1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ladislas Ntaganzwa akamatwa

Daniel Gakuba10 Desemba 2015

Meya wa zamani na mmoja kati ya watuhumiwa wakuu tisa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, Ladislas Ntaganzwa, amekamatwa akituhumiwa kwa kuwachinja maelfu ya watu na kuandaa ubakaji wa jumla mwaka 1994.

https://p.dw.com/p/1HLQq
Tangazo la kusakwa kwa Ladislas Ntaganzwa.
Tangazo la kusakwa kwa Ladislas Ntaganzwa.Picha: Getty Images/AFP

Kukamatwa kwa Ntaganzwa mwenye umri wa miaka 53 kumetangazwa na Kitengo cha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (MICT) na kwa mujibu wa kitengo hicho, mtu huyo anakabiliwa na mashitaka ya kuchochea mauaji dhidi ya maelfu ya watutsi katika maeneo mbali mbali, na pia kuhamasisha watu kufanya madhambi mengine kama ubakaji na uhalifu mwingine wa kingono.

Watu zaidi ya laki nane waliuawa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994, wengi wao wakiwa kutoka jamii ya watutsi, katika mauaji ya maangamizi ambayo kwa sehemu kubwa yalifanywa na wale wa jamii ya wahutu.

Mpango wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani wa kutoa zawadi kwa waliowakamata washukiwa wa uhalifu wa kivita, ulikuwa umetangaza kitita cha dola milioni tano kwa upande utakaosaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.

Ingawa MICT haikutoa maelezo zaidi kuhusu kukamatwa kwa Ntaganzwa, mkuu wa idara ya Rwanda ya kuwasaka washukiwa wa mauaji ya kimbari wanaojificha nje ya nchi, John Bosco Siboyintore, ameiambia DW kwamba Rwanda imetoa ushirikiano katika mchakato huo.

''Umekuwepo ushirikiano kati ya idara yetu Rwanda na kitengo cha mahakama ya kimataifa ya uhalifu. Nisingependa kuzungumza mengi kuhusu mazingira ya kukamatwa kwake, lakini cha muhimu zaidi ni kwamba hatimaye ametiwa mbaroni', alismea Siboyintore.

Watuhumiwa wengine bado hawajapatikana

Watuhumiwa wengine wakuu wanane wa mauaji hayo mabaya ya Rwanda bado wanaendelea kujificha miaka 21 baada ya kufanyika mauaji hayo. Hao ni pamoja na aliyekuwa mfanyabiashara maarufu, Felcien Kabuga, Mwanajeshi Augustin Bizimungu, Protais Mpiranya na Fulgence Kayishema. Wengine ni Pheneas Munyarugarama, Aloys Ndimbati, Ryandikayo na Charles Sikubwabo.

Ntaganzwa aliyekamatwa alikuwa akitafutwa na Mahakama ya Kimataifa kwa ajili ya Rwanda iliyokuwa na makao yake mjini Arusha, lakini mwaka 2012 faili la kesi yake lilihamishiwa katika mahakama za Rwanda, na baada ya kukamatwa kwake, mkuu wa kitengo cha mahakama ya kimataifa ya uhalifu Bubacar Jallow, ameiomba Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo kumkabidhi kwa Rwanda.

Jallow ameiomba Kongo kumsafirisha mtuhumiwa huyo kwenda Rwanda bila kukawia. Mkuu wa idara ya Rwanda ya kuwasaka watuhumiwa wa mauaji ya kimbari amesema Rwanda haijui lini Kongo itafanya hivyo.

Baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, inaripotiwa kuwa Ntaganzwa alikimbilia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati huo ikiitwa Zaire, na kwamba amekuwa akifichwa na waasi wa Rwanda wa FDLR wanaonuia kuiondoa madarakani serikali mjini Kigali.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Mafuvu na mifupa ya wahanga wa mauaji ya maangamizi nchini Rwanda.
Mafuvu na mifupa ya wahanga wa mauaji ya maangamizi nchini Rwanda.Picha: Getty Images/C. Somodeville