababu kusini itaamua kwamba Sudan igawanyike kuwa mataifa mawili, na Sudan Kusini liwe taifa huru, amesema hakuna maelezo yoyote kuwa Wasudan Kusini watakuwa na haki na faida sawa Sudan kaskazini.

Alipoulizwa iwapo Wasudan kusini watakuwa wageni Sudan kaskazini lakini kwa faida fulani, Bashir aliitika ndio bila ya kufafanuwa zaidi. Kura  ya maoni ya Sudan kusini ya kuamua iwapo watataka kujitenga na kuwa taifa huru hapo kesho, inajiri kutokana na mkataba wa amani wa mwaka 2005 uliomaliza miongo kadhaa ya vita vya ndani kati ya Kaskazini na Kusini, na huenda ikasababisha taifa hilo lililokubwa barani Afrika kugawanyika.

Rais Bashir amesema asilimia 20 ya ajira katika sekta ya umma hivi sasa, katika jeshi, usalama,na kiraia, zimeshikiliwa na Wasudan Kusini.

Mwandishi: Maryam Abdalla /Afpe

Mhariri:Halima Nyanza