1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Air Hijack

Othman, Miraji27 Agosti 2008

Mkasa wa kutekwa nyara ndege ya Sudan

https://p.dw.com/p/F5lI
Ndege ya Sudan iliotekwa nyara, ikiwa katika kiwanja cha ndege cha Kufra, nchini LibyaPicha: AP

Watekaji nyara waliowashikilia abiria 100 ndani ya ndege ya Shirika la Sun la Sudan ilioko katika kiwanja cha ndege cha Kufra nchini Libya wamewaachilia mahabusu wao. Lakini watekaji nyara wawili na wafanya kazi saba wa ndege hiyo bado wamo ndani ya ndege hiyo, huku mashauriano yakiendelea. Hapo kabla abiria walipewa maji, lakini sio chakula, na wengine walizimia pale mtambo wa kutoa hewa baridi ndani ya ndege hiyo uliposhindwa kufanya kazi.

Hapo kabla ilitajwa kwamba walikuwemo abiria 95 na wafanya kazi saba ndani ya ndege hiyo.

Mkasa huo ulianza jana alasiri pale ndege hiyo ilipoondoka Nyala, mji mkubwa kabisa katika Mkoa wa Darfur, kuelekea mji mkuu wa Khartoum. Wakuu wa Libya waliiruhusu ituwe katika kiwanja cha kijeshi cha Kufra, kusini mashariki ya nchi hiyo, baada ya kuishiwa na mafuta.

Watekaji nyara wanadai kwamba wao ni kutoka Jeshi la Ukombozi la Sudan, ambalo kiongozi wake, Abdel Wahid Mohammed Nur, anaishi uhamishoni mjini Paris, na kwa mujibu wa rubani wa ndege hiyo, watekaji nyara wanafikia watu kumi au zaidi. Kwa mujibu wa mkurugenzi wa kiwanja cha ndege cha Kufra ni kwamba watekaji nyara wanakataa kuzungumza moja kwa moja na wakuu wa Libya. Wao wanataka wapatiwe ndege ya kuwapeleka Paris pamoja na mafuta.

Lakini mwenyewe Abdel Wahid Nur, ambaye kikundi chake ni moja kati ya makundi mawili muhimu ambayo yamekuwa yakipigana huko Darfur tangu mwaka 2003, alisema kwa njia ya simu kwamba wao hawahusiki na utekaji nyara huo. Naye Ibrahim al-Hillo, kamanda wa jeshi la Ukombozi la Sudan linaloongozwa na Abdel Wahid Nur, amesema kitendo hicho ni matokeo wazi ya ukanadamizi wanaofanyiwa watu waliopoteza makaazi katika Vita vya Darfur. Alisema majeshi ya serekaliy a Sudan yanauwa watu huko Darfur, na jamii ya kimataifa haijiingizi, kwa hivyo watu wa Darfur wafanye nini? Wanajeshi wa kuweka amani wa Umoja wa Mataifa huko Darfur wamesema watu 33 walizikwa jana kufuatia mapapmbano ya silaha baina ya polisi na watu wanaoishi katika kambi za wakimbizi katika mkoa huo.

Nayo serekali ya Sudan imewataka wakuu wa Libya kuwakamata na kuwarejesha Khartoum watekaji nyara hao iliowaita kuwa ni magaidi. Ilisema inalaani kitendo hicho na inawasiliana na kushauriana na wakuu wa Libya. Msemaji wa serekali alisema lengo kwanza ni kuhakikisha usalama na kuachiliwa huru Wa-Sudan wote waliomo ndani ya ndege hiyo, ikiwa pamoja marubani. Pili kuhakikisha kwamba watekaji nyara wanakabidhiwa serekali ya Sudan ili wafikishwe mbele ya sheria. Msemaji wa serekali ya Sudan alitoa mwito kwa jamii ya kimataifa ilaani kitendo hicho cha utekaji nyara, na akasema wakuu wa Libya wamekuwa wenye kutoa msaada katika kutafuta ufumbuzi.

Mjini Paris, waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Bernard Kouchner, amesema kila kitu kinazingatiwa ili kulinda maisha ya watu waliomo ndani ya ndege hiyo, japokuwa hajasema wazzi wazi kama Ufaransa itakuwa tayari kuipokea ndege hiyo.

Mzozo wa Darfur umepata makali tangu pale mwendeshai mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mwezi uliopita alipoomba apatiwe waranti kuwezesha kukamatwa Rais Omar al-Bashir wa Sudan, akituhumiwa kuendesha uhalifu wa kivita na kusababisha mauaji ya kimbari.

Umoja wa Mataifa unasema hadi watu laki tatu wameuwawa na zaidi ya milioni 2.2 wameyakimbia makkaazi yao tangu mzozo huo wa Darfur kuchipuka Febrauri mwaka 2003. Sudan inasema watu alfu kumi wameuwawa.