1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuteuliwa Gauck apiganie wadhifa wa Rais wa shirikisho

21 Februari 2012

Jinsi karata zilivyochanganywa na malengo ya kuteuliwa mwanaharakati wa haki za binaadam Joachim Gauck awe rais wa shirikisho ndio suala kuu lililochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

https://p.dw.com/p/146P8
Joachim Gauck na mwandani wake Daniela SchadtPicha: picture-alliance/dpa

Masuala ya kila aina yanajitokeza,mfano wa haya ya gazeti la mjini Ingolstadt la "Donaukurier" linalojiuliza:Kipi hasa muhimu:Kuteuliwa Joachim Gauck awe rais wa shirikisho au tathmini ya suala,imekwenda kwendaje akachaguliwa, nani ataondoka patupu na nani atafaidika?Ili kuweza kugunduwa kile kinachowakera wananchi wengi katika pirika pirika za kisiasa,na mkiruhusu,kipi kinawaudhi katika vyama vya kisiasa, basi yote hayo majibu yake yalibainika katika mkasa wa jumapili usiku.Mara tu baada ya mgombea kupatikana,mashindano yakaanza upya kama kawaida kupitia vyombo vya habari,lengo likiwa watu kujitafutia faida,wao pamoja na vyama vyao.Hadhi na hishma ya wadhifa huo-sifa ambazo kila kwa mara zilikuwa zikipigiwa upatu hadi Wulff alipong'atuka,zinaonyesha si muhimu tena.

Joachim Gauck / Nominierung / Bundespräsident
Joachim Gauck baada ya kuteuliwa kugombea wadhifa wa raisPicha: dapd

Gazeti la Financial Times Deutschland linampima mteule mmwenyewe wa kiti cha rais na kuandika:Joachim Gauck si mtu ambae atakapokuwa rais wa shirikisho atatilia maanani nani kamfanyia nini.Na hasa SPD na walinzi wa mazingira Die Grüne wataduwaa jinsi mgombea wao atakavyokuwa,atakapokuwa rais wa shirikishgo.Mhafidhina zaidi pengine na shabiki mkubwa wa mfumo wa kibepari pengine kuliko vile ambavyo mashabiki wa Gauck kutoka vyama hivyo viwili vya SPD na Die Grüne wanavyopendelea awe.Na jasiri kuliko wengi kati ya mameneja.Hali hiyo imebainika alipotetea Ajenda 2010 na jinsi alivyokosoa vuguvugu la wanaopinga mtindo wa benki kuzidi kujitajirisha.Hata raia wa shirikisho watabidi wajirekebishe:hakutakuwa tena na vivutio na urembo katika kasri la Bellevue-badala yake kutakuwa na kipaji -sifa itakayoinufaisha Ujerumani.

Gazeti la "Sächsische Zeitung" la mjini Dresden linahisi hakujakuwa na haja ya kumtafuta mwengine:Kipaji chake mwenyewe ndicho sababu za kuteuliwa kwake na sio kwamba alikuwa mchamungu wa kutoka Mashariki na mpigania uhuru.Gauck amejipatia umaarufu mkubwa kutokana na kugombea nafasi hiyo mwaka 2010 na pia na juhudi zake za kila wakati za kuhutubia kuhusu mada tofauti.Yote hayo yamemsaiadia kugeuka kipenzi cha umma na kuzusha suala;Kwanini achaguliwe mwengine ikiwa kuna mgombea ambae sehemu kubwa ya jamii,maskini na tajiri,mashariki na mashariki wanamthamini na kumtaka agombee wadhifa huo?

Deutschland Joachim Gauck
Joachim GauckPicha: dapd

Na gazeti la Neue Presse la mjini Hannover linasema Ujerumani inahitaji rais na sio mbabe:Gauck ni mgombea anaeheshimika,mwenye wasifu wa kuvutia,mhafidhina mwenye kiu cha uhuru,lakini si mbabe.Na mtu kama huyo hahitajiwi.Ujerumani haitaki kuokolewa.Inahitaji rais tu ambae atakuwa huru,hatoelemea upande wa chama chochote na ambae atakiwakilisha kwa hadhi na muruwa cheo chake cha urais.Kiongozi atakaetambua mada gani zitawafaa wananchi,na vipi kufikia nyoyo za wananchi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman