1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kutawazwa Barack Obama kama rais wa 44 wa Marekani

Miraji Othman21 Januari 2009

Barack Obama, rais wa kwanza wa Marekani mwenye asili ya Kiafrika

https://p.dw.com/p/GdNg
Barack Obama na mkewe, Michelle, wakielekea kanisani kabla ya Barack Obama kuapishwa kuwa rais wa 44 wa MarekaniPicha: AP

Ilikuwa inangojewa kwa hamu kubwa, nakusudia hotuba ya Barack Obama alioitoa jana pale alipoapishwa akisimama juu ya ngazi za jengo la Bunge la Marekani mjini Washington. Rais huyo mpya alisema Marekani, katika siku za mbele, lazima ichukuwe juhudi zaidi za kuukiuka mzozo ambao nchi yake inakabiliana nao. Aliwatia moyo Wamarekani, na hasa wale wenye asili ya Kiafrika.

Mamilioni ya watu huko Marekani na duniani kote waliingojea siku ya jana. Kwa Barack Obama kula kiapo kama rais wa wa 44 wa Marekani, nchi hiyo sasa imepata uso mwengine, tena uso ulio mpya. Uso huo hautakuwa kaidi, wenye kuangalia tu njia iliojichagulia, bila ya kujali hasara itakayopatikana. Huo utakuwa uso utakaoangalia kulia na kushoto, utakaotilia barabara maanani maoni ya marafiki na pia wahakiki. Uso huo utawaangalia mahasimu usoni na pia kuwakaribia kidogo. Enzi ya Marekani kujiamulia tu yenyewe peke yake mambo ya kisiasa imekwisha. Hotuba ya rais huyo mpya wa Marekani pia ilikuwa ni yenye kuachana wazi wazi na siasa za mtangulizi wake, George Bush.

Barack Obama aliwataka wananachi Wamarekani, katika kujitahidi kuwa na usalama, wasiachane na zile thamani za Kimarekani. Ule ukweli kwamba Marekani ni dola ilio na nguvu kubwa za kijeshi, haina maana kwamba iweze kufanya inavyopenda. Rais huyo alitangaza kwamba ataongozwa na maarifa ya kiutaalamu kuliko na nadharia. Kutokana na imani hiyo, ndio maana wafuasi wake wamemchaguwa. Katika hotuba hiyo aliyaweka wazi na kuyatetea yale anayotaka yafanyike na pia matarajio ya ulimwengu uliobaki.

Wakati huo huo, Barack Obama, katika masuala kadhaa, ameyapunguza matumaini yaliowekewa kipindi cha utawala wake. Hamna mtu atakayeweza kuyatamiza, kwani mzozo ulioko sasa ni mkubwa, matataizo yalioko ni ya aina mbali mbali. Lakini yeye hataacha kubeba dhamana. Kuwaondosha wanajeshi wa Kimarekani kutoka Iraq kwa njia ya mpangilio, kuleta amani nchini Afghanistan, kupunguza silaha za kinyukliya, kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani- yote hayo, katika hotuba yake ya kwanza kama rais, ameahidi kuyashughulikia.

Karibuni lazimaBarack Obama atapimwa kutokana na mafanikio au angalau maendeleo yatakayopatikana katika masuala hayo, na hasa kabisa kuitatua hali mbaya ya kiuchumi ambayo Marekani inakabiliana nayo hivi sasa.

Ameweka wazi katika hotuba yake kwamba yeye peke yake hataweza kuyatanzuwa mambo yote hayo. Hivyo amewataka wananchi wa Marekani wajioandae barabara, kila mmoja anatakiwa kufanya hivyo. Hivyo, Obama anafuata njia zilizotumiwa na marais wa kabla, John F. Kennedy na Franklin D. Roosevelt.

Sura hii mpya ya Marekani hauangalii tu njia nyingine, lakini uso huo ni wa rangi nyingine. Ni karibu miaka 60 iliopita, alisema Obama katika hotuba yake, baba yake alikataliwa kuhudumiwa katika mikawa mingi. Sasa jambo kama hilo haliko tena, na hali hiyo imemfanya alishukuru taifa lake katika juhudi za kufikia ile fikra za kimsingi za waasisi wa taifa hilo. Kwa Wamarekani wenye asili ya Kiafrika tukio la Obama kuchukuwa wadhifa huo linawapa matumaini, ambayo wengi wao walikuwa hawayaamini.

Mapambano ya Wamarekani wenye asili ya Kiafrika kuwa na haki sawa hayajamalizika. Bado Wamarekani weusi wana vipato vilivyo chini, ukilinganisha na wenzi wao Wamarekani weupe, bado watoto weusi katika nchi hiyo wanapata mafunzo yasiokuwa mazuri shuleni, ukilinganisha na wenziwao weupe. Hata hivyo, ile ndoto ya mwanaharakati wa haki za kiraia, marehemu Martin Luther King, pale alipoongoza maandamano mjini Washington ambapo aliezea juu ya umuhimu na haja ya kuishi pamoja kwa amani bega kwa bega baina ya watu weusi na weupe , ndoto hiyo imekaribia zaidi kutimia kutokana na tukio la jana la kuapishwa Barack Obama kuwa rais wa Marekani.