1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LAGOS:Chama kimoja cha upinzani chakataa kujiunga na serikali

6 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBlJ

Chama kimoja kikubwa cha upinzani nchini Nigeria kinakataa kujiunga na serikali ya Rais mpya wa Nigeria Umaru Yar’Adua kwa madai kuwa uchaguzi uliopita ulifanyika kinyume na sheria.

Rais Yar’Adua alivikaribisha rasmi vyama vitatu vikuu vya upinzani kujiunga na serikali yake katika juhudi za kuondoa hisia kwamba uchaguzi wa mwezi Aprili iliyopita haukuwa halali.Kulingana na waangalizi wa Umoja wa Ulaya uchaguzi huo hauaminiki.

Chama kikuu cha upinzani nchini Nigeria All Nigeria Peoples Progressive Party ANPP na chama kidogo cha Peoples Progressive Alliance,PPA vimekubali kujiunga na serikali.Chama cha Action Congress AC kiliamua kujiondoa baadaa ya mvutano wa ndani kutokea.

Bwana Yar’Adua alitangazwa kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa kwanza wa kupokezana uongozi kutoka kiongozi wa kiraia kinyume na ilivyokuwa awali kutoka viongozi wa kijeshi.

Wapinzani wakuu wa Rais Yar’Adua ni kiongozi wa kijeshi wa zamani Muhammadu Buhari wa chama cha ANPP na makamu wa rais wa zamani Atiku Abubakar wa chama cha AC.Viongozi hao wawili wako mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo.