1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya maoni ya Sudan Kusini kufanyika kesho

Mohamed Dahman8 Januari 2011

Kura hiyo itaamua iwapo Sudan Kusini ijitenge na Kaskazini na kuwa taifa huru. Hata hivyo, kura hiyo tayari imegubikwa na hofu baada ya watu sita kuuawa.

https://p.dw.com/p/zvE7
Rais wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir (Kulia) na kiongozi wa Sudan Kusini, Salva Kiir.Picha: picture-alliance/dpa

Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan amesema kwamba Sudan Kusini haiko tayari kwa uhuru na kama matokeo inaweza kukabiliwa na ukosefu wa utulivu.

Bashir ametowa onyo hilo wakati shamrashamra za furaha zikiwa zimegubika Sudan Kusini ambapo wananchi wake wanajiandaa kupiga kura hiyo ya maoni kudai uhuru wa jimbo lao na kuwapa fursa ya kujitenga na Sudan Kaskazini baada ya miongo mitano ya mzozo wa maafa.

Wananchi wa Sudan Kusini kwa kiasi kikubwa wanatarajiwa kuunga mkono kwa kishindo kikubwa uhuru kutoka kwa ndugu zao wa kaskazini ambao wamepigana nao vita mara mbili.

Lakini al- Bashir katika mahojiano na kituo cha televisheni ya Kiarabu cha Al -Jazeera amesema taifa hilo jipya litapata tabu. Bashir anasema kusini inapata taabu kutokana na matatizo mengi. Imekuwa katika vita tokea mwaka 1959 na haina uwezo wa kuwahudumia wananchi wake au kuunda taifa au serikali.

Bashir anasema Wasudan Kusini wanaamini kwamba sababu ya mateso yao yote ni kudhibitiwa na Sudan Kaskazini na wanafikiri kwamba wataweza tu kuondokana na mateso hayo kwa kutenganisha kusini na kaskazini.

Rais Bashir ambaye ni mwanajeshi aliyeongoza vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe dhidi ya waasi kwa muongo mmoja na nusu kabla ya kufikia makubaliano ya mwaka 2005 amesema ana wasi wasi juu ya taathira itakayokabiliana nayo Sudan Kaskazini kutoka na matatizo ya Sudan kusini ambayo hayaepukiki.

Amesema iwapo kuna vita kwa jirani yako huwezi kuwa katika amani. Katika mahojiano hayo na Al Jazeera Bashir amesema Sudan kaskazini na Kusini zinaweza kuunganisha nguvu zao kwa kuwa na mfumo kama wa Umoja wa Ulaya iwapo kusini itaamuwa kujitenga.

Amesema wananchi wa Sudan kusini wanaweza kupewa ukaazi wa bure huko kaskazini,uhuru wa kwenda wanakotaka, haki ya kufanya kazi na kumiliki mali nchini Sudan baada ya kugawanyika kwa nchi hizo lakini hawatoweza kuwa na uraia wa nchi zote mbili.

Akifafanuwa zaidi Bashir amesema kwa hivi sasa hawazungumzii juu ya kuanzisha ulinzi wa pamoja bali wanajadili kuanzisha umoja kati ya washirika wawili kuangalia maslahi ya pamoja katika usalama,uchumi na maendeleo kama vile ilivyo katika Umoja wa Ulaya.

Hali Sudan Kusini ni ya furaha wakati uhuru uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu unakaribia na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR linasema kwamba watu wa Sudan kusini waliokimbilia kaskazini wakati wa vita hivi sasa wanarudi kwa kiwango cha watu 2,000 kwa siku.

Lakini wachambuzi wengi wameonya kwamba Wasudan kusini hawatokabiliwa na kipindi rahisi katika eneo la kimaskini lililoathiriwa na mapambano makali kati ya makabila yanayohasimiana.

Shirika la misaada la Uingereza la Oxfam limesema kwamba taifa hilo jipya litakabiliwa na changamoto kubwa mno na litahitaji msaada wa muda mrefu kutoka jumuiya ya kimataifa.

Melinda Young mkuu wa Oxfam huko Sudan kusini amesema umaskini sugu, ukosefu wa maendeleo na tishio la umwagaji damu mambo ambayo yamevuruga matumaini ya maisha ya kila siku hayatatoweka baada ya kura hiyo ya maoni. Amesema bila ya kujali matokeo masuala hayo yanahitaji kushughulikiwa.

Takriban watu milioni 4 watashiriki katika kura hiyo ya maoni ambayo imeamuliwa katika makubaliano ya amani ya mwaka 2005 ambayo yamekomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1983 hadi mwaka 2005 kati ya Waislamu walio wengi Sudan kaskazini na Wakristo walio wengi Sudan kusini.

Mzozo wa vita vya pili vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan umesababisha watu milioni mbili kupoteza maisha yao na wengine mamilioni kuachwa bila ya makaazi.

Al- Bashir katika wiki za karibuni ametuliza hofu ya kurudia tena kwa vita kwa kusema kwamba yuko tayari kukubali matokeo ya kura hiyo ya maoni lakini baadhi ya watu wana wasi wasi kwamba masuala yaliokosa ufumbuzi bado yanaweza kuzusha mzozo mpya.

Mpaka wa kusini na kaskazini ambao unagawa maeneo ya machimbo ya mafuta nchini Sudan bado haukukamilishwa sawa na hatima ya eneo la Abyei lenye utajiri wa mafuta ambalo lazima liamuwe liungane na kaskazini au kusini.

Kura hiyo inayoanza kupigwa hapo kesho inatarajiwa kumalizika hapo tarehe 15 na ili kwamba matokeo yake yahesabiwe kuwa yamefana asilimia 60 ya waliojiandikisha kupiga kura wanatakiwa wawe wamepiga kura wapige kura hiyo.

Habari zaidi zinasema kwamba watu sita wameuwawa katika mapigano kati ya waasi na wanajeshi wa jeshi la Sudan kusini. Mashambulio hayo ni ukumbusho wa mpasuko mkubwa uliopo katika eneo hilo la kusini lisilo na maendeleo ambalo linakabiliwa na mauaji ya kikabila na uporaji wa mifugo.

Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini-SPLA, Philip Aguer amesema kuwa vikosi vyake viliwashambulia wapiganaji wanaomuunga mkono kiongozi wa waasi, Galwak Gai hapo jana na wapiganaji hao wakajibu mashambulizi hii leo. Aguer amesema kuwa wapiganaji hao wamekuja kutoka Kaskazini kwa ajili ya kuharibu uchaguzi wa kura ya maoni.

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa SPLA, jana waliwaua wapiganaji wawili na leo wamewaua wapiganaji wanne. Mara kwa mara viongozi wa Sudan Kusini wamekuwa wakiishutumu Sudan Kaskazini kwa kuwaunga mkono wapiganaji wanaojaribu kuvuruga kura hiyo ya kihistoria. Hata hivyo, viongozi wa Kaskazini wamekanusha shutuma hizo.

Mwandishi:Mohamed Dahman/AFP/RTRE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo