1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura zaendelea kuhesabiwa Ukraine

P.Martin1 Oktoba 2007

Matokeo ya mwanzo ya uchaguzi uliofanywa siku ya Jumapili nchini Ukraine,yaonyesha kuwa muungano wa vyama vinavyoelemea kambi ya magharibi vinaongoza.

https://p.dw.com/p/CH7N
Rais wa Ukraine Viktor Jushchenko na mkewe Kateryna wakipiga kura mjini Kiev
Rais wa Ukraine Viktor Jushchenko na mkewe Kateryna wakipiga kura mjini KievPicha: AP

Kwa hivi sasa,kundi la waziri mkuu wa zamani,Yulia Tymoschenko linatia fora.

Baada ya kuhesabiwa asilimia 60.5 ya kura zilizopigwa siku ya Jumapili,kundi la Yulia Tymoschenko linaongoza kwa asilimia 34,likifuatwa na Viktor Janukovich aliepata asilimia 31 huku Rais Viktor Yushchenko akidunduliza asilimia 16 kwa hivi sasa.

Lakini wingi wa vyama vinavyoelemea kambi ya magharibi unaweza kupunguka.Kwani sasa Halmshauri ya Uchaguzi imeanza kuhesabu kura zilizopigwa maeneo ya mashariki ya Ukraine ambayo humuunga mkono Viktor Janukovych.Vyama vya kikomunisti na kisoshalisti ni muhimu sana kwa Janukovych,kwani kwa kushirikiana na vyama hivyo vidogo tu ndio ataweza kuzuia serikali ya Rangi ya Chungwa inayoelemea kambi ya magharibi.Hata hivyo mwenyekiti wa chama cha „Ukraine Yetu“ ana matumaini ya kuunda serikali.Lizenko amesema:

„Hata ikiwa vyama vya kidemokrasia vitakuwa na wingi wa mbunge mmoja tu,basi kwa msaada wa mbunge huyo tutaunda serikali ya kidemokrasia.“

Lakini Yanukovich anasema,matokeo rasmi bado hayakutangazwa kwa hivyo si jambo la dhamana kusema cho chote kabla ya hapo.

Ni dhahiri kuwa mrembo Tymoshenko anapania kumrithi Yanukovich kama waziri mkuu,na hivyo kurejea kwenye wadhifa alioshika kufuatia Mapinduzi ya Rangi ya Chungwa,na kuja kutimuliwa na Yushchenko miezi saba baadae.Tymoshenko anaejulikana kwa hotuba zake za uchochezi ameshasema,anataka kuunda serikali mpya pamoja na Yushchenko katika kipindi cha siku mbili zijazo.

Uchaguzi wa Jumapili uliitishwa mapema,kwa matumaini ya kumaliza mgogoro kati ya Rais Yushchenko na Waziri Mkuu Yanukovych.Huo ni uchaguzi wa tatu kupata kufanywa nchini Ukraine katika kipindi cha miaka mitatu.Kwa mujibu wa tume ya wasimamizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya,uchaguzi huo umetimiza viwango vya Ulaya vinavyokubalika.

Jumuiya ya kimataifa inangojea kwa hamu matokeo ya uchaguzi huo kwani Marekani,Umoja wa Ulaya na Urusi zinapania kuwa na ushawishi nchini Ukraine-taifa lililoeleza kuwa lina hamu ya kujiunga na Umoja wa Ulaya na NATO.Ukraine iliyokuwa jamhuri ya zamani ya Soviet Union,inajaribu kufanya mageuzi ya kiuchumi na kisiasa mfano wa nchi za Magharibi.