1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lengo la kutokomeza Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria hatarini

18 Septemba 2023

Ripoti mpya iliyochapishwa leo na taasisi ya Global Fund inasema mabadiliko ya tabianchi na mizozo duniani vinatatiza juhudi za kimataifa za kupambana na magonjwa matatu hatari ambayo ni UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu.

https://p.dw.com/p/4WS5c
Dawa za kutibu kifua kikuu
Mizozo na mabadiliko ya tabianchi vinatatiza juhudi za kutokomeza Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria duniani Picha: Jekesai NJIKIZANA/AFP

Ripoti ya taasisi hiyo ambayo ni mfuko wa kimataifa wa kupambana na maradhi hayo matatu, inaonesha kwamba ijapokuwa miradi ya kupambana na Ukimwi, Malaria na Kifua Kikuu imerejea kote duniani baada ya kuathiriwa na janga la virusi vya corona, lakini hivi sasa inakabiliwa na vizingiti vinavyotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na mizozo.

Mkuu wa Taasisi ya Global Fund, Peter Sands, amesema majanga ya kimazingira mfano wa mafuriko yanaongeza idadi ya wagonjwa na kufanya vigumu matibabu kuwafikia.

Ongezeko la joto pia limefanya ugonjwa kama Malaria kusambaa hata kwenye maeneo ambayo kabla hayakuwa na visa vya maradhi hayo.

Afisa huyo amesema hali inayoendelea sasa inatishia malengo ya kutokomeza magonjwa hayo matatu ifikapo mwaka 2030.