1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"kwa njia hiyo mvutano hautatatuliwa"

26 Septemba 2007

Alipozungumza jana mbele ya mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa, rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad alisema mzozo huu wa mradi wa kinyuklia wa nchi yake umeisha. Wakati huo huo aliulaumu Umoja huu kwa kufuata sera za kuweka vikwazo dhidi ya Iran inayoitishwa na “nchi fidhuli” kama alivyosema Ahmadinejad. Kabla ya rais huyu hajaanza kutoa hotuba yake, ujumbe wa Marekani uliondoka katika chumba cha mkutano kama kutoa ishara ya upinzani wake. Hiyo lakini siyo njia ya kutatua mizozo, anasema mwandishi wetu Peter Philipp.

https://p.dw.com/p/CH7d

Katika historia ya Umoja wa Mataifa kuna hotuba nyingi ambazo zinakumbukwa vizuria kama zile za Nikita Christshow na Fidel Castro, Yasser Arafat na Hugo Chavez. Lakini rais Mahmoud Ahmadinejad anapopanda jukwaa si tukio la aina hii tena. Yale anayosema na namna anavyozungumza, yaani kwa kiburi na kwa ukaidi, kwa kuonyesha hasira na kutetea dini – yote haya yanajulikana awali, na huenda wale ambao Ahmadinejad anawalenga kuyaambia haya hawamsikii tena. Hususan jamii ya Marekani ambayo Ahmadinejad alitaka kuifumbua macho na kuwaambia Wamarekani aina nyingine ya ukweli ambao hawajawahi kuusikia.

Lakini si tu Ahmadinejad pekee ambaye anatumia vibaya fursa ya kuwepo mkutano huu. Vilevile Marekani na nchi za Ulaya zimeonyesha kuwa hazina chombo chochote cha kumshinikiza Ahmadinejad. Hayo yalikuwa wazi pale Ahmadinejad alipoalikwa na chuo kikuu cha Columbia ambapo ushujaa wa kumwalika mgeni huyu maarufu uliharibika mara moja baada ya kumwita mgeni “dikteta mdogo asiyeona mbali” wakati wa kumkaribisha. ´

Utendaji huu uliendelea hivyo hivyo kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa. Rais Sarkozy wa Ufaransa hakufuta kabisa uwezekano wa kuishambulia Iran na Kansela Merkel wa Ujerumani aliarifu kwamba si ulimwengu unaopaswa kutoa ushahidi kuhusu mradi wa kinyuklia wa Iran, bali ni Iran yenyewe inayofaa kujieleza. Hoja hiyo lakini haina msingi wala wa kisiasa wala wa kisheria. Hata hivyo, sura iliyotolewa ni kwamba nchi za Ulaya pamoja na Marekani zina msimamo wa pamoja dhidi ya Iran.

Licha ya hiyo lakini, misimamo haiambatani kabisa. Ikiwa Umoja wa Mataifa utazungumzia upya suala la kuiwekea vikwazo Iran, nchi za Ulaya bila shaka zinakuwa na maoni mbalimbali. Nyingi kati yao zina maslahi fulani ya kiuchumi. Kwa Marekani ni rahisi kuweka vikwazo kwa sababu biashara yake na Iran si kwa njia rasmi. Ujerumani ilipunguza kiwango cha bidhaa zinazouzwa Iran, Ufaransa lakini haijachukua hatua wazi.

Na je, hayo yote ni kwa sababu Iran inalaumiwa kufanya kitendo ambacho hakina ushahidi? Kwa kutumia mbinu hii, nchi za Magharibi zinampa Ahmadinejad sababu nzuri kuigawa dunia kati ya nchi bora na nchi mbaya. Hiyo haitamsaidia yeyote, si Marekani wala Iran. Ila tu ni hatua ya busara pale Ahmadinejad aliposema mzozo juu wa mradi wa kinyuklia umeisha kwa sababu serikali yake imeahidi kwamba inafanya uchunguzi wa nishati ya kinyuklia kwa azma ya matumizi ya amani.

Kwa vyovyote vile lakini, kwa njia hiyo, mvutano hautatatuliwa. Ikiwa pande zote mbili zinataka kweli kutafuta suluhisho, inabidi ziwe na mawazo bora zaidi.