1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lawama za kisiasa zajengeka nchini Pakistan

17 Agosti 2007

Marekani inalaumiwa kwa kujiingiza katika maswala ya ndani ya Pakistan huku taarifa zikiashiria kwamba taifa hilo kubwa linajaribu kutafuta mbinu za kugawana madaraka kati ya rais Parvez Musharaf na hasimu wake mkubwa aliyekuwa waziri mkuu wa zamani bibi Benazir Bhutto ambae yuko uhamishoni nchini Uingereza.

https://p.dw.com/p/CH9R
Rais Parvez Musharraf wa Pakistan
Rais Parvez Musharraf wa PakistanPicha: AP

Habai kutoka duru zote za kiserikali na upande wa upinzani hata hivyo zimepuuza taarifa hizo na kukanusha kwamba Washington inamtia kishindo kiongozi wa kijeshi wa Pakistani Jenerali Parvez Musharraf juu kufikia makubaliano ya kisiasa kati yake na waziri mkuu wa zamani bibi Benazir Bhutto kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Msemaji wa serikali amesema kwamba raia wa Pakistan ndio wana jukumu la kumchagua kiongozi wanaempenda kwa hivyo sio haki kuanza kubeba mbeleko kabla mwana hajazaliwa hatua ambayo naibu waziri wa habari wa Pakistan Tariq Azeem anasema ni sawa na kuwadhihaki wapiga kura wa nchini mwake.

Gazeti la Marekani la New York Times liliripoti jana kwamba Marekani inajadili mabadiliko ya kisiasa na viongozi wenye ushawishi mkubwa nchini Pakistan na wakati huo huo kutafuta uwezekano wa kugawana madaraka kati ya rais Musharraf na bibi Benazir Bhutto.

Kwa mujibu wa taarifa za gazeti hilo ni kwamba waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza Rice alizungumza kwa simu na jenerali Musharraf juu ya pendekezo la kugawana madaraka na bibi Bhutto wiki iliyopita huku likiwanukuu maafisa wa Marekani na pia wa Pakistan.

Awali ikulu ya Marekani ilisema kwamba maafisa wake wa ngazi za juu walikutana na wanasiasa kujadili juu ya kuwepo hali ya kisiasa yenye msimamo wa kadiri nchini Pakistan na vile vile kuhusu maswala ya uchaguzi huru na wa haki nchini humo.

Bibi Bhutto inaarifiwa kuwa alikutana na jenerali Parves Musharraf mwezi uliopita katika Falme za nchi za Kiarabu na baadae akakutana na maafisa wa serikali ya rais George .W. Bush wa Marekani ikiwa ni pamoja na mjumbe wa Marekani katika umoja wa mataifa Zalmay Khalilzad.

Maafisa hao wa Marekani wana imani kwamba ushirikiano wa kisiasa kati ya rais Musharraf na bibi Benazir Bhutto utamsaidia rais huyo wa Pakistan kubakia madarakani hata ingawa anaendelea kupoteza umaarufu nchini mwake.

Lakini si rais Parvez Musharraf au bibi Benazir Bhutto hata mmoja wao hajakiri kuwa wamewahi kukutana.

Benazir Bhutto kiongozi wa chama cha Pakistan Peoples Party amesema kuwa ana nia ya kurejea nyumbani kushiriki katika uchaguzi na amemtolea mwito jenerali Musharraf kung’atuka kutoka kwenye uongozi wa kijeshi.

Raja Zafarul Haq, kiongozi wa ngazi ya juu wa chama cha kisiasa cha waziri mkuu mwingine wa zamani Nawaz Sharif amesema hali hiyo inaonyesha jinsi gani mambo ya ndani ya Pakistan yalivyoingiliwa katika kipindi cha miaka minane cha utawala wa kidikteta wa jenerali Parvez Musharaf.

Amesema kuwa nia ya Marekani ni kuona kuwa vyama vya ambavyo vinatenganisha dini na siasa vinaungana na rais Musharraf ili kuvunja nguvu ya vyama vya kiislamu vinavyo pinga ushawishi wa Marekani katika sera zake za nje.