1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwa heri Ujerumani Uefa Euro 2012

Admin.WagnerD29 Juni 2012

Hayawi hayawi hatimaye yalikuwa, moto uliwaka usiku wa jana mjini Warsaw kufuatia mchuano mkali baina ya Ujerumani na Italia. Italia ili ndiyo ilikuwa mbabe zaidi baada ya kuibuka na ushindi wa bao 2-1.

https://p.dw.com/p/15NtE
Italien feiert in Bonn.jpg Fotograf: Thomas Klein für DW Thema: Torjubel nach dem 1:0 beim Public Viewing Ort: Bonn, Friesdorf Datum: 27.6.2012
Picha: Thomas Klein

Ni kijana mwenye umri wa miaka 21 ndiye aliyeufanya usiku wa jana (28.6.2012) kuwa mchungu kwa Wajerumani baada kwa kufunga mabao yote mawili ya timu yake.

Namzungumzia Mario Balloteli ambaye bila mzaa aliweza kumuacha kwenye mshangao mlinda mlango wa Ujerumani Manuel Neuer kwa kuziona nyavu zake mara mbili katika kipindi cha kwanza. Bao lake la kwanza alilipata kwenye dakika ya 20 baada ya kupata pasi kutoka kwa Antonio Cassano.

Italia wakishangilia moja ya mabao yao dhidi ya Ujerumani
Italia wakishangilia moja ya mabao yao dhidi ya UjerumaniPicha: AP

Hakuishia hapo kwani dakika ya 36 aliandika bao la pili kwa timu yake kutokana na pasi ndefu ya Riccardo Montolivo iliyompita Nahodha Phillip Lahm hadi nyavuni na hivyo kuzidi kuwaweka Wajerumani kwenye wakati mgumu. Ni wakati wa lala salama, dakika nne za nyongeza ndipo Ujerumani ilipojitutumua kupitia penati iliyopigwa na Mesut Özil ambayo ilikuwa kama kifuta machozi kwao.

Juhudi za Ujerumani kusaka tiketi ya fainali

Mchezo kwenye dakika hizo za mwisho ulikuwa ni wa vuta nikuvute huku Ujerumani wakionekana kuongeza makali lakini wapi, ilikuwa ni sawa na kukumbuka shuka wakati alfajiri imeshafika.

Wachezaji wa Ujerumani wakiwa katika taharuki baada ya kipigo cha 2-1
Wachezaji wa Ujerumani wakiwa katika taharuki baada ya kipigo cha 2-1Picha: AP

Ujerumani hakikuweza kufua dafu mbele ya Waitaliano licha ya kuingia dimbani ikiwa na mbadailiko kadhaa yaliyofanywa na Kocha wake Joachim Loew. Nia ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kumdhibiti mchezaji wa Italia Andrea Pirlo pamoja na kuongeza nguvu ya mashabulizi.

Baadhi ya wakati ilionekana kupoteza mwelekeo na hivyo kutoa kitisho dhaifu kwa Italia hasa upande wa kulia licha ya kuwepo Jerome Boateng upande huo.

Italia: Tuliujua udhaifu wa adui yetu

Kwa upande wao Waitaliano wao walikuwa makini hasa kwenye safu ya mashambilizi na mchezaji wake Pirlo ambaye alifanya kazi kwa utulivu kama kawaida yake nyuma ya Daniele De Rossi Montolivo na Claudio Mrchisio.

Kocha wa Italia Cesare Prandelli anasema kuwa walijiandaa vya kutosha na mchezo wa jana. " Tulijuwa Wajerumani ni wazuri kwenye kujilinda. tulitaka kuumiliki mpira na tufanye maajabu kupitia safu yetu ya kati. Siku zote tunakuwa na mtu ambaye yuko huru kati na tuliweza kumtumia Cassano kufanya kazi yenye matunda." alisema kocha huyo mara baada ya kumalizika mchezo huo.

Naye Joachim Löw alizungumzia kuhusu mabadiliko aliyoyafanya kwenye kikosi chake na kusema alimrejesha Gomez kwa sababu alikuwa amefunzwa vilivyo akaiva na ameonyesha kuwa kwenye mstari kwa kufunga mabao matatu kwenye kinyangányiro hichi cha UEFA EURO 2012. Löw alisema pia kuwa Toni Kroos aliingia ili waweze kuumiliki mpira katika eneo la kati.

Joachim Löw, Kocha wa timu ya Taifa ya Ujerumani
Joachim Löw, Kocha wa timu ya Taifa ya UjerumaniPicha: Reuters

Italia au Uhispania Uefa Euro 2012?

Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani Juergen Klinsmann, ambaye alifanya kazi na Löw kama msaidizi wake kwenye fainali za kombe la dunia mwaka 2006 amesema kuwa Italia ilishinda mchezo wa jana kwa kupitia mashambilizi yake ya katikati. Amesema eneo hilo ndio udhaifu uliowaponza Ujerumani kwenye mchezo huo.

Wakiwa nafasi ya tatu kwenye fainali mbili zilizopita za kombe la dunia, na kulikosa taji la mabingwa barani Ulaya mwaka 2008, haya ni mashindano ya nne mfululizo ambayo Ujerumani angalau imeweza kufika nusu fainali.

Sasa kibarua kimebaki kwa Italia itakayochuana na Uhispania mabingwa watetezi siku ya Jumapili (Julai Mosi) mjini Kiev, Ukraine. Waitaliano wana matumaini kuwa huenda historia ikajirudia na kunyakua taji hilo la UEFA EURO 2012 kama ilivyokuwa mwaka 2006.

Kikosi cha Uhispania kwenye fainali za Uefa Euro 2012
Kikosi cha Uhispania kwenye fainali za Uefa Euro 2012Picha: dapd

Bila shaka hata Wahispaniola nao wana ndoto pia za kulitwaa taji hilo la ubingwa barani Ulaya. Ni nani atakayetimiza ndoto yake na yupi ataishia kuota tu? Jibu litapatikana siku hiyo ya Jumapili kule mjini Kiev, Ukraine.

Mwandishi: Stumai George/ DPAE/AFPE