1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kusoma nchini Ujerumani

3 Machi 2011

Kwa wanafunzi walío nje na wanaotaka kuendelea na masomo yao nchini Ujerumani, kuna njia nyingi zinazowapa fursa ya kuongeza elimu yao kwa kiwango chochote wanachokitaka, kuanzia digrii ya kwanza, ya pili hadi udaktari.

https://p.dw.com/p/10A09
Kusoma nchini Ujerumani
Kusoma nchini Ujerumani

Taratibu za kujiunga na vyuo vikuu nchini Ujerumani


Mwanafunzi yeyote wa kigeni anayetaka kusomea Ujerumani, ni lazima afahamu masharti ya kuingia Ujerumani tangu akiwa nchini kwao. Afisi ya Wanafunzi wa Kigeni hukagua nyaraka zote kuhakikisha kwamba zinatimiza masharti yaliyowekwa.

Kwa mfano, ikiwa vyeti vya nchi inayohusika vinatambuliwa nchini Ujarumani. Endapo hali si hivyo, kuna uwezekano wa mwanafunzi kujiunga na "Studienkolleg" ili ajiimarishe kabla ya kujiunga na chuo kikuu.

Taarifa za ziada kuhusu kusajiliwa, masharti ya lugha na nyaraka nyingine zinazohitajika kwa maombi ya nafasi ya kusoma, zinapatikana kutoka Shirika la Msaada wa Masomo la Kijerumani (DAAD). Ni lazima nakala za nyaraka zote zipigwe mihuri ya kuziidhinisha na pia zitafsiriwe kwa lugha ya Kijerumani..

Marekebisho ya Bologna


Katika mwaka 1999 mawaziri wa elimu wa mataifa 29 ya Ulaya, ikiwemo Ujerumani, waliamua kuufanya mfumo wa elimu uwiane katika Ulaya nzima. Mojawapo ya marekebisho ilikuwa kuanzishwa kwa shahada za digrii za "Bachelor" na "Master". Kwa sasa hivi mataifa 40 yanashughulikia marekebisho haya ya mfumo wa elimu barani Ulaya.

Vitabu mbalimbali vya kujifunzia lugha ya Kijerumani
Vitabu mbalimbali vya kujifunzia lugha ya KijerumaniPicha: picture alliance/dpa

Uamuzi huo wa mawaziri unatarajiwa kuafikiwa kikamilifu kufikia mwaka 2010. Ingawa mataifa mengi yanakabiliwa na matatizo ya kutimiza lengo hilo, mchakato mzima wa marekebisho unatarajiwa kukamilika kufikia mwaka 2020.


Masomo ya lugha ya Kijerumani


Mwanafunzi anayenuia kusomea nchini Ujarumani masomo ambayo hayasomeshwi kwa lugha ya Kiingereza, anapaswa kujifunza lugha ya Kijerumani. Kuna aina tofauti tofauti za mitihani ya lugha kwa mfano DSH, yaani "Deutsche Sprachprüfung für den Hochschulzugang ausländischer Studienbewerber".

Neu: Mallorca ACHTUNG: NUR FÜR STUDIEREN IN DEUTSCHLAND VERWENDEN!

Tangu akiwa nchini kwao, mwanafunzi anaweza kufanya mtihani wa "TestDaF" maanake (Test Deutsch als Fremdsprache). Wale ambao wamesomea shule za Kijarumani au wana stashahada za Taasisi ya Goethe hawahitajiki kufanya mtihani.

Vyeti vya lugha ya Kijarumani vinavyohitajika katika vyuo vikuu nchini Ujarumani vinapatikana katika Taasisi za Goethe kote ulimwenguni.

Huduma kwa Wasomi wa Kigeni


Taasisi zinazolenga kuwapata wanasayansi na watafiti wa kutajika ni lazima zijitahidi kuwa na upekee wa aina fulani. Vyuo vikuu vya Ujerumani vinapowakaribisha wasomi vinawapa pia fedha za kutunza watoto na pia vinawasaidia kuwatafutia wake au waume zao nafasi za kazi katika miji yao mipya.

Kazi zenyewe zinaweza kuwa katika chuo kikuu kinachohusika au kwenye shirika linaloshirikiana na chuo kikuu hicho.

Masomo pamoja na kazi


Baadhi ya vyuo vikuu na vyuo vya kawaida nchini Ujerumani vinashirikiana na makampuni kutoa mafunzo ambapo wanafunzi hupata uzoefu wa kikazi wa moja kwa moja wakati bado wakiendelea na masomo yao. Kazi na mazoezi ni vitu viwili vinavyoambatana.

Mwanafunzi anayekamilisha aina hii ya mafunzo hupata tajriba ya kikazi na pia shahada ya chuo kikuu.

Vyuo Vikuu vya Kisomi


Nchini Ujarumani kuna vyuo vikuu tisa vilivyopewa sifa ya "Vyuo Vikuu vya Kisomi" kutokana na ufanisi wake katika nyanja ya utafiti na mipango ya siku za usoni.

Lengo la Serikali ya Ujarumani la mwaka 2005/2006 kuvitangaza vyuo hivyo kuwa vya kisomi lilikuwa kuvifanya vijulikane na viwe na nafasi ya ushindani katika ulingo wa kimataifa.

Kufikia sasa vyuo vilivyoteuliwa ni Chuo Kikuu cha Ufundi (TU) cha Munich, Chuo Kikuu cha Ludwig Maximilian cha Munich, RWTH cha Achen, Chuo Kikuu huru (FU) cha Berlin pamoja na vyuo vikuu vya Heidelberg, Goettingen, Karlsruhe, Freiburg na Konstanz. Vyuo Vikuu hivyo huwasilisha kwenye kurasa zao za wavuti miradi vinayotarajia kuafikia siku zijazo.

Vyeti tofauti tofauti

Hapo awali wanafunzi wa shahada za "Magister" na "Diplom" na pia waliojifunza ualimu walikuwa wakijichagulia na kujiamulia fungu la masomo waliyotaka kusoma.

Shahada ya "Magister" ilihitaji masomo matatu, mtihani wa kitaifa ulihitaji masomo matatu na shahada ya "Diplom" ilihitaji somo moja. Kwenye mfumo wa masomo ya shahada za "Bachelor" na "Master", mwanafunzi kimsingi anatakikana kusoma somo moja. Vyuo vikuu vingi tayari vinafundisha mafungu ya masomo yanayotegemeana kimaudhui na pia kulingana na mahitaji kwenye uwanja wa ajira.

Kutokana na hali hii, mafungu mengi ya masomo yameanzishwa na bado yakianzishwa. Taarifa zaidi kuhusu habari za masomo zinapatikana kwenye ukurasa wa wavuti wa www.hochschulkompass.de.

Masomo katika mtandao

Mpango wa masomo kupitia mtandao wa tovuti unawavutia sana watu ambao tayari wanafanya kazi kwa kuwa si lazima kwao kuhudhuria madarasa. Vyuo vikuu nchini Ujerumani vimekuwa mbioni kufundisha shahada hizo za mtandaoni na mara nyingine wanafunzi kutoka mataifa ya kigeni wanaweza kujisajili kusoma masomo hayo kupitia vyuo vikuu vya nchini kwao.

Chuo kikuu cha pekee kinachotoa mafunzo ya mtandaoni ni Chuo Kikuu cha Hagen katika jimbo la North Rhine Westphalia. Mafunzo hayo yanahusu masomo ya uchumi na biashara na wanafunzi hupata masomo kupitia mtandao wa tovuti au hupelekewa masomo kwa njia ya barua.

Wanafunzi na walimu wao wanawasiliana kila wakati na kutokea mahali kokote. Wanafunzi kutoka mataifa ya kigeni wanaweza pia kushiriki kwenye mpango huu wa masomo.

Msaada wa kifedha

Mwanafunzi yoyote anayeingia Ujerumani bila msaada wa masomo, ni lazima athibitishe kwamba ana fedha za kutosha kujisimamia kimasomo katika mwaka wake wa kwanza. Mwanafunzi huyo anahitajika kuhifadhi kiasi Euro elfu nane (8,000 €) kwenye akaunti ya akiba ya benki. Msaada wa kifedha wa serikali wa masomo hutolewa kwa raia wajerumani au wakati mwingine kwa raia wa mataifa ya Ulaya.

Kulingana na kifungu cha sheria kuhusu elimu na mafunzo katika taifa la Ujerumani (BAföG), serikali inaweza kuwafadhili wanafunzi ikiwa wazazi wao hawawezi kuwakimu kimasomo. Mwanafunzi anayekabiliwa na matatizo ya kifedha anaweza kushauriana au kutafuta msaada kupitia shirika la huduma kwa wanafunzi ama " Studentenwerk" au jumuiya za vyuo vikuu.


Ithibati ya kutimizwa kwa masharti

Baadhi ya masomo yanamhitaji mwanafunzi anayetaka kujisajili kuthibitisha kwamba amekamilisha " grundstaendiges Studium" maanake shahada au cheti cha msingi. Kwa wakati huu vyeti au shahada zinazotambuliwa ni "Bachelor", "Diplom", "Magister" au mtihani wa Kitaifa.

Kujisajili

Ni lazima kwa mwanafunzi kujisajili kwa masomo anayotaka kusoma kwenye chuokikuu kinachohusika. Kimsingi, kila mwanafunzi ana hiari ya kuchagua chuo kikuu na wahadhiri anaowataka. Vyuo vikuu vya kibinafsi, vyuo vya sanaa na muziki na pia vyuo vya michezo huamua wanafunzi vinaowasajili kwa kuwafanyia mitihani au mahojiano.

Kwa masomo yanayowaniwa na wanafunzi wengi kuna utaratibu maalumu wa kuwachagua kutegemea alama wanazopata katika mtihani wa mwisho wa shule ya upili.

Mwanafunzi anayetaka kujisajili ni lazima ajaze fomu zinazohusika na pia athibitishe kwamba anafahamu Kijerumani (kwa masomo yanayosomeshwa kwa lugha ya Kijerumani), awasilishe nyaraka kuthibitisha ikiwa alihitimu chuo kikuu chochote nchini kwao. Ni lazima pia awe na bima ya afya. Aidha mwanafunzi anatakikana kulipa karo ya muhula.

Kiwango maalumu cha alama (Numerus Clausus)

Kwenye masomo ambayo yanawaniwa na wanafunzi wengi, kuna kiwango maalumu cha alama kinachoweka kudhibiti idadi ya wanafunzi. Kiwango hicho kinaitwa "Numerus Clausus".

Ni wanafunzi wanaofikisha kiwango cha alama kilichowekwa wanaosajiliwa. Wanafunzi wa kigeni hawazingatiwi kwenye utaratibu wa kiwango hiki cha "Numerus Clausus" kwa kuwa wengi wao huingia Ujerumani kwa kufadhiliwa na pia kuna taratibu nyingine zilizotengwa kutathmini viwango vyao.


Vyama vya Wanafunzi

Kuna kiasi vyama 58 vya wanafunzi wa vyuo vikuu vinavyoshughulikia masuala ya wanafunzi. Vyama hivyo vinashughulikia makazi, vinagharamia shughuli za mikahawa ya vyuo vikuu, vinatoa huduma kwa watoto wa wanafunzi na pia vinajumuishwa kwenye harakati za vyuo vikuu kwa maslahi ya wanafunzi.

Ada

Vyama hivyo vya wanafunzi hupata kiasi fulani cha fedha zinazotokana na ada ya wanafunzi. Ada pia hutumiwa kugharamia shughuli za usimamizi wa vyuo vikuu, na pia taasisi za utetezi wa wanafunzi yaani "AStA".

Wanafunzi wote wanapaswa kulipa ada wanaposajiliwa. Baadhi ya majimbo yameanzisha utaratibu wa wanafunzi kulipa karo ya ziada ya Euro 500 kila muhula.


Usajili wa pili wa wanafunzi

Vyuo vikuu vina jukumu la kuwateua baadhi ya wanafunzi miongoni mwa idadi kubwa ya wanafunzi wanaoomba kusajiliwa kwa masomo maarufu.

Wanafunzi hupeleka maombi ya kusajiliwa kwa vyuo vingi kwa wakati mmoja huku wakisubiri kupata nafasi katika vyuo wanavyovipenda zaidi miongoni mwa vyuo walivyopeleka maombi. Mwanafunzi anapopewa nafasi ya kujiunga na chuo kikuu, nafasi hiyo haiwezi kufutwa kabla ya muhula kuanza bila ya ridhaa ya mwanafunzi mwenyewe.

Wakuu wa vyuo vikuu mbalimbali waliamua kuanzisha shughuli ya jumla ya kuchunguza na kujaza nafasi za masomo zilizoachwa wazi kwenye vyuo vikuu vyao. Nafasi za usajili wa pili wa wanafunzi hupatikana kila mwanzo wa muhula kwenye ukursasa wa wavuti: www.freie-studienplaetze.de.

Vile vile, kuna ukurasa mwingine wa wavuti Studieren.de. ambao unashughulika na maswala ya vyuo vikuu ambapo habari mpya hupatikana mara kwa mara.

Aidha majuma machache kabla ya mwisho wa muhula mwanafunzi anaweza kupata taarifa kuhusu nafasi za masomo kupitia www.studieren.de/freie-studienplaetze.

Wanafunzi walemavu

Vyama vya wanafunzi vinafadhili vituo vya kuwasaidia wanafunzi walemavu. Baadhi ya vyuo vikuu vimejengwa kwa kuzingatia maslahi ya walemavu.

Vyama vya wanafunzi pia hutetea kuweko mabweni yasiyo na vizuizi vinavyowatatiza wanafunzi walemavu. Kila chuo kikuu huajiri msimamizi wa maswala ya wanafunzi walemavu. Vyuo vikuu vina vyama vinavyowashauri na kuwasaidia wanafunzi walemavu na wasio walemavu.

Wanafunzi walio na watoto

Vyama vya wanafunzi (Studententwerk) pia huwasaidia wanafunzi walio na watoto. Vyama hivyo huwasaidia wanafunzi hao kutafuta makazi, shule za chekechea na pia walezi wa watoto.

Vyuo vikuu vinavyotaka kuwavutia wasomi au wanafunzi wa kiwango cha juu kutoka kote ulimwenguni mara nyingi huwa na vivutio maalumu kwa wasomi na wanafunzi hao.

Miongoni mwa vivutio hivyo ni kuwatafutia mahali pa kutunziwa watoto wao, shule zinazofaa na pia makazi. Taarifa zaidi zinapatikana kwenye Afisi ya Wanafunzi wa Kigeni (Akademisches Auslandsamt).

Kituo cha kuwakaribisha wanafunzi wa kigeni

Mwanafunzi yeyote wa kigeni anayejiunga na chuo kikuu chochote nchini Ujerumani anaweza kuwasiliana na Afisi ya Wanafunzi wa Kigeni (Akademisches Auslandsamt) kwa ushauri na msaada wowote anaohitaji.

Juu ya hayo, baadhi ya vyuo vikuu vina vituo vya kuwakaribisha wanafunzi wa kigeni. Vituo hivyo pia huwaunganisha wanafunzi wapya na wale wa zamani ili kuwasaidia kuyaelewa vizuri mazingira yao mapya.

Baadhi ya vyuo vikuu huwa na shughuli ya juma zima ya kuwatambulisha wanafunzi maeneo ya miji na habari kuhusu nchi pamoja na wakazi wake.

Aidha idara zinazohusika huandaa shughuli za kutoa maelekezo kwa wanafunzi wapya mwanzoni mwa muhula.

Masharti ya usajili


Baadhi ya masomo yanayowaniwa na wanafunzi wengi yamewekewa idadi maalumu ya wanafunzi. Kwa mfano wanaotaka kusomea utabibu (udaktari) alama wanazopata kwenye mtihani wa mwisho wa shule ya upili zinazingatiwa sana pale wanaposajiliwa kwa masomo hayo.

Kila mwanafunzi anapaswa kupeleka maombi yake binafsi katika chuo kikuu anachotaka kujiunga nacho. Taarifa za ziada kuhusu masomo na jinsi ya kuandika barua ya maombi zinapatikana kwenye vyuo vikuu vinavyohusika.

Ni bora kwa wanafunzi kupeleka maombi kwenye vyuo vikuu mbali mbali. Afisi ya Wanafunzi wa Kigeni ya kila chuo kikuu ndiyo inayotoa nafasi za masomo kwa wanafunzi wa kigeni.

Mwanafunzi anayetaka kupeleka maombi ya nafasi za usajili katika vyuo vikuu vingi kwa wakati mmoja, anaweza kutumia huduma za mtandaoni za ukurasa wa wavuti wa "Arbeits- und Servicestelle für Internationale Studienbewerbungen" yaani www.uni-assist.de/english.

Kiungo hicho kinatoa huduma ya kuzipitia nyaraka za wanafunzi waliopeleka maombi ya nafasi za masomo ili kuhakikisha kwamba wana nyaraka zote zinazohitajika. Nyaraka hizo baadaye huwasilishwa kwenye vyuo vikuu vinavyohusika.


Mwandishi: Gaby Reucher
Tafsiri: Omar Babu
Mhariri: Mohammed Khelef