1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leicester City waendelea kuongoza Premier League

2 Februari 2016

Leicester City imeendelea kushika usukani wa ligi ya Premier ya England wakati kalenda ikibadilika kuwa mwezi wa Februari. Manchester City na Arsenal zinawafwata unyounyo vijana hao wa kocha Claudio Ranieri

https://p.dw.com/p/1HnQd
Fußball Manchester United gegen Leicester City Barclays Premier League
Picha: Getty Images/L. Griffiths

Mbweha hao walitarajiwa kujikwaa wakati msimu ukiendelea lakini hali haijakuwa hivyo hadi sasa na wanaongoza kwa pointi tatu juu ya msimamo wa ligi hiyo ngumu barani Ulaya wakifuatiwa na Machester City na Arsenal London.

Leicester City inakumbana na kikosi na kocha nyota Juergen Klopp kesho Jumanne wakianza mbio zinazoweza kuwa mtihani kwa uwezo wao.

Mchezo huo utafuatiwa hata hivyo na pambano dhidi ya Manchester City na kisha Arsenal hali itakayoondoa mlundikano wa michezo katika sehemu ya juu ya msimamo wa ligi.

Vipigo viwili dhidi ya Mbweha hao msimu huu vimetoka Liverpool na Arsenal na mlinzi wa Leicester City Christian Fuchs anasema hali hiyo ni somo kubwa na motisha kwa siku zijazo.

Manchester City ama Arsenal zinaweza kuchukua usukani wa ligi hiyo iwapo zitashinda michezo yake ya ligi. Manchester City inakwenda kupambana na Sunderland, wakati Arsenal inakumbana na Southampton.

Arsenal ilipokea kipigo cha kugaragazwa baada ya Krismass mwaka jana kwa kuchapwa mabao 4-0 na Southampton na timu hiyo inaingia katika pambano hilo ikiwa kifua mbele kuiangusha tena Arsenal.

Tottenham itakuwa na kibarua na Norwich, Manchester United inakumbana na Stoke City, West Ham iko nyumbani ikiisubiri Aston Villa, Crystal Palace ina miadi na Bournemouth na Swansea ni wageni wa West Bromwitch, wakati Watford inakuwa mwenyeji wa Chelsea na Newcastle wanakwenda kwa Everton siku ya Jumatano.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga