1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LAGOS: Nigeria yakataa kambi ya kikosi cha Marekani barani Afrika

20 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CP1i

Rais wa Nigeria, Umaru Yar ´Adua, amesema hatakubali nchi yake itumiwe kama kambi ya jeshi la Marekani barani Afrika, AFRICOM.

Gavana wa jimbo la Kwara, Bukola Saraki, amesema rais Yar´Adua amesisitiza Nigeria haitakubali kambi ya jeshi la Marekani kujengwa katika ardhi yake, lakini ataunga mkono juhudi za kuunda kikosi cha Afrika kitakachotumiwa wakati haja ikitokea.

Gavana Sakari ameyasema hayo baada ya rais Yar ´Adua kukutana na viongozi wa zamani na wa sasa wa Nigeria.

Naibu waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, John Negroponte, aliitembelea Nigeria wiki iliyopita kuzungumzia mpango wa kuanzisha kikosi cha AFRICOM akisema kinaendana na sera ya ulinzi ya Marekani.

Serikali ya Marekani ilitangaza mwanzoni mwa mwaka huu kwamba wizara ya ulinzi itajenga makao makuu ya kikosi cha Marekani barani Afrika kuratibu maslahi ya kijeshi na kiusalama ya Marekani barani humo.