1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leipzig yaiduwaza Leverkusen

Bruce Amani
19 Novemba 2016

RB Leipzig ilipata iliendeleza rekodi katika historia yake kwa kunyakua pointi tatu baada ya ushindi wa 3-2 dhidi ya Bayer Leverkusen na kuiondoa Bayern Munich kileleni mwa Bundesliga

https://p.dw.com/p/2Svu2
Bundesliga Leverkusen gegen leipzig
Picha: Getty Images/Bongarts/A. Grimm

Vijana hao wapya katik Bundesliga, ambao sasa hawajashindwa baada ya mechi 11 mfululizo, wana uongozi wa pengo la pointi tatu kileleni mbele ya Bayern Munich, ambao watachuana na Borussia Dortmund Jumamosi jioni katika mpambano wa vilabu vikuu vya Ujerumani – maarufu kama "Der Klassiker”.

"Kutoka kwa mtazamo wa kisaikolojia, tulifayna vyema sana katika kipindi cha pili wakati tulikuwa nyuma mara mbili”, alisema kocha wa Leipzig Ralph Hasenhuettl.

Kevin Kampl akisherehekea bao lake la ufunguzi
Kevin Kampl akisherehekea bao lake la ufunguziPicha: picture alliance/AP Photo/M. Meissner

Baada ya kubadilishana magoli katika dakika nne za mwanzo – Kevin Kampl wa Leverkusen akifunga bao baada ya dakika moja kabla ya mwenzake Julian Baumgartlinger kujifunga katika lango lake kuisawazishia Leipzig – winga wa Leverkusen anayechezea pia timu ya taifa ya Ujerumani Julian Brandt aliwaweka wenyeji kifua mbele tena muda mfupi tu kabla ya kipindi cha mapumziko.

Mambo yalichukua mkondo tofauti katika mchuano huo baada ya Brandt kupata penalty katika dakika ya 54 lakini mkwaju wa Hakan Calhanoglu ulipanguliwa na kipa wa Leipzig Peter Gulasci.

Mchezaji wa Uswisi Emil Forsberg aliisawazishia Leipzig baada ya kukimbia na mpira peke yake katika dakika ya 67 kabla ya beki Willi Orban kuwafungia vijana hao wapya katika Bundesliga bao la kichwa na la ushindi katika dakika ya 81.

Klabu hiyo, inayofadhiliwa na kampuni ya kinywaji cha kuongeza nguvu mwilini Red Bull, ina pointi 27 kutokana na mechi 11 huku mabingwa Bayern Munich wakiwa na 24.

Lakini vijana hao wapya wanakabiliwa na shinikizo kali kutoka kwa mashabiki wa timu pinzani wanaoamini kuwa wafadhili wa klabu hiyo wanahujumu wazo la kandanda la Ujerumani la kutokuwa kitu cha kufanyiwa matangazo ya kibiashara. Ijumaa usiku, basi la timu lilipakwa rangi wakati likielekea katika uwanja wa BayArena

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Caro Robi