1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leipzig yapepea, Bayern yayumba

Bruce Amani
21 Novemba 2016

RB Leipzig wamekamata usukani wa Bundesliga katika msimu wao wa kwanza katika ligi hiyo kuu ya kandanda hapa Ujerumani, wakati udhibiti wa Bayern Munich katika miaka ya karibuni ukionekana kudhoofika

https://p.dw.com/p/2T1XO
Bundesliga | Bayer 04 Leverkusen - RB Leipzig 2:3
Picha: picture-alliance/ZB/T. Eisenhuth

Bayern ilionja kichapo cha kwanza msimu huu na chao cha kwanza tangu mapema Machi wakati ilizabwa moja bila na Borussia Dortmund katika mchuano maarufu wa "Der Klassiker” Jumamosi jioni. Na beki wa Bayern Mats Hummels alikiri baadaye kuwa kiwango cha Bayern kimeonaka kupungua nah ii inatokana na mabadiliko ya mfumo wa makocha. "BVB ilikuwa imara leo, lakini sio kwamba tulikuwa timu dhaifu, lakini walifunga bao nasi tukakosa nafasi nyingi lakini bila shaka nilidhani ingekuwa tofauti, lakini kwa kuzingatia mchezo, ulikuwa mkali, wa hali ya juu na naamini ulikuwa mzuri sana".

Kocha wa Dortmund Thomas Tuchel ambaye alisherekea ushindi wake wa kwanza dhidi ya Bayern akiwa kocha wa Dortmund, alikiri baada ya mechi kuwa mpango wake wa kushambulia kwa kasi kwa kumuweka Mario Götze nyuma ya washambuliaji wawili ulifua dafu "Tuna furaha kubwa leo kwa sababu tulifanya kazi kubwa na kuteseka sana, lakini tukiwa na umoja, tulicheza kwa kujituma, nidhamu na tukawa na nafasi nzuri za kufunga"

Bayern ilionja kichapo cha kwanza msimu huu
Bayern ilionja kichapo cha kwanza msimu huuPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Bayern sasa wako katika nafasi ya pili kwa mara ya kwanza tangu Septemba 2015, pointi tatu nyuma ya Leipzig ambao walishinda 3-2 dhidi ya Bayer Leverkusen, ikiwa ni ushindi wao wa sita mfululizo na kujikusanyia pointi 27.

Hoffenheim ililazimika kutoka sare ya 2-2 dhidi ya wageni Hamburg. Sare hiyo ina maana kuwa Hoffenheim na Leipzig ndizo timu pekee ambazo hazijapoteza mchuano wowote kufikia sasa katika Bundesliga. Hoffenheim ilipata hadi nafasi ya tano na pointi 21 nyuma ya Borussia Dortmund na Cologne kwa tofauti ya mabao na mbele ya Hertha Berlin na Eintracht Frankfurt.

Frankfurt iliizaba Werder Bremen mabao mawili kwa moja. Borussia Moenchengladbach ilishindwa na Cologne mabao mawili kwa moja uhsindi ambao ulimridhisha kocha wa Cologne Peter Stöger "Tusisahau kuwa sisi ni timu inayocheza katika Bundesliga kwa mwaka wa tatu, na tulicheza dhidi ya timu ambayo inacheza katika Champions League na sio kwa sadfa, tulicheza sana. katika kipindi cha kwanza kilikuwa kigumu na kufikia sasa hakuna anayeweza kutupuuza, na hiyo ni habari njema".

Katika mechi hiyo Anthony Modeste aliifungia Cologne bao moja, lake la 12 msimu huu sawa na Pierre-Emerick Aubameyang. Schalke iliinyamazisha Wolfsburg kwa bao moja kwa sifuri, ikiwa ni ushindi wao wa kwanza ugenini msimu huu.

Kwingineko, Ingolstadt iliifunga Darmstadt moja bila, Mainz ikaizaba Freiburg 4-2 wakati Augsburg ikitoka sare ya 0-0 na Hertha Berlin.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef